Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-01-05 20:44:42    
Uchaguzi mkuu wa Iraq wakabiliwa na matatizo mengi

cri

    Kutokana na kukaribia kwa siku ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa Iraq tarehe 30 Januari, hali ya usalama nchini Iraq inaongezeka kuwa ya wasiwasi siku hadi siku. Kuuawa kwa mkuu wa mkoa wa Baghdad Bwana Ali al-Haidri kumeleta utatanishi zaidi kwa mustakabali wa uchaguzi mkuu wa nchi hiyo.

    Kufanyika kwa uchaguzi mkuu ni jambo kubwa katika mchakato wa kufanya ukarabati wa kisiasa wa Iraq, lakini bado kuna mashaka mengi kama uchaguzi mkuu wa nchi hiyo unaweza kufanyika kwa wakati au la.

    Kwanza, hali ya usalama nchini Iraq haiwezi kuboreshwa kimsingi. Hivi karibuni shughuli za kimabavu zimekuwa zikitokea hapa na pale nchini Iraq. Idara ya upelelezi ya Iraq imedokeza kuwa, hivi sasa nchini Iraq kuna watu laki mbili wanaoipinga Marekani, idadi hiyo inazidi ile ya askari wa Marekani nchini Iraq, na kati yao kuna wanamgambo elfu 40. Wanamgambo hao wanaweza kuwalenga na kuwaua maofisa wa Iraq kwa ufanisi, na kikosi cha usalama cha Iraq hakiwezi kuwalinda maofisa hao kwa ufanisi. Mbali na hayo baadhi ya wanamgambo wanaoipinga Marekani walitoa taarifa ikiwataka watu wa Iraq wasishiriki kwenye uchaguzi mkuu, na hata kutishia kufanya mashambulizi dhidi ya wapiga kura, vituo vya upigaji kura na wafanyakazi wa vituo hivyo. Hata waziri wa mambo ya nje wa Marekani Bwana Colin Powell amekiri kuwa, kutokana na kukaribia kwa siku ya kufanyia uchaguzi mkuu, matukio mengi zaidi ya mashambulizi yatatokea nchini Iraq. Katika hali kama hiyo, wapiga kura watathubutu kupiga kura zao? Na matokeo yenye kiasi kidogo cha wapiga kura yataaminika au la?

    Pili, matayarisho ya uchaguzi mkuu bado hayajakamilika. Vyombo vya habari vinaona kuwa, tofauti na uchaguzi mkuu wa nchi nyingine, shughuli za kampeni nchini Iraq zinaendelea kwa kimya. Hakuna mabango, hakuna mijadala kwenye televisheni, na hakuna mihadhara, raia wengi wamelalamika kuwa, hawana njia yoyote ya kufahamu hali ya wagombea, hivyo ni vigumu kwao kufanya uchaguzi sahihi. Aidha, kutokana na ukosefu wa dhamana ya usalama, hadi sasa vituo vya upigaji kura bado havijathibitishwa, hata wafanyakazi wa muda laki mbili na elfu 50 kwa ajili ya uchaguzi huo waliandikishwa kimyakimya.

    Tatu, uchaguzi huo utakuwa na uwakilishi au la. Chama cha Kiislam cha Iraq ambacho ni chama kikubwa cha madhehebu ya Sunni ya Iraq, tarehe 27 Desemba kilitangaza kujitoa kwenye uchaguzi mkuu, jambo hilo ni pigo kubwa kwa uchaguzi mkuu wa Iraq. Kama chama hicho hakitashiriki kwenye uchaguzi mkuu, basi madhehebu ya sunni yanayochukua hadhi muhimu katika jukwaa la kisiasa la Iraq hayatakuwa na wawakilishi wao kwenye bunge. Zaidi ya hayo, ikiwa matokeo ya uchaguzi mkuu hayawezi kukidhi matakwa ya vyama vyote vya kisiasa vya Iraq, huenda utazusha msukosuko mpya. Gazeti la New York Times la Marekani jana lilitoa habari ikisema kuwa, waziri mkuu wa serikali ya muda ya Iraq Bwana Ayad Allawi tarehe 3 alimpigia simu rais Bush wa Marekani, walibadilishana maoni kuhusu matatizo yaliyokuwepo kabla ya kufanya uchaguzi mkuu mwishoni mwa mwezi huu. Kabla ya hapo, waziri wa ulinzi wa Iraq Bwana Hazem Shaalan tarehe 3 alisema kuwa, kama vyama vya kisiasa vya madhehebu ya Sunni vitakubali kushiriki kwenye uchaguzi mkuu, serikali ya muda inaweza kuahirisha upigaji kura, lakini waziri wa mambo ya nje wa Iraq na msemaji wa serikali ya Marekani wote walisisitiza kuwa, hivi sasa bado hakuna mpango wa kuahirisha siku ya upigaji kura.

    Wachambuzi wanaona kuwa, japokuwa serikali ya muda ya Iraq na serikali ya Marekani zote zinatumai kuwa uchaguzi mkuu wa Iraq utafanyika kwa wakati na kwa mafanikio, lakini uchaguzi mkuu si dawa kabisa ya kutatua masuala yote yaliyoikabili Iraq. Serikali ya Bush ikishikilia kufanya uchaguzi mkuu bila kujali hali halisi ya nchini Iraq kutokana mpango uliowekwa, basi Marekani huenda itajiingiza katika hali mbaya zaidi nchini Iraq.

Idhaa ya Kiswahili 2005-01-05