
Tetemeko kubwa la ardhi na mawinbi makubwa yaliyosababishwa na tetemeko hilo kwenye bahari karibu na kisiwa cha Sumatra, Indonesia yamekuwa maafa makubwa zaidi ya kimaumbile yaliyotokea katika miongo kadhaa iliyopita katika sehemu ya Bahari ya Hindi. Kikawaida maradhi hutokea baada ya maafa makubwa, hivyo hivi sasa kazi ya dharura ya jumuiya ya kimataifa ni kukinga maradhi, ama sivyo madhara ya maradhi huenda yatakuwa makubwa zaidi kuliko maafa ya kimaumbile.
Madhara ya maradhi huwa ni makubwa zaidi kwani watu hawawezi kuishi bila ya kunywa na kutumia maji, lakini maji huchafuliwa baada ya maafa ya mafuriko, watu wakinywa maji hayo huambukizwa na maradhi. Tena maradhi hayo hutokea baada ya muda fulani, lakini ni vigumu kuyadhibiti. Kufuatana na uzoefu wa kihistoria, maradhi makubwa husababisha msukosuko wa kijamii na hali isiyo tulivu.
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Kofi Annan alisema kuwa maafa hayo ni makubwa zaidi katika historia. Alisisitiza mara nyingi kuwa, lazima tuzingatie mara moja masuala ya ukosefu wa chakula, hali ya afya na usafi wa maji ili kuzuia maradhi yasitokee katika sehemu hizo. Mkurugenzi mtendaji anayeshughulikia maendeleo endelevu na usafi wa mazingira wa Shirika la Afya Duniani WHO Bw. David Nabaro ameonya kuwa, kutokana na ukosefu wa maji na hali mbaya ya kimaisha, maradhi kadhaa yakiwemo kuhara, malaria, homa ya dengue na maradhi ya mfumo wa hewa huenda yatatokea katika sehemu hizo hasa sehemu ambazo watu wengi wamejikusanya, na maradhi hayo yakitokea yatasababisha vifo vya watu wengi zaidi.
Hivi sasa tatizo la kukinga maradhi ni kubwa. Suala la kwanza ni fedha. Ingawa jumuiya ya kimataifa imetoa vitu na fedha nyingi kwa sehemu zilizokumbwa na maafa, lakini kutokana nchi kadhaa zilizoendelea kutojitahidi kushiriki katika kazi hiyo, ukosefu wa msaada bado ni mkubwa. Taarifa ya Shirika la Afya Duniani jana ilisema kuwa, hivi sasa bado zinatakiwa dola za kimarekani milioni 40 kuhakikisha vitu vya mahitaji kwa watu wa sehemu hizo. Suala la pili ni usafirishaji. Mawimbi makubwa yameharibu kabisa barabara za sehemu hizo, na kuzuia sana maendeleo ya kazi za uokoaji na uchukuzi wa vitu. Shirika la Afya Duniani lilisisitiza kuwa, lazima tuzingatie zaidi mkoa wa Aceh katika Kisiwa cha Sumatra uzingatiwe zaidi ambao ni karibu zaidi na kiini cha tetemeko la ardhi. Si kama tu watu wengi wamekufa na kujeruhiwa katika maafa, bali pia katika mkoa huo migogoro wa kijeshi imeendelea kwa miaka mingi na hali ya afya ni mbaya, hivyo hatari ya maradhi huko ni mkubwa zaidi. Hivi sasa mawasiliano ya barabara kutoka mikoa mingine hadi mkoa wa Aceh katika Kisiwa cha Sumatra yamepooza. Ingawa serikali ya Indonesia imeanzisha kituo cha uokoaji huko, lakini uchukuzi wa ndege unaotegemewa ni mdogo. Suala la tatu ni ushirikiano wa jumuiya ya kimataifa. Nchi nyingi duniani zinaunga mkono kufanya uokoaji zikiongozwa na Umoja wa Mataifa, lakini kuna nchi kadhaa ambazo zinataka kujipatia uongozi kwa maslahi yao yenyewe, na hii bila shaka italeta athari mbaya katika kazi ya uokoaji.
Hatuwezi kubashiri maafa ya kimaumbile, lakini tunaweza kubashiri maradhi makubwa baada ya maafa ya kimaumbile. Kutokana na uzoefu, maradhi hayo yanaweza kukingika. Hivyo nchi na mashirika husika yashirikiane kupunguza madhara ya maradhi kufuatana na uongozi wa Umoja wa Mataifa ni jambo muhimu ili kushinda maafa ya kimaumbile.
Idhaa ya Kiswahili 2004-12-31
|