Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-12-30 15:52:06    
Mahmoud Abbas aanza kampeni ya kugombea nafasi ya mwenyekiti wa mamlaka ya Palestina

cri
Hivi karibuni, mwenyekiti mtendaji wa chama cha ukombozi wa Palestina ambaye pia ni mgombea pekee wa kundi kuu la PLO, Fatah Bw. Mahmoud Abbas, alikwenda kwenye miji mbalimbali iliyoko kwenye kando ya magharibi ya mto Jordan na kuanza kampeni ya kugombea nafasi ya mwenyekiti wa mamlaka ya utawala wa Palestina. Vyombo vya habari vinaona kuwa uchaguzi mkuu wa Palestina utakaofanyika tarehe 9 Januari mwaka kesho utakuwa uchaguzi wa Mahmoud Abbas peke yake. Wapalestina wanamtarajia Abbas kurithi juhudi za Arafat, kuwa mwenyekiti mpya wa mamlaka ya Palestina na kuwaongoza kutimiza amani katika mashariki ya kati.

    Tarehe 28, Abbas aliwasili kwenye kituo cha kwanza cha kampeni za ugombeaji wake, mjini Jericho na kufanya mkutano wa hadhara wa kwanza wa kampeni ulioanzishwa tarehe 25. Tarehe 29, Abbas alikutana na raia walioko katika miji wa Tulkarm na Qalqilyah na kuwahutubia. Miji hiyo miwili yote iko karibu na ukuta wa utenganishaji uliojengwa na Israel.

    Mahmoud Abbas kwanza alitoa hotuba kwenye uwanja wa michezo mjini Tulkarm. Baadaye alifika mjini Qalqilyah kukutana na waungaji mkono wake wenye uchangamfu wapatao mia kadhaa huku mgongo wake ukitazama ukuta wa utenganishaji. Bw Abbas alipotoa hotuba alieleza kuwa ukuta wa utenganishaji hautaleta amani kwa watu wa Israel, wala hautaleta usalama. Aliitaka Israel kuondoa ukuta huo ili kutimiza amani ya haki. Bw Abaas pia alifafanua msimamo wake wa ugombeaji kwa wapiga kura, yaani kujenga nchi huru ya Palestina ambayo mji mkuu wake ni Jerusalem kwa mazungumzo ya amani, kuwahakikisha wakimbizi Wapalestina kurejea kwenye maskani yao na kuwaachia huru Wapalestina wote waliofungwa na kutoa mwito wa kudumisha umoja ndani ya Palestina.

    Hotuba ya Abbas ilikatishwa mara kwa mara kwa vigelegele vya wasikilizaji wake. Lakini kampeni za wagombea wengine zilikuwa kimya. Kwa wapalestina wengi, Bw Abbas amekuwa kiongozi wao mpya.

    Kadiri uchaguzi mkuu unavyokaribia, ndivyo nchi kadhaa zimeimarisha uungaji mkono wa kisiasa na kiuchumi kwa Bw Abbas. Tarehe 28, serikali ya Marekani iliipatia mamlaka ya Palestina msaada wa uchumi wa dola za kimarekani milioni 20, ili kueleza imani yake kwa mageuzi ya kisiasa yanayofanywa na Bw Abbas. Israel hivi karibuni ilichukua hatua mfululizo za kuhakikisha uchaguzi mkuu wa Palestina unafanyika bila vikwazo, hatua ambazo zimesaidia kampeni ya Bw Abbas.

    Kwa upande mwingine, msimamo wa Bw Abbas kwenye hotuba ya ugombeaji pia umesababisha malalamiko kutoka kwa Israel. Waziri wa mambo ya nje wa Israel Bw. Silvan Shalom tarehe 27 aliushutumu msimamo huo wa Bw Abbas kwa kuharibu mazingira ya furaha ya kutimiza amani kati ya Israel na Palestina katika Mashariki ya Kati na duniani. Anaona kuwa Bw Abbas kutoa hotuba kama hiyo katika hali iliyopo sasa hakutawatia moyo, na Israel haiwezi kukaa kimya kutokana na msimamo wa Bw Abbas.

    Vyombo vya habari vinaona kuwa Bw Abbas anayetetea kutatua mgogoro kati ya Palestina na Israel kwa mazungumzo ya amani anaungwa mkono na watu wa Palestina na wa nchi nyingine, lakini pia anakabiliwa na shinikizo kubwa kutoka nchini Palestina na nchi za ng'ambo, hivyo Bw Abbas ameathirika wakati wa kutunga na kutekeleza programu yake ya kisiasa. Kutokana na hayo, kampeni za Bw Mahmoud Abbas hazitaendelea bila vikwazo.

Idhaa ya kiswahili 2004-12-30