Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-01-04 15:57:51    
China yawasaidia watu wa Sri Lanka kwa nguvu zote katika ukarabati wa taifa

cri
    Sri Lanka imekumbwa na hasara kubwa ya watu na mali katika tetemeko la ardhi lililotokea katika bahari ya Hindi na mawimbi makubwa yaliyosababishwa na tetemeko hilo. Hivi sasa, serikali ya Sri Lanka imeunda kituo cha taifa cha shughuli za kupambana na maafa, ili kusimamia ukarabati baada ya maafa hayo. China ikiwa rafiki mkubwa wa Sri Lanka imewasaidia kwa nguvu zote watu wa Sri Lanka katika ukarabati huo.

    Baada ya kutokea kwa maafa hayo, balozi wa China nchini Sri Lanka Bw. Sun Guoxiang siku zote ameshughulikia kuwasaidia watu wa Sri Lanka katika ukarabati wa taifa. Tarehe 3 alihojiwa na mwandishi wa habari, akisema:

    "Baada ya kutokea kwa maafa hayo, kwanza viongozi wa China rais Hu Jintao na waziri mkuu Wen Jiabao waliwatumia salamu rais na waziri mkuu wa Sri Lanka na rais wa Maldives. Baadaye, serikali ya China iliamua kuzipelekea nchi hizo shehena ya kwanza ya vitu vya kupambana na maafa, yaani kuipatia Sri Lanka vitu vyenye thamani ya Yuan za Renminbi milioni 10 na fedha taslimu ya dola za kimarekani laki 2 na kuipatia Maldives fedha taslimu dola za kimarekani laki 3. Tarehe 29 alasiri, ndege maalum ya China iliyobeba vitu hivyo iliwasili nchini Sri Lanka, usiku wa siku hiyo baadhi ya vitu hivyo vilipelekwa katika sehemu zilizokumbwa na maafa ".

    Balozi Sun Guoxiang alieleza kuwa kadiri maafa yanavyoendelea, ndivyo serikali ya China imavyoongeza sana misaada yake kwa Sri Lanka. Tarehe 2 serikali ya China ilithibitisha idadi ya pili ya misaada yenye thamani ya Yuan za Renminbi milioni 15 iliyokuwa ikipelekwa nchini Sri Lanka na kikosi cha utoaji misaada ya matibabu cha China tarehe 3 alfajiri kiliwasili mjini Galle, mji uliokumbwa na maafa makubwa kabisa nchini humo. Ofisa wa ubalozi wa China nchini Sri Lanka Bw. Cao Ansheng aliyefuatana na kikosi hicho cha China mjini Galle ana imani kuwa kikosi hicho kitafanya kazi kwa ufanisi wake akisema:

    "Sasa kikosi cha matibabu kinafanya matayarisho ya kazi, baadaye kitawasiliana na maofisa wa matibabu wa sehemu ya huko, ili wawaongoze madaktari wa China kwenda sehemu zilizokumbwa na maafa".

    Kwa kweli, kabla ya kikosi cha utibabu kufika katika sehemu zilizokumbwa na maafa, ubalozi wa China nchini Sri Lanka ulikuwa umefanya kazi nyingi za kupambana na maafa hayo. Balozi Sun Guoxiang alikwenda mwenyewe kwenye sehemu nne zilizokumbwa na maafa na kuona kuwa maafa hayo ni makubwa sana. Sasa serikali ya Sri Lanka inakabiliwa na changamoto mbili, ya kwanza ni kufikisha vitu vya misaada katika sehemu hizo, ya pili ni kusafisha sehemu hizo, ili kuzuia maambukizi ya magonjwa. Balozi Sun akizungumzia uhusiano kati ya China na Sri Lanka na kazi ya utoaji misaada ya China, anasema kwa msisimko:

    "Naona watu wa Sri Lanka wana matarajio makubwa kutoka kwa China. Watu wa China na wa Sri Lanka wana urafiki asili. Sasa rafiki amepatwa na shida, China hakika itamsaidia rafiki yake kwa nguvu zote na kuwasaidia watu wa Sri Lanka wawe na imani ya kujiokoa katika maafa hayo.

Idhaa ya kiswahili 2005-01-04