Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2004-12-31 16:49:02    
Ukosefu wa mambo matano wajitokeza katika maafa ya mawimbi makubwa yaliyosababishwa na tetemeko la ardhi katika bahari ya Hindi

cri
    Kwanza, hakuna mfumo wa utabiri. Ingawa hivi sasa binadamu bado hawajaweza kudhibiti kabisa tetemeko na mawimbi makubwa ya bahari yanayosababishwa na tetemeko, lakini utabiri unaweza kupunguza ukali wa maafa. Si muda mrefu baada ya tetemeko la ardhi lenye ngazi ya 9.2 kutokea mwaka 1964 kwenye jimbo la Alaska, nchini Marekani, mara moja uchunguzi wa mawimbi kwenye ukingo wa bahari ya Pasifiki na mfumo wa utabiri wa mawimbi makubwa ya bahari ulianzishwa. Lakini mfumo wa utabiri kama huo haukuanzishwa hadi sasa katika bahari ya Hindi na kusababisha maafa hayo makubwa kutokea tena baada ya miaka 40.

    Pili, ukosefu wa uokoaji wenye uongozi mmoja. Maafa yanapotokea uongozi mmoja ni wa lazima ili kupambana na maafa kwa ushirikiano. lakini hali ilivyo katika uokoaji wa maafa hayo imedhihirisha kuwa hakuna uongozi wa namna moja, bali kila nchi inajishughulisha namna yake bila kuwa na ushirikiano na nchi nyingine. Ingawa nchi zilizoathirika zote ziko nyuma kiuchumi na haziwezi kuchukua hatua zenye mafanikio makubwa, lakini ushirikiano ukiwa mzuri, na kuwaondoa watu haraka na kusaidiana kimali na kupashana habari kwa wakati, maafa pia yangeweza kupungua.

    Tatu, tahadhari ya usalama ni hafifu na ukubwa wa maafa haukukadiriwa vya kutosha. Habari kutoka Thailand zinasema kuwa wataalamu wa utabari wa hali ya hewa walikuwa wamegundua dalili ya tetemeko la ardhi kabla ya wakati, lakini hawakutilia maanani kama maafa makubwa yangetokea, na hata walifikiri kuwa wakitangaza habari ya kutokea kwa mawimbi makubwa baharini kutokana na tetemeko la ardhi yangeathiri mapato ya utalii, kwa hiyo waliifadhi habari hiyo wakiwa na tumaini la bahati nasibu ya kutotokea kwa mawimbi hayo. Taarifa iliyotolewa na chombo cha habari nchini India imesema kuwa kabla ya kutokea kwa machafuko ya bahari, jeshi la India lilipata onyo la kutokea kwa machafuko hayo, lakini kutokana na urasimu mbaya ulioshamiri ulichelewesha nafasi nzuri ya kuchukua hatua za lazima kupambana na maafa kabla ya wakati.

    Nne, kupigania tu maslahi na kupuuza uharibifu wa mazingira. Safari hii athari ya mawimbi makubwa ya bahari imekuwa kubwa, na haikumwachia binadamu dakika za kutuliza akili. Baadhi ya wataalamu wanasema kuwa nchi nyingi kwenye ukingo wa bahari kuna kizuizi cha kimaumbile, yaani misitu ya mikoko, lakini kutokana na binadamu kuzingatia tu maslahi, wameharibu misitu hiyo. Katika miaka miongo kadhaa watu walikata misitu hiyo na kujenga mabwawa ya kufuga samaki na kamba, na miamba ya pwani pia imepungua sana. Pamoja na hayo, mahoteli mengi kwenye pwani kwa ajili ya watalii pia yameongeza hasara ya mali na vifo.

    Tano, kukwepa jukumu lipaswalo na kupuuza tatizo la pamoja la binadamu wote. Kutokea kwa maafa ya kimaumbile kunaweza kutokea wakati wowote na katika nchi yoyote, lakini kukinga na kupambana na maafa ni jukumu la binadamu wote. Na hasara ya maafa inaweza tu kupunguzwa kwa kadiri ya chini kabisa kwa ushirkiano wa nchi zote duniani. Lakini katika maafa hayo, mwanzoni baadhi ya nchi ambazo hazikuathirika moja kwa moja na maafa hayo zilichukua msimamo wa kutojali bila kuzingatia ipasavyo. Rais Bushi wa Marekani aliendelea kupitisha likizo yake baada ya kuarifiwa maafa hayo na alikosolewa vibaya na wananchi wake. Na baadhi ya miji mikuu ya nchi zilizoendelea haikushughulikia sana kuchangisha misaada, hali hiyo ilikosolewa na Umoja wa Mataifa.

    Lakini ni jambo la kufurahisha kwamba hivi sasa jumuiya ya kimataifa imetambua ukukbwa wa maafa hayo na imechukua hatua madhubuti kutoa msaada. Hatua hizo ni za lazima lakini hazitoshi, binadamu lazima watafakari namna ya kukwepa maafa kama hayo yasirudie rudie.

Idhaa ya kiswahili 2004-12-31