Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-12-29 15:44:57    
Uchaguzi mkuu wa Iraq wakabiliana na mtihani mgumu

cri
    Kutokana na hesabu isiyokamilika, kutoka usiku wa tarehe 26 mpaka jana, mashambulizi yaliyotokea nchini Iraq, ambayo yalilenga jeshi la Marekani nchini Iraq, jeshi la wananchi la Iraq na maaskari wa Iraq yamesababisha vifo vya watu 74 na mamia ya watu kujeruhiwa. Jana watu wasiopungua 42 waliuawa, wengi kati yao walikuwa maaskari na wanajeshi wa jeshi la wananchi la Iraq. Katika mji ulio karibu na Tikrit, maskani ya rais wa zamani wa Iraq Bw. Saddam, wapinzani wa Marekani walikalia kituo cha polisi baada ya kuwaua askari 12, baadaye walilipua jengo la ofisi ya kituo cha polisi. Katika kituo cha polisi cha wilaya ya Ishaki kilichoko kusini mwa kituo cha upinzani wa Marekani Samarra, askari wanne na mwanajeshi mmoja wa Iraq waliuawa na wapinzani hao. Mjini Baghdad, kamanda wa jeshi la wananchi la Iraq anayeshughulikia usalama wa mji mkuu Bw. Modher Abud alipokwenda ofisini alishambuliwa kwa mlipuko wa kujiua. Ingawa alinusurika, lakini watu 6 waliokuwa wakiambatana naye na wapita njia walijeruhiwa.

    Juzi asubuhi, kiongozi wa kamati kuu ya mapinduzi ya Kiislam ya Iraq, ambayo ni chama kikubwa cha madhehebu ya Shia ya Iraq, Bw. Abdel Azizal-Hakim katika ofisi ya Baghdad alishambuliwa kwa mlipuko wa kujiua wa gari lenye mabomu, ingawa hakujeruhiwa, lakini watu 13 waliuawa na wengine 50 walijeruhiwa. Msemaji wa Bw. Azizal-Hakim alilaani nguvu za utawala wa zamani zilizobaki kuzusha mashambulizi hayo ili kuzuia mchakato wa kisiasa wa Iraq. Katika orodha ya wagombea 228 iliyotolewa na "umoja wa mshikamano wa Iraq", Bw. Azizal-Hakim ni mtu wa kwanza, ambaye ni mwenye matumaini makubwa kabisa kushinda kwenye uchaguzi na kuingia katika mamlaka ya Iraq na kuwa kiongozi wa kidini. Madhehebu ya Shia ya Iraq, ambayo yanachukua zaidi ya asilimia 60 ya idadi ya watu wa Iraq, inataka kupitia uchaguzi ili kuibadili hali nzuri ya idadi kuwa hali nzuri ya mamlaka, hivyo madhehebu ya Shia yanaunga mkono kufanya uchaguzi mkuu katika wakati uliowekwa. Pia kutokana na sababu hiyo, watu wanaopinga uchaguzi wanazusha mauaji ya siri kwa viongozi wa madhehebu ya Shia.

    Kinyume cha madhehebu ya Shia, baadhi ya vyama vya madhehebu ya Suni vinataka kuahirishwa kwa uchaguzi mkuu mpaka hali ya usalama ya Iraq itakapokuwa nzuri na jeshi la kigeni kuondoka kutoka Iraq. Vyama hivyo vinaona kuwa, uchaguzi mkuu unaofanyika katika hali ya jeshi la Marekani kuendelea kukalia hautakuwa wa haki. Waumini wa madhehebu ya Suni walishika madaraka mengi muhimu katika utawala wa zamani. Baada ya utawala ule kuangushwa, madhehebu ya Suni yanaipinga sana Marekani. Juzi chama cha Kiislam, ambacho ni chama kikubwa kabisa cha madhehebu ya Suni, kilitangaza kujitoa kutoka kwenye uchaguzi mkuu. Kabla ya hapo, chama hicho kiliikabidhi kamati ya uchaguzi wa Iraq orodha ya wagombea 275. Chama hicho kilisema kuwa, sababu ya kujitoa kwenye uchaguzi ni kwamba usalama hautahakikishwa na wapiga kura hawana haki ya kutosha ya kujua hali halisi.

    Vyombo vya habari vya Marekani juzi vilidokeza kumbukumbu ya ofisa mmoja wa Umoja wa Mataifa anayesaidia kazi ya uchaguzi mkuu wa Iraq, ambayo inaandika matatizo yanayoukabili uchaguzi huo.

    Wachambuzi wanaona kuwa, suala la usalama bado ni kikwazo kikubwa cha kufanyika kwa uchaguzi mkuu katika wakati uliowekwa. Jeshi la Marekani nchini Iraq baada ya kushambuliwa katika kituo cha Marekani cha Mosul na kusababisha vifo vya watu wengi, linajishughulisha na usalama wao, hivyo haliwezi kupeleka watu wengi kuhakikisha usalama wakati wa uchaguzi. Watu wengi wana wasiwasi kuwa, kama hali ya usalama haitaimarishwa wakati wa uchaguzi, basi hata kufanya uchaguzi kwa nguvu, watu wengi hawatathubutu kwenda kupiga kura, pamoja na ususia wa vyama vya Suni, bila shaka uchaguzi utaathiriwa. Hivyo, uchaguzi mkuu wa Iraq bado unakabiliana na mtihani mgumu.

Idhaa ya kiswahili 2004-12-29