Mkutano maalum wa wakuu wa umoja wa Asia ya kusini na kusini mashariki utafanyika kesho tarehe 6 huko Djakarta, mji mkuu wa Indonesia. Hii ni mara ya kwanza kwa jumuiya ya kimataifa kufanya mkutano wa ngazi ya juu wa kimataifa kuhusu jinsi ya kupambana na maafa na kufanya ukarabati baada ya kutokea kwa maafa ya tetemeko la ardhi na machafuko ya bahari yaliyosababishwa na tetemeko hilo. Wakuu kutoka nchi zaidi ya 20 na wajumbe wa mashirika ya kimataifa watahudhuria mkutano huo, waziri mkuu wa China Bwana Wen Jiabao ataongoza ujumbe wa serikali ya China kushiriki kwenye mkutano huo. Mkutano huo umeonesha vya kutosha ufuatiliaji na ushirikiano mzuri wa jumuiya ya kimataifa kwa kazi ya kupambana na maafa na utoaji misaada.
Tetemeko la ardhi na machafuko ya bahari yaliyotokea kwenye bahari ya Hindi ni maafa ya pamoja kwa binadamu, maafa hayo pia yamewaunganisha pamoja binadamu. Katika kukabiliana na maafa hayo, jumuiya ya kimataifa imeonesha mshikamano usiowahi kutokea hapo kabla. Hadi leo, nchi mbalimbali duniani zimeshatoa misaada yenye thamani ya dola za kimarekani bilioni mbili kwa nchi zilizokumbwa na maafa. Nchi nyingi pia zimepeleka vikosi vya uokoaji kwa sehemu zilizokumbwa na maafa.
Umoja wa Mataifa umefanya kazi kubwa katika shughuli za kupambana na maafa. Baada ya kutokea kwa tetemeko la ardhi na machafuko ya bahari yaliyosababishwa na tetemeko hilo, Umoja wa Mataifa na mashirika yake yalituma haraka vikundi vya kutathmini hasara za maafa na kuratibu kazi ya uokoaji. Umoja wa Mataifa pia umeanzisha vituo maalum vya kuratibu kazi za uokoaji na usimamizi wa angani, na kuchangisha dola za kimarekani bilioni 1.5 kwa nchi zilizokumbwa na maafa. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Kofi Annan tarehe 3 usiku alifunga safari kwenda Djakarta, kujadiliana na viongozi wa nchi za Asia kusini kuhusu maafa hayo, pia atahudhuria mkutano wa wakuu wa tarehe 6.
Bwana Annan amesema kuwa, lengo kuu la mkutano wa wakuu wa Djakarta ni kuonesha nia ya binadamu katika kupambana na maafa, kuzisaidia nchi zilizokumbwa na maafa kurudisha maisha ya kawaida, kuitaka jumuiya ya kimataifa kutimiza ahadi ya misaada haraka iwezekanavyo. Habari zinasema kuwa, Umoja wa Mataifa umepanga kuigawa kazi ya uokoaji katika vipindi viwili, kipindi cha kwanza ni kutoa misaada ya dharura, kuwaokoa na kuwatibu watu waliojeruhiwa; kipindi cha pili ni kuzisaidia sehemu zilizokumbwa na maafa kufufua uzalishaji mali na kufanya ukarabati. Kufanyika kwa mkutano wa wakuu wa Djakarta kunaashiria kuanza kwa kazi ya kipindi cha pili.
Ikiwa nchi jirani ya nchi za Asia ya kusini na kusini mashariki, na nchi kubwa inayowajibika, China imetoa mchango mkubwa katika shughuli za kupambana na maafa. Kwenye mkutano wa wakuu wa Djakarta, waziri mkuu wa China Wen Jiabao ataeleza nia thabiti ya serikali na wananchi wa China kwa nchi na watu waliokumbwa na maafa na kueleza msimamo wa serikali ya China katika kupambana na maafa. China ni moja ya nchi za kwanza zilizopeleka vifaa vya misaada na vikosi vya madaktari kwa nchi zilizokumbwa na maafa, baada ya kupeleka shehena ya kwanza ya misaada, serikali ya China pia iliongeza vifaa vya misaada yenye thamani ya yuan milioni 500. Hii ni misaada mikubwa kabisa katika historia ya utoaji misaada ya China. Katika siku za hivi karibuni, fani mbalimbali nchini China zimeanzisha shughuli za kuchangia fedha na kusaidia kupambana na maafa, jambo hilo limeonesha vya kutosha ufuatiliaji na uungaji mkono wa watu wa China kwa watu waliokumbwa na maafa.
Maafa hutokea bila kutegemea, lakini ufuatiliaji na upendo wa binadamu ni wa dhati. Tuna imani kuwa, kwa juhudi za pamoja na ushirikiano mzuri wa jumuiya ya kimataifa, binadamu itapita maafa yoyote.
Idhaa ya kiswahili 2005-01-05
|