Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-12-29 16:49:32    
Machafuko ya bahari yaliyosababishwa na tetemeko la ardhi baharini yaleta pigo kwa utalii na bima

cri

    Tetemeko kubwa la ardhi lililotokea karibu na kisiwa cha Sumatra, Indonesia, na mawimbi makubwa yaliyosababishwa na tetemeko hilo yalileta pigo kubwa kwa utalii wa nchi za Asia ya Kusini Mashariki na Asia ya Kusini, wakati huo huo sekta ya utalii na bima duniani pia imeathirika vibaya, hata hivyo wataalamu wanaona kuwa maafa hayo hayataathiri sana uchumi duniani.

    Tetemeko hilo baharini na mawimbi makubwa yaliyosababishwa na tetemeko hilo yalitokea wakati wa musimu wa utalii, siku za Krismasi na mwaka mpya, watalii wa nchi mbalimbali walipokuwa wakiburudika na ufukwe na kuota jua. Lakini baada ya kutokea maafa, mara watalii walikatiza utalii wao na kuondoka huko mapema iwezekanavyo.

    Sekta ya utalii ni kama nguzo ya uchumi nchini Thailand, kwa wastani kila mwaka nchi hiyo inapokea watalii milioni 12 kutoka nchi za nje. Mwaka 1997 msukosuko wa mambo ya fedha ulipotokea barani Asia, utalii nchini Thailand uliupiga jeki uchumi wa Thailand. Tetemeko hilo na maafa yaliyotokea ghafla yamegubika kivuli utalii wa Thailand na hasa sehemu ya kusini ya nchi hiyo. Vyombo vya habari vinatangaza kuwa mawimbi makubwa yaliyosababishwa na tetemeko la ardhi yameharibu mahoteli mengi na miundombinu ya utalii, yamesababisha zaidi ya vifo vya watalii 700 wa nchi za nje. Mkuu wa Idara ya Utalii ya Thailand kwa makadirio alisema kuwa pengine watalii kiasi cha milioni 1.2 wamefuta mpango wao kutalii nchini humo, na mapato ya utalii yatapungua kwa dola za Kimarekani milioni 750. Ukarabati hadi kufufua kabisa hali ya utalii kama awali pengine unachukua miaka miwili.

    Wataalamu wanasema kuwa katika muda fulani wa karibu, sekta ya utalii katika nchi zilizoathirika zitakabiliana na hofu ya watalii kutokana na maafa. Tetemeko hilo kubwa na mawimbi makubwa yaliyosababishwa na tetemeko hilo hayakuwahi kutokea katika miaka hata mia iliyopita, uharibifu wake utawakaa sana watu akilini na hofu yake haitafutika kupitia matangazo ya vyombo vya habari. Licha ya kazi ya ukarabati, kazi ya kuanzisha mfumo wa utabiri ni muhimu zaidi kwa kuondoa hofu ya watalii.

    Lakini wachambuzi wanaona kuwa maafa hayo hayataathiri sana uchumi wa nchi hizo zilizoathirika. Sababu muhimu ni kuwa vituo vya viwanda na bandari katika nchi hizo hazikuharibiwa, hasara iliyoletwa na maafa hayo ni sekta ya utalii tu. Kwa kusaidiwa na jumuia ya kimataifa, nchi hizo zina uwezo wa kupambana na maafa hayo, na si muda mrefu uchumi utafufuka.

    Licha ya sekta ya utalii wa kikanda, maafa hayo pia yataathiri utalii na bima duniani.

    Kitu kinachostahili kutajwa hapa ni bima duniani. Maafa yaliyosababishwa na tetemeko kali la ardhi baharini yamekuwa kama ni moto kwenye kidonda, kwani bima duniani limelipa dola za Kimarekani bilioni 42 kutokana na maafa mbalimbali ya kimaubile, kati ya maafa hayo, dola za Kimarekani 27 zilitolewa na bima kwa ajili ya maafa yaliyosababishwa na kimbunga nchini Marekani na Japan. Lakini magazeti barani Ulaya yanaona kuwa ingawa eneo linaloathiriwa na maafa hayo ni kubwa na limesababisha vifo vya watu wengi, lakini hayakuathiri sehemu muhimu ya kiuchumi duniani, kwa hiyo hayataathiri sana uchumi duniani.

Idhaa ya Kiswahili 2004-12-29