Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-12-28 14:44:29    
Mgombea wa urais wa chama cha upinzani Bw.Yushchenko atangaza kuwa ameshinda katika uchaguzi mkuu wa Ukraine

cri
    Duru la pili la upigaji kura wa uchaguzi mkuu wa Ukraine lilifanyika upya tarehe 26. Kutokana na takwimu za tume kuu ya uchaguzi wa Ukraine zilizotolewa asubuhi ya tarehe 27 kwa saa za huko, mgombea wa urais wa chama cha upinzani Bw. Victor Yushchenko amepata kura nyingi zaidi kuliko mgombea mwingine Bw. Viktor Yanukovych ambaye pia ni waziri mkuu wa Ukraine. Bw. Yushchenko ametangaza ushindi wake kwenye makao makuu ya uchaguzi mkuu.

    Duru la pili la upigaji kura kwenye uchaguzi mkuu wa Ukraine lilifanyika tarehe 21 mwezi Novemba. Tume kuu ya uchaguzi mkuu wa wakati huo ilitangaza kuwa Bw. Yanukovych alishinda kwa kura chache tu, lakini Bw. Yushchenko alikataa kushindwa na kuishutumu serikali ya Ukraine kuwa ilifanya vitendo vya udanganyifu katika upigaji kura huo. Wafuasi wa pande mbili walifanya maandamano na mkusanyiko mikubwa mara kwa mara na kusababisha mgogoro wa kisiasa katika nchi hiyo. Baadaye mahakama kuu ya Ukraine iliamuru kuwa matokeo ya upigaji kura ya tarehe 21 mwezi Novemba ni batili na kutangaza tarehe 26 mwezi Decembakuwa siku ya kufanya duru la pili la upigaji kura la uchaguzi mkuu.

    Kutokana na taarifa zilizotolewa na tume kuu ya uchaguzi mkuu wa Ukraine, wapiga kura milioni 37.40 walijiandikisha katika upigaji kura, na kulikuwa na vituo 32,118 vya kupiga kura na wachuuguzi 12,000 kutoka nchi za nje.

    Mgombea wa urais wa chama cha upinzani Bw.Yushchenko baada ya upigaji kura alisema kuwa, vipindi vya Bw. Leonid Kuchma na Bw. Yanukovych vimepita na Ukraine imeingia kipindi kipya cha siasa ya kidemokrasia. Alisema?" tunapaswa kukumbuka ushindi wetu wa siku hii na kuhifadhi ushindi huo ili kuimarisha uhuru na haki yetu. Bw. Yushchenko alionesha kuwa, maisha ya jamii ya Ukraine hayawezi kuamuliwa na Russia, Poland, Marekani au Ulaya, bali mustakabali wa Ukraine unapaswa kuamuliwa na wananchi wa Ukraine tu. Aliwataka wananchi wa Ukraine wajitahidi kufanya kazi kwa ustawi wa taifa lao.

    Mgombea mwingine wa urais wa Ukraine Bw. Yanukovych tarehe 27 usiku katika mkutano na waandishi wa habari huko Kiev alisema kuwa, hakukubali kushindwa katika uchaguzi huo, kwa sababu kulikuwepo na vitendo vingi vya kukiuka taratibu na matukio ya mauaji wa wapiga kura. Bw. Yanukovych alisema kuwa, atawaomba mahakimu wote wa mahakama kuu wasikilize kesi ya kukiuka taratibu katika uchaguzi huo, na anataka hatimaye mahakama kuu itangaze kuwa duru hili la upigaji kura ni batili. Anataka mahakama kuu na watu wanaohusika waweze kusuluhisha mgogoro huo kwa utaratibu wa sheria. Bw, Yanukvyoch alisema kuwa, hataongoza wafuasi wake kufanya maandamano makubwa, lakini huenda wafuasi wake watafanya harakati za upinzani huko Kiev kwa hiari yao.

    Kabla ya hapo, Bw. Yanukovych tarehe 26 baada ya upigaji upya kura kumalizika alikataa kushirikiana na watu wa kundi la Bw. Yushchenko. Aliviambia vyombo vya habari kuwa, ikiwa atashindwa, basi ataunda kundi jipya la upinzani na wafuasi wake, na kupinga mshindani wake na matokeo ya uchaguzi mkuu.

    Aidha, jumuiya ya kimataifa imetoa maoni tofautia kuhusu uchaguzi mkuu wa Ukraine. Wachunguzi kutoka nchi za magharibi kama Marekani walisifu uchaguzi huo, lakini wachunguzi kutoka Jamhuri huru kama Russia walishukia uchaguzi huo.

    Wachambuzi walionesha kuwa, ingawa mgombea wa urais wa chama cha upinzani wa Ukraine ametangaza kushinda katika uchaguzi mkuu, lakini mustakabali wa hali ya Ukraine bado haujulikani. Rais mpya wa Ukraine anakabiliwa na kazi ngumu ya kuendeleza uchumi wa nchi yake na kulinda mshikamano wa jamii na kuendeleza uhusiano kati yake na nchi za nje.

Idhaa ya kiswahili 2004-12-28