Mkutano wa viongozi wa nchi za Asia ya Kusini Mashariki kuhusu maafa ya mawimbi makuwa yaliyosababishwa na tetemeko la ardhi baharini utafanyika kesho Djakarta, mji mkuu wa Indonesia. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Kofi Annan na viongozi au wajumbe wa nchi zaidi ya 20 watahudhuria mkutano huo na kujadiliana namna ya kuzisaidia nchi zilizokumbwa na maafa hayo. Wachambuzi wanaona kuwa kufanyika kwa mkutano huo wa viongozi wakubwa wa nchi nyingi mara tu baada ya kutokea kwa maafa makubwa kumeonesha mshikamano mkubwa na nia thabiti ya kimataifa katika mapambano dhidi ya maafa.
Tetemeko la ardhi na mawimbi makubwa yaliyosababishwa na tetemeko hilo baharini yameletea maafa makubwa ya hali na mali na yamebebesha mizigo mizito kwa nchi za Asia ya Kusini Mashariki, nchi zilizoathirika zinahitaji misaada ya haraka ya kimataifa na kuungwa mkono katika ukarabati wa kitaifa. Katika kukabiliana na hali mbaya ya dharura, waziri mkuu wa Singapore Lee Hsien Loong alitoa wito wa kuitisha mkutano mkubwa wa nchi za Asia ya Kusini Mashariki ili kujadili mambo ya ukarabati wa nchi hizo. Wito wake mara ulikubaliwa, viongozi au wajumbe wakiwemo waziri mkuu wa China Bw. Wen Jiabao, waziri mkuu wa Japan Junichiro Koizumi, rais wa Indonesia Susilo Bambang Yudhoyono, waziri mkuu wa Malaysia Abdullah Ahmad Badawi, waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Colin Powell, nchi zaidi ya 20 zilizoathirika, nchi wahisani na mashirika ya kimataifa watahudhuria mkuktano huo.
Imefahamika kuwa viongozi au wajumbe wa mkutano huo watajadiliana masuala kuhusu misaada, ukarabati na uimarishaji wa kukinga maafa. Na kutokana na mafunzo yaliyopatikana kutoka tetememko la ardhi na mawimbi yaliyosababishwa na tetemeko hilo, watajadili namna ya kuanzisha mapema iwezekanavyo mfumo wa utabiri wa mawimbi makubwa ya tetemeko la ardhi baharini.
Indonesia ni nchi iliyoathirika vibaya zaidi, hivi sasa watu zaidi ya elfu 90 wamepoteza maisha yao. Rais wa Indonesia amesema kuwa nchi yake imekuwa na mpango wa kuanzisha mfumo wa utabiri wa mawimbi makubwa ya bahari ili kuzuia maafa makubwa zaidi kutokea. Viongozi wa nchi nyingine za Asia ya Kusini Mashariki pia walitoa ombi hilo. Ingawa Philipines sio nchi iliyoathirika moja kwa moja na maafa hayo, lakini rais sa nchi hiyo Gloria Macapagal Arroyo pia alisema kuwa mkutano huo haifai kujadili tu misaada bali vilevile ujadili kuimarisha ushirikiano wa kufaidika na habari kwa pamoja na kuanzisha mfumo wa utabiri wa kikanda. Isitoshe nchi za Thailand na Singapore pia zilisisitiza uzito wa ushirikiano huo na mfumo huo. Waziri wa mambo ya nje wa Thailand Surakiart Sathirathai alipendekeza kuwa sehemu fulani ya misaada ya fedha itumike kwa ajili ya kuanzisha mfumo huo.
Jambo linalostahili kutajwa hapa ni kuwa Umoja wa Mataifa ulifanya juhudi nyingi za matayarisho ili kufanikisha mkutano huo kufanyika. Imefahamika kuwa Umoja wa Mataifa umegawanya juhudi za mapambano dhidi ya maafa katika vipindi viwili, kipindi cha kwanza ni kuokoa na kutibu walioathirika. Kipindi cha pili ni kusaidia ukarabati wa nchi zilizoathirika. Kufanyika kwa mkutano huo kunamaanisha kipindi cha pili kuanza. Kabla ya hapo Umoja wa Mataifa umekusanya fedha nyingi, na kwenye mkuktano huo katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Kofi Annan atatoa wito kwa nchi hisani na mashirika ya kimataifa kuharakisha kutimiza ahadi zao za kutoa misaada bila kuchelewa kwa nchi zilizoathirika.
Idhaa ya kiswahili 2004-01-05
|