|
Katibu mkuu wa Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki Bw. Mohammed el Baradei tarehe 5 huko Vienna alisema kuwa kutokana na kukubaliwa na Iran, wataalamu wa shirika lake watafanya ukaguzi wa zana za kijeshi katika sehemu ya Parchin nchini Iran ndani ya muda wa siku au wiki kadhaa zijazo. Vyombo vya habari vinaona kuwa hii ni hatua mpya katika utatuzi wa suala la nyuklia, kwa kuwa mwaka jana wakaguzi wa shirika hilo hawakuruhusiwa kuingia kwenye sehemu hiyo.
Sehemu ya Parchin iko umbali wa kilomita 30 kusini ya Tehran, mji mkuu wa Iran, imefahamika kuwa huko ni kituo cha kuendeleza makombora ya nyuklia nchini Iran, lakini Iran toka mwanzo ilikana kwamba zana za huko zina uhusiano wowote na mpango wa kuendeleza silaha za nyuklia. Mwezi Novemba mwaka jana ripoti ya Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki kuhusu tathmini ya tatizo la nyuklia nchini Iran ilitaja kwa makusudi kwamba wakaguzi wake hawakuruhusiwa kuingia kwenye sehemu hiyo. Wachambuzi wanaona kuwa sababu ya ripoti kutotoa uamuzi wowote kuhusu shughuli za kuendeleza silaha za nyuklia nchini Iran inatokana na kutoweza kuingia katika sehemu hiyo yenye "kitandawili".
Lakini basi, ni kwa nini sasa Iran imebadilisha msimamo wake na kuruhusu wakaguzi kuingia katika sehemu ya Parchin?
Kama inavyojulikana kuwa, Shirikka la Kimataifa la Nishati la Atomiki limewahi kupitisha maazimio mengi tokea mwezi Juni mwaka juzi na hasa azimio lililopitishwa tarehe 18 Septemba mwaka jana, ambalo lilitaka Iran isimamishe shughuli zote za kusafisha uranium kabla ya tarehe 25 Novemba. Ili kuishawishi Iran ikubali azimio hilo, nchi tatu za Ufaransa, Ujerumani na Uingereza zilitoa "mpango wa jumla" wa kuisaidia Iran nishati ya nyuklia, kujenga kinu cha nyuklia na kuanzisha ushirikiano wa sekta mbalimbali na kuiunga mkono Iran ijiunge na WTO. Tarehe 14 Desemba mwaka jana Iran na nchi hizo tatu zilifikia mkataba, na Shirika la Kimataifa la Nishati la Atomiki lilipitisha uamuzi kuwa halitawasilisha suala la nyuklia la Iran kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Huu ni ushindi wa kipindi fulani kwa Iran kutokana na kukwepa hali ambayo Marekani ilitumai kuwa suala la nyuklia la Iran litawasilishwa kwenye Baraza la Usalama na kuiadhibu.
Kuanzia katikati ya mwezi wa Desemba mwaka jana Iran na nchi tatu za Ufaransa, Ujerumani na Uingereza zilianza kujadili "mpango wa jumla". Imejulikana kuwa mazungumzo yalipata maendeleo fulani, Iran ilisema uhusiano kati ya Iran na Umoja wa Ulaya umefungua "ukurasa mpya", na upande wa nchi tatu unasema tatizo la nyuklia la Iran limeingia katika "kipindi kipya", na kutangaza kuwa mazungumzo ya kiteknolojia yanaweza kuanzishwa mara moja. Hayo ndio mazingira ambayo yameifanya Iran ikubali wakaguzi wa shirika la kimataifa la nyuklia waingie katika sehemu ya Parchin. Magazeti ya Ulaya yanaona kuwa hii ni juhudi ya Iran kwa ajili ya kusukuma mazungumzo na Umoja wa Ulaya.
Iran inaelewa fika kuwa ni faida kwa Iran kutoipatia Marekani kisingizio chochote ya kuleta matata, na inaweza kutumia fursa hiyo kuendeleza uhusiano na Umoja wa Ulaya na kujipata faida za kiuchumi. Kutokana na wazo hilo na baada ya kupima kwa pande zote mbinu zake kuhusu suala la nyuklia zinazobadilika mara kwa mara hulegeza masharti katika dakika ya mwisho, kwa kufanya hivyo licha ya kuweza kutuliza Umoja wa Ulaya na pia inaweza kupata uungaji mkono kutoka nchi wanachama wengi wa Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki na kuitenga Marekani. Safari hii Iran imelegeza masharti katika wakati mwafaka, ni maendeleo ya mbinu zake kuhusu utatuzi wa suala la nyuklia.
Lakini, kama Iran itabadilisha tena msimamo wake, utatuzi wa tatizo la nyuklia nchini Iran bado utakuwa na safari ndefu.
Idhaa ya kiswahili 2005-01-06
|