Kikundi cha matibabu cha China kimeanza kazi yake katika mji wa Galle, kusini mwa Sri Lanka, ulioathiriwa zaidi na maafa. Utaalam na upendo wao unapongezwa sana na watu wa sehemu iliyokumbwa na maafa.
Bw. Sugath Chandana, mama yake, mke wake na jamaa zake wengine wengi walipotea kutokana na mawimbi makubwa yaliyosababishwa na tetemeko la ardhi, lakini yeye alinusurika, alipokaribisha kikundi hicho, alisema:"Kila siku kuna vikundi vya matibabu vya nchi nyingine vinavyofika hapa, lakini walikaa kwa saa moja mbili tu, ila kikundi cha matibabu cha China kinakaa hapa usiku na mchana. Wenyeji wenzetu wanaridhika sana na kikundi hicho."
Kikundi hicho chenye watu 14 kilifika huko Colombo, mji mkuu wa Sri Lanka tarehe 2 subuhi, mara baada ya kushuka kutoka kwenye ndege, kilikwenda moja kwa moja huko Galle, mji ambao umeathirika zaidi na maafa. Tarehe 3 waliweka mahema na kuanza kuwatibu wagonjwa mchana na kulala kwenye mahema usiku.
Mjumbe wa kikundi hicho Bw. Xia Jiyong alimwambia mwaandishi wa habari kuwa waliamka alfajiri tarehe 4 na kufanya matayarisho ili waweze kuanza kazi yao. Alisema:"Tulifanya matayarisho kuanzia saa kumi na mbili alfajiri, tuliandaa vifaa na dawa mbalimbali, na kuanza kuwatibu wagonjwa saa mbili, hadi kufikia sasa, tumewatibu wagonjwa kwa muda wa saa tatu. Kwa kuwa leo ni siku ya kwanza, wagonjwa walikuwa wengi sana."
Kikundi hicho kinashughulikia sehemu ya Hikkaduwa, kitongoji cha Galle, kabla ya maafa kulikuwa na wakazi zaidi ya elfu 10, lakini hivi sasa, idadi ya wakazi imepungua na kufikia elfu 7. Hivi sasa kikundi hicho kinawashughulikia watu hao waliosalimika. Kutokana na hali duni ya sehemu hiyo, wajumbe wa kikundi hicho usiku wanalala kwenye mahema, na mchana wanakula biskuti na tambi za mara moja, kibaya zaidi ni kuwa hakuna maji ya moto, wanapaswa kula tambi hizo kikavu. Miongoni mwa wajumbe wa kikundi hicho, kuna wanawake kadhaa, kwa uhakika wanakabiliana na matatizo mengi zaidi. Lakini kila mmoja wa kikundi hicho alieleza kuwa watajitahidi kupambana na matatizo, na hawalali mpaka baada ya kumtibu mgonjwa wa mwisho wa kila siku.
Mkuu wa kikundi hicho daktari Wang Bingqiang, ambaye anatoka Hospitali ya Urafiki ya Beijing, alimwambia mwandishi wa habari kuwa anahisi sana urafiki wa watu wa huko kwa serikali na wananchi wa China. Alisema:"Tunaweza kuhisi urafiki kati ya serikali ya China na ya Sri Lanka na kati ya wananchi wa China na wa Sri Lanka. Wasri Lanka wanaunga mkono kazi yetu na kutusaidia kadiri wanavyoweza. Tunatiwa moyo sana."
Bw. Wang alisema kuwa wakiwa kikundi cha kwanza cha matibabu kutoka China, waliona kuwa hali ya hapo ni mbaya, watu wengi walikufa, kujeruhiwa au hawajulikani walipo, pia walipata hasara kubwa ya mali. Ingawa kuna matatizo mengi, lakini wanahudumu wa afya wa China watatekeleza vizuri wajibu wa kibinadamu na kufanya vizuri kazi ya daktari.
Idhaa ya Kiswahili 2005-01-05
|