Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-12-28 14:33:57    
Mazungumzo ya siku ya kwanza kati ya makatibu wa kidiplomasia wa India na Pakistan hayajapata maendeleo makubwa

cri
     Katibu wa kidiplomasia wa Pakistan Bw. Riaz Khokhar na katibu wa kidiplomasia wa India Bw. Shyam Saran wanaongoza ujumbe wao kushiriki katika mazungumzo hayo ya siku mbili, ambayo yatamalizika leo. Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Pakistan Bw. Masood Khan katika mkutano na waandishi wa habari alieleza kuwa, mazungumzo ya siku ya kwanza yalifanyika katika hali ya dhati ya moyo na kiujenzi. Alisema kuwa pande hizo mbili ziliangalia upya mazungumzo ya kipindi cha kwanza yaliyomalizika mwezi Septemba na mazungumzo mengine yaliyofanyika baadaye, na pande zote zimekubali kuendelea kusukuma mbele mchakato wa amani kati ya India na Pakistan. Kuhusu hatua za kujenga uaminifu wa nyuklia na silaha za kawaida, pande hizo mbili zilijadili mapendekezo yaliyokabidhiwa nao. Kabla ya mapendekezo hayo kupokewa, pande hizo mbili pia zitafanya ukaguzi na uchambuzi kwa kina.

     Katika mazungumzo hayo, pande hizo mbili pia zilijadili masuala mengine yakiwemo kupambana pamoja na biashara ya dawa za kulevya, suala la ardhi oevu kati ya nchi hizo mbili na kuanzisha safari za abiria kwa garimoshi kati ya mikoa ya Rajasthan na Sind na safari za abiria kwa basi kati ya miji mikuu ya Kashmir mbili, vilevile zilibadilishana maoni yao kuhusu kuwaachia huru wavuvi wanaofungwa, kubadilishana wafungwa na kuanzisha ubalozi mdogo katika Karachi na Mumbai.

     Baada ya mazungumzo hayo kumalizika, katibu wa kidiplomasia wa India Bw. Saran alikutana na waziri wa mambo ya nje wa Pakistan Bw. Khurshid Kasuri na kumwarifu hali ya mazungumzo hayo. Leo pande hizo mbili zitajadili suala la Kashimir.

     Ingawa mazungumzo ya jana hakujapata maendeleo makubwa, lakini maendeleo yapo. Bw. Masood Khan alidokeza kuwa, Pakistan itaendelea kutekeleza uamuzi wa upande mmoja wa kusimamisha vita katika sehemu ya Kashmir inayoidhibiti, na India imeeleza kuwa inapenda kupunguza jeshi lililoko katika Kashmir. Katibu wa kidiplomasia wa India Bw. Saran baada ya mazungumzo alisema kuwa, India itapanua eneo la kujenga uaminifu.

     Wazo la kuanzisha mchakato wa mazungumzo kati ya India na Pakistan lilitolewa na viongozi wa nchi hizo mbili waliposhiriki kwenye mkutano wa 12 wa wakuu wa umoja wa ushirikiano wa Asia ya kusini uliofanyika huko Islamabad mwezi Januari, mwaka 2004. Baada ya mchakato huo kuanzishwa mwezi Februari, mwaka 2004, pande hizo mbili zilifanya mazungumzo mengi ya ngazi ya wataalamu kuhusu masuala ya nyanja 8 yakiwemo suala la Kashmir, na makatibu wa kidiplomasia wa nchi hizo mbili pia walifanya mazungumzo mara nyingi. Mwezi Septemba, mwaka huu, pande hizo mbili zilimaliza mazungumzo ya kipindi cha kwanza, na kuanza duru la pili la mchakato wa mazungumzo. Kwa mujibu wa mpango uliowekwa, lengo la mazungumzo hayo ni kuangalia upya mazungumzo kabla ya hapo na kufanya maandalizi kwa mazungumzo ya siku za usoni.

     Kwa kuwa masuala kati ya nchi hizo mbili yana utatanishi, hivyo pande hizo mbili zote zilifuata hali halisi kuhusu matokeo ya mazungumzo hayo, lakini zote zilieleza kuwa zinapenda kuendelea kufanya mazungumzo ili kupata maendeleo makubwa. Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Pakistan Bw. Masood Khan alisema kuwa, kutatua mgogoro kati ya nchi hizo mbili, ambao umekuwepo kwa nusu karne si rahisi, hivyo inapaswa wapewe nafasi na muda wa kutosha. Katibu wa kidiplomasia wa India kabla ya mazungumzo hayo pia alieleza kuwa pande hizo mbili zinapaswa kuchukua hatua zenye unyumbufu. Wachambuzi wanaona kuwa nchi hizo mbili zilieleza kuendelea kufanya mazungumzo, hali hiyo yenyewe ni maendeleo. Mazungumzo yatasaidia kuimarisha uaminifu kati ya pande hizo mbili na kutatua masuala mbalimbali kati yao.

Idhaa ya kiswahili 2004-12-28