Katibu wa kidiplomasia wa Pakistan Bw. Riaz Khokhar na katibu wa kidiplomasia wa India Bw. Shyam Saran waliongoza ujumbe wao kushiriki katika mazungumzo hayo. Taarifa ya pamoja iliyotolewa na pande hizo mbili baada ya mazungumzo inasema kuwa, mazungumzo hayo yalifanyika katika "hali ya dhati ya moyo na kiujenzi". Pande hizo mbili pia zimeeleza nia yao ya kuendelea kusukuma mbele mchakato wa mazungumzo.
Taarifa inasema kuwa, pande hizo mbili zilijadili suala la amani na utulivu na kukubali kuzidi kuwasiliana, pia zilijadili kuchukua hatua zaidi ili kuimarisha uaminifu katika mipaka ya nchi hizo mbili na sehemu ya Kashmir. Pia pande hizo mbili zilijadili kuhusu mswada wa makubaliano wa "kuarifiana majaribio ya makombora", ingawa hazikusaini makubaliano, lakini mazungumzo hayo yamepunguza tofauti kati ya nchi hizo mbili kuhusu suala hilo.
Taarifa pia inasema kuwa, pande hizo mbili zimekubali kufanya mazungumzo ya kipindi cha tatu katika mwezi Aprili hadi mwezi Juni mwaka 2005, ambapo zitajadili kuhusu masuala ya mgogoro wa mipaka, kupambana na ugaidi, kupambana na biashara ya dawa za kulevya na ushirikiano wa uchumi na biashara. Aidha, maofisa na wataalamu wa nchi hizo mbili watashauriana kuhusu usalama wa mipaka na hatua za kujenga uaminifu katika nyanja za silaha za nyuklia na silaha za kawaida kuanzia mwezi Januari hadi Juni, mwaka 2005. Mwezi Julai au Agosti, mwaka 2005, makatibu wa kidiplomasia wa nchi hizo mbili watafanya mazungumzo tena huko New Delhi, mji mkuu wa India na kuangalia upya mazungumzo ya kipindi kipya.
Taarifa pia inatangaza kuwa, mawaziri wakuu na mawaziri wa mambo ya nje wa nchi hizo mbili huenda watafanya mazungumzo wakati mkutano wa 13 wa wakuu wa umoja wa ushirikiano wa kikanda wa Asia Kusini utakapofanyika huko Dacca, mji mkuu wa Bangladesh mwezi Januari, mwaka 2005. Aidha, waziri wa mambo ya nje wa India Bw. Natwar Singh atafanya ziara nchini Pakistan mwezi Februari, mwaka 2005 ili kujadili uhusiano kati ya India na Pakistan.
Habari zinasema kuwa, makatibu wa kidiplomasia wa nchi hizo mbili walifanya mazungumzo ya muda wa saa moja kuhusu suala la Kashmir, lakini hayakupata maendeleo makubwa kama ilivyokadiriwa mwanzoni. Bw. Saran alisema kuwa suala la Kashmir ni suala lenye utatanishi, nchi hizo mbili zinapaswa kupewa muda ili kulitatua. Pia alisema kuwa, Pakistan lazima ichukue hatua nyingi zaidi kuzuia watu wenye silaha kuingia katika sehemu ya Kashmir inayodhibitiwa na India. Lakini Bw. Khokhar alisema kuwa, Pakistan imefanya kwa uwezo wake kuwazuia. Alisema, katika suala la Kashmir, pande zote lazima zifanye mazungumzo ili kupunguza tofauti.
Katika mazungumzo hayo ya siku mbili, katibu wa kidiplomasia wa India Bw. Saran kwa nyakati tofauti alikutana na waziri wa mambo ya nje na waziri mkuu wa Pakistan. Waziri mkuu wa Pakistan Bw. Shaukat Aziz alipokutana na Bw. Saran alisema kuwa, anaridhika na mchakato wa mazungumzo ya hivi sasa na anatumai kuwa mazungumzo hayo yataweka mazingira mazuri kwa utatuzi wa masuala yaliyopo kati ya nchi hizo mbili. Bw. Aziz alisema kuwa, anatarajia kukutana na waziri mkuu wa India Bw. Manmohan Singh. Pia alitoa salamu za rambirambi kutokana na watu waliokufa na pole kwa waliojeruhiwa katika tetemeko la ardhi na mawimbi makubwa yaliyosababishwa na tetemeko hilo siku za karibuni.
India na Pakistan zilianzisha mchakato wa mazungumzo mwazoni mwa mwaka huu na zilifanya majadiliano kuhusu masuala ambayo bado hayajatatuliwa.
Wachambuzi wanaona kuwa, kutokana na hali ya utatanishi, haiwezekani kupata maendeleo kwa kufanya mazungumzo kadhaa. Nchi hizo mbili zilieleza kuwa kuendelea kufanya mazungumzo ndio maendeleo. Mazungumzo yatasaidia kuimarisha uaminifu kati ya pande hizo mbili na kutatua masuala mbalimbali kati yao.
Idhaa ya kiswahili 2004-12-29
|