Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-12-30 15:55:38    
Jumuiya ya kimataifa yaongeza misaada kwa nchi zilizokumbwa na maafa ya mawimbi makubwa yaliyosababishwa na tetemeko la ardhi

cri

    Tetemeko kubwa la ardhi na mawimbi makubwa yaliyoshababishwa na tetemeko hilo yaliyotokea tarehe 26 katika bahari ya Hindi zimeleta hasara kubwa kwa baadhi ya nchi za Asia ya Kusini na Kusini Mashariki, na jumuiya ya kimataifa inafualitia sana tukio hilo na imetoa misaada ya dharura kwa nchi hizo. Kutokana na harasa kubwa zilizoletwa na maafa hayo na kuongezeka kwa idadi ya watu waliokufa, jumuiya ya kimataifa inaongeza misaada.

    Tarehe 28, Idara husika za Umoja wa Mataifa zilifanya mkutano wa kuratibu misaada kwa nchi zilizokumbwa na maafa hayo huko Geneva. Wawakilishi wa nchi hizo walitoa ripoti kuhusu hasara ya maafa na kujadili kuhusu suala la misaada.

    Naibu mratibu wa misaada ya dharura wa Umoja wa Mataifa Bi. Yvette Stevens kwenye mkutano na waandishi wa habari alisema kuwa, katika siku mbili tatu zijazo, Umoja wa Mataifa utatoa mwito wa dharura kwa jumuiya ya kimataifa na kuchangisha nchi mbalimbali fedha za misaada zinazokaridiwa kufikia dola bilioni 1.6 za kimarekani, ili kutoa misaada kwa nchi hizo mapema. Hivi sasa, kutokana na takwimu za Umoja wa Mataifa, fedha za jumla za misaada zimezidi dola milioni 81 za kimarekani. Lakini kutokana na makadirio ya benki ya dunia, nchi hizo zinahitaji fedha za misaada karibu dola bilioni 5 za kimarekani.

    Katika siku za karibuni, nchi zilizoendelea zimeongeza misaada. Baada ya Marekani kutangaza mpango wa kutoa msaada wa dola milioni 15 za kimarekani, wizara ya mambo ya nje ya nchi hiyo tarehe 28 ilisema kuwa, Marekani itatoa msaada wa ziada wa dola milioni 200 za kimarekani kwa nchi zilizokumbwa na maafa.

    Serikali ya Australia jana ilitangaza kuzidisha msaada wa dola milioni 25 za kiaustralia, na mpaka sasa nchi hiyo kwa jumla imetoa msaada wa dola milioni 35 za kiaustralia.

    Chansela wa Ujerumani Gerhard Schroeder jana alitangaza huko Berlin kuwa, serikali ya nchi hiyo itaongeza msaada wa dharura kutoka Euro milioni 2 hadi kufikia Euro milioni 20.

    Serikali ya Japani iliahidi kutoa msaada wa dharura wa vitu vya mahitaji vyenye thamani ya dola milioni 30 za kimarekani, vikiwa ni pamoja na vyakula, dawa na mahema.

    Serikali ya Ufaransa na Uingereza jana zilitangaza kwa nyakati tofauti kutoa misaada ya Euro milioni 15 na Euro milioni 21.3.

    Aidha, Umoja wa Ulaya baada ya kutoa msaada wa dharura wa Euro milioni 3, tarehe 28 ulitangaza kuongeza msaada wake hadi kufikia Euro milioni 50.

    China ikiwa nchi inayoendelea, pia imeamua kutoa msaada kwa kulingana na uwezo wake, vitu vyenye thamani ya yuan milioni 21.6 vitasafirishwa kwa ndege kwa nchi zilizokumbwa na maafa. Jana, msaada wa China wa vitu vya mahitaji wa tani 100 ulifika huko Colombo, na msaada wa fedha dola laki 3 za kimarekani umekabidhiwa kwa serikali ya Thailand, na usiku wa siku hiyo, serikali ya China iliamua kuongeza msaada wa dharura kwa kisasi kikubwa.

    Qatar, Saudi Arabia na Kuwait pia zilitangaza kutoa msaada wa dola milioni 2 za kimarekani.

    Kuanzia terehe 27, baadhi ya misaada ya vitu vya mahitaji ilianza kufika kwenye sehemu zilizokumbwa na maafa. Mratiba wa kazi za utoaji misaada ya dharura wa Umoja wa Mataifa alisema kuwa, katika saa 48 zijazo, mamia ya ndege zinazobeba vitu vya misaada kutoka nchi 24 zitafika sehemu mbalimbali za maafa, na mpaka sasa nchi 16 zimepeleka vitu vya misaada nchini Sri Lanka iliyokumbwa na harasa kubwa. Jumuiya nyingi zikiwa ni pamoja na shirika la watoto wa Umoja wa Mataifa, jumuiya ya madaktari wasiyo na mipaka, shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia mambo ya wakimbizi, shirika la mpango na maendeleo la Umoja wa Mataifa, shirika la idadi ya watu wa Umoja la Mataifa na jumuiya ya kimataifa ya msalaba mwekundu zote zilipeleka watu wanaotoa misaada pamoja na vitu vya misaada. Jumuiya ya kimataifa, mashirika ya kimataifa na idara za kutoa misaada pamoja na nchi zilizokumbwa na maafa, zimeanza kuchukua hatua kubwa ya kutoa misaada duniani.

Idhaa ya Kiswahili 2004-12-30