Tarehe 27 Israel iliwaachia huru wafungwa 159 wa Palestina. Vyombo vya habari wanaona kuwa hiki ni kitendo kingine ambacho viongozi wa Israel walikifanya kuonesha urafiki kwa Palestina, na kwa kiasi fulani kitendo hiki kitasaidia uchaguzi mkuu wa Palestina kufanyika salama mnamo Januari 9 mwakani.
Katika siku hiyo, wafungwa hao wa Palestina walipanda bas la Israel wakiwa chini ya uangalizi wa askari wa Israel na kupelekwa mpaka kwenye vituo vya polisi vilivyoko kwenye ukingo wa magharibi wa Mto Jordan na sehemu ya Gaza, kisha walipanda basi la Palestina na kupelekwa hadi kivuko cha mji wa Palestina, huko waliachiwa huru, walijiunga na jamaa na marafiki zao waliokuwa wakiwasubiri huko.
Kutokana na maelezo ya Israel, kati ya wafungwa walioachwa huru, 113 walifungwa kwa tuhuma za kuhatarisha usalama wa Israel katika mgogoro wa miaka minne iliyopita kati ya Palestina na Israel, wengine 46 walikamatwa kutokana na kuingia nchini Israel kinyume cha sheria. Israel ilisema kuwa imewaachia wafungwa hao kwa sababu hawahusiki moja kwa moja na mashambulizi dhidi ya raia wa Israel, na wamekaribia kumaliza kutumikia vifungo vyao.
Mwenyekiti wa Kamati ya Utendaji ya Chama cha Ukombozi cha Palestina Bw. Abbas tarehe 27 alionesha kukaribisha kitendo hicho cha Israel na alitaka Israel iwaachie huru wafungwa wote wa Palestina. Alisema kuwa Palestina inataka Israel iendelee kuwaachia huru wafungwa wengine. Waziri mkuu wa serikali ya mamlaka ya Palestina Bw. Qurei pia alisema, anatumai Israel itawaachia huru wafungwa wote wa kisiasa wa Palestina.
Imefahamika kuwa Israel imewafunga Wapalestina 7,000 gerezani, na hatima yao siku zote inawatia wasiwasi watu wa Palestina. Hivi sasa kampeni ya uchaguzi mkuu inapofanyika, Abbas ameingiza juhudi za kupigania uhuru wa wafungwa wa Palestina katika kampeni yake, Bw. Abbas pia anatumai kuvishawishi vikundi mbalimbali vya upinzani vya kijeshi vikubaliane na Israel kusimamisha vita kwa ufanisi wake huo.
Ingawa wafungwa walioachiwa huru sio wengi na wafungwa hao sio wakubwa kama Palestina inavyotarajia, lakini pia inasaidia Abbas kupata wapiga kura wengi zaidi na heshima kubwa zaidi, na pia inasaidia kujenga imani kati ya Palestina na Israel. Waziri mkuu wa Israel Sharon katika siku hiyo pia alisema kuwa kuwaachia huru wafungwa hao kunamaanisha matumaini mema ya Israel kufanya usuluhishi kuhusu mpango wa upande mmoja wa Israel. Msemaji wa serikali ya Israel pia alisema kuwa kama Palestina itatekeleza ahadi zake na kupambana na watu wenye siasa kali, na kufanya mageuzi ya kiserikali, Israel itawaachia huru wafungwa wengi zaidi wa Palestina.
Licha ya kuwaachia huru wafungwa wa Palestina, serikali ya Israel tarehe 26 iliidhinisha mfululizo wa hatua ili uchaguzi mkuu ufanyike salama katika sehemu ya ukingo wa magharibi wa Mto Jordan, sehemu ya Gaza na sehemu ya mashariki ya Jerusalem. Hatua hizo ni pamoja na Israel kuondoa jeshi lake kwa muda kutoka sehemu ya magharibi ya ukingo wa magharibi wa Mto Jordan kabla ya uchaguzi kufanyika Januari mwakani, kuruhusu jeshi la Palestina kulinda usalama katika sehemu za Palestina; na katika siku za uchaguzi mkuu itaachia uhuru vituo wa vya polisi vilivyofungwa na Israel na kulegeza masharti kwa uhuru wa watu wa Palestina, kuruhusu wagombea kuwa na uhuru wa shughuli katika ardhi ya mamlaka ya Palestina na kuwaruhusu kufanya kampeni ya kiwango kidogo cha uchaguzi katika sehemu ya mashariki ya Jerusalem; kukubali Palestina na Israel kuweka vituo vitatu vya mawasiliano ili kutatua matatizo yanayoweza kutokea katika siku za uchaguzi mkuu; kukubali watu wa Palestina wa sehemu ya mashariki ya Jerusalem kupiga kura kwa posta kama uchaguzi mkuu ulivyofanywa mwaka 1996.
Kwa dhati ya moyo vyombo vya habari vinatumai kuwa pande mbili za Palestina na Israel zitatumia fursa hiyo ya uchaguzi mkuu wa Palestina kuanzisha tena mazungumzo na kuanza mchakato wa amani.
Idhaa ya kiswahili 2004-12-28
|