Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-01-04 21:20:35    
Kabila la wasala

cri

   

    Katika sehemu ya Dunhua, mkoani Qinghai, kaskazini magharibi ya China, wanaishi kabila la wasala ambao zaidi ya miaka 700 iliyopita mababu wa wasala wa Dunhua walikuwa wakiishi katika Asia ya kati.

    Wasala wanaishi katika wilaya ijiendeshayo yenyewe ya Dunhua, mkoani Qinghai, kaskazini magharibi mwa China. Huko kuna ziwa moja lenye maji nadhifu liitwalo "chemchemi ya ngamia" na ndani ya ziwa hilo kuna mwamba mmoja mweupe uitwao "mwamba wa ngamia". Chemchemi ya ngamia ni kama alama ya kabila la wasala. Inasemekana kuwa hapo kale, katika sehemu ya Samarkhan ya Asia ya kati (yaani katika Jamhuri ya Uzbekstan ya hivi leo), kulikuwa na ndugu wawili Galeman na Arhaman, ambao waliheshimiwa sana na waumini wa kiislamu wa huko. Mfalme aliwaonea wivu ndugu hao wawili akafanya hila ya kuwadhulumu. Galeman na Arhaman waliamua kuhama na kutafuta ardhi mpya ya kuishi. Wakiongoza jamaa zao 18 walianza safari yao ya kuelekea mashariki wakifuatana na ngamia mmoja mweupe ambaye alibeba mgongoni mwake udongo na maji ya nyumbani pamoja na kurani.

    Baada ya safari ndefu, Galeman na Arhaman pamoja na jamaa zao walifika katika milima ya Manda wilayani Dunhua. Usiku kwa bahati mbaya ngamia mweupe alipotea njia akatoweka. Iliwabidi wamtafutetafute. Kulipokucha walifika kwenye ziwa lenye maji safi wakaona ngamia wao mweupe anasimama ziwani lakini ameshageuka kuwa mwamba. Baada ya kuchunguza udongo na maji ya huko, waligundua kwa furaha kwamba udongo na maji yote yanafanana na yale ya nyumbani kwao, hivyo wakaamua kupiga maskani kando ya ziwa hilo. Na hiyo ndiyo hadithi inayosimulia jinsi wasala walivyotoka mbali na walivyoamua kuishi kwenye ziwa la ngamia.

    Wataalamu wa fani ya makabila wanasema kuwa lugha ya wasala inatofautiana kabisa na lugha ya kichina katika misamiati au sarufi; kidogo inafanana na lugha wanayoitumia watukmenistan na wauzbekstan wa leo. Kutokana na nyimbo za kabila hilo, tunaweza kujua kuwa mavazi ya wasala pia yanafanana na yale ya watu wa Asia ya kati. Hivi sasa wanaume wa kabila la wasala wanavaa kofia nyeupe au nyeusi, na wanawake hujifunika buibui. Kwa kuwa wasala ni wafuasi wa dini ya kiislamu, wanawake wote wanavaa buibui. Wasichana aghalabu huvaa buibui za rangi ya kijani. Baada ya kufunga ndoa na kuzaa watoto, huvaa buibui nyeusi. Akina mama wenye umri zaidi ya miaka 60, huanza kutumia buibui nyeupe.

   Hadi leo wavulana na wasichana wa kabila la wasala hawachumbiani na ndoa yao inaamuliwa na wazazi. Wazazi wa mvulana fulani wakitaka kumtafutia mtoto wao mchumba inawabidi waombe mposaji apeleke posa kwa wazazi wa msichana. Posa hiyo ikikubaliwa, wazazi wa mvulana huwapelekea chai na zawadi nyingine wazazi wa msichana. Zawadi hizo zikipokelewa, wazazi wa pande mbili huchagua siku ya harusi.

   Wasala ni watu wenye bidii na busara; wanapenda kazi. Wasala wengi wana kipaji cha kufanya biashara. Hivi sasa China inafuata sera za mageuzi ya kiuchumi na mlango wazi kwa nje. Busara za wasala za kufanya biashara zimejulikana zaidi na zaidi. Wasala wengi sana wanashughulikia biashara ya ngozi. Hivi sasa wilaya wanakokaa wasala ni soko kubwa la biashara ya ngozi.

   

Idhaa ya Kiswahili 2005-01-04