Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-12-30 19:09:34    
Maisha ya mwanakampuni binafsi Bwana Li Xinghao na familia yake

cri

    Bwana Li Xinghao mwenye umri wa miaka 50 ni meneja mkuu wa kampuni ya viyoyozi ya Zhigao mjini Guangdong, ambayo ni kampuni binafsi kubwa kabisa inayozalisha viyoyozi nchini China. Mwaka 2004 ni mwaka mwenye mafanikio makubwa kwa bwana Li Xinghao: viyoyozi vyake vilivyouzwa viliongezeka kwa asilimia 50 kuliko mwaka jana; na amechaguliwa kuwa mmoja kati ya watu kumi hodari wenye moyo wa uvumbuzi na mageuzi nchini China; ameingizwa kwa mara ya tatu kwenye orodha ya matajiri wakubwa wa China bara na gazeti la Forbes, ambalo ni gazeti maarufu sana la kibiashara la Marekani.

    Bwana Li Xinghao anaishi katika kijiji cha Fenggang, mji wa Foshan, mkoani Guangdong. Kijiji hicho kiko karibu na mji wa Guangzhou, kusini mwa China. Japokuwa Fenggang ni kijiji, lakini hakionekani tena kuwa ni kijiji, kwa kuwa mashamba yote ya kijiji hicho yamechukuliwa na nyumba za wakazi, maduka na viwanda.

    Nyumba ya bwana Li Xinghao ni jengo lenye ghorofa tatu. Ghorofa ya chini ni karakana ya kutengeneza glavu za pamba. Bwana Li Xinghao na mkewe siku zote wanafanya kazi nje, ni mama yake tu mwenye umri wa miaka zaidi ya 80 ndio anabaki nyumbani pamoja na yaya. Japokuwa mama yake ni mwembamba na mfupi, lakini yeye bado ana afya nzuri, na ni hodari wa kushona nguo. Nguo anazozivaa huwa anazishona mwenyewe. Alisema:

    "Mtoto wangu ana kazi nyingi, yeye huondoka nyumbani saa kumi na mbili hivi asubuhi. Mchana hana wakati wa kukaa nyumbani, wakati fulani anarudi nyumbani mara mbili tatu tu kwa wiki."

    Bwana Li Xinghao alizaliwa katika familia ya mkulima, baba yake alifariki dunia mapema sana, hivyo aliishi maisha ya taabu alipokuwa mtoto. Hakuwa na budi ila kuacha masomo kabla ya kuhitimu kutoka shule ya sekondari ya juu.

    Ili kukidhi familia yake, Bwana Li Xinghao aliwahi kufanya biashara ndogondogo na kuendesha duka dogo. Kabla ya miaka 10 iliyopita, alifungua karakana ya kukarabati vifaa vya kupooza hewa. Baada ya miaka kumi, karakana hiyo ndogo imekuzwa kuwa kampuni kubwa ya kisasa inayozalisha viyoyozi, bidhaa za elektroniki, kemikali, miradi ya viumbe na kadhalika, mtandao wake wa mauzo umewekwa katika nchi na sehemu zaidi ya 200 duniani.

    Mkoa wa Guangdong ni sehemu yenye maendeleo makubwa ya uchumi binafsi nchini China. Bwana LI Xinghao alisema kuwa, kampuni yake isingeweza kupata maendeleo makubwa namna hiyo bila kupata uungaji mkono wa serikali ya mkoa. Alisema:

    "Katika miaka ya hivi karibuni, idara za serikali zimeinua tija ya kazi na mwamko wa kutoa huduma. Waliposikia mimi nilitaka kuuza hisa za kampuni yangu kwenye soko la hisa, watu wa serikali walikuja kuniuliza kama nahitaji msaada wowote."

    Hivi sasa kampuni ya Zhigao inafanya ushirikiano na kampuni nyingi za kimataifa duniani. Wakati kampuni yake inapostawi, Bwana Li Xinghao hakusahau kufanya shughuli za hisani kwa wanakijiji wake. Wafanyakazi wengi wa kampuni yake wanatoka kwenye kijiji chake, wazee wenye umri wa miaka 55 na zaidi wa kijiji chake kila mwezi wanaweza kupata posho ya maisha kutoka kwenye kampuni yake. Zaidi ya hayo, alikuwa ametumia fedha zake mwenyewe kujenga uwanja wa mpira wa kikapu, bwawa la kuogelea, kituo cha wazee na bustani.

    Mafanikio makubwa ya bwana Li Xinghao hayawezi kutengana na msaada wa mke wake Bibi Zhou Wanling. Wakati mume wake alipojitahidi kuboresha maisha ya familia yake, Bi. Zhou licha ya kufanya shughuli za nyumbani, pia alitafuta fursa ya kufanya biashara nje. Sasa japokuwa familia yake imetajirika, lakini kila siku Bi. Zhou anakwenda kazini kwenye kampuni yao kwa pikipiki kama wafanyakazi wengine.

    Bwana Li Xinghao ana mabinti wawili, wa kwanza anasoma nchini New Zealand, na mwingine anasoma katika shule ya sekondari mjini Guangdong. Mwezi Septemba mwaka huu binti wa kwanza Li Xiuhe alirudi nyumbani kutoka New Zealand kuwatazama wazazi, alishangaa kuona mabadiliko makubwa yaliyotokea katika mwaka huu. Alisema:

    "Kijiji kimependeza zaidi, baba yangu amehamia jengo jipya la ofisi, karakana mpya zinajengwa, mambo yote yanabadilika, karibu nilishindwa kutambua nyumbani kwetu."

    Mabinti wawili wa Bwana Li Xinghao wanaishi katika mazingira mazuri ya kifamilia, matumaini yake siyo kuwaelimisha kuwa warithi wa kampuni yake, bali ni kuwafanya wawe watu walioelimika kuwa na uwezo wa kuendeleza kampuni. Kama binti yake ana uwezo wa kutosha bila shaka atampa binti yake uongozi wa kampuni yake, ama sivyo atamkabidhi mtu hodari na anayewajibika kwa jamii.

Idhaa ya Kiswahili 2004-12-30