|
Idara ya habari ya rais ya Ukraine imetangaza kuwa, rais Kuchma tarehe 5 alisaini amri ya kuvunja serikali, na kuitaka serikali ya sasa iendelee kutekeleza wajibu wake kabla ya serikali mpya kuanzishwa. Vyombo vya habari vya Ukraine vinaona kuwa, hii inaonesha kwamba mgogoro wa kisiasa ulioendelea kwa muda wa zaidi ya mwezi mmoja umetulia.
Tarehe 31 mwezi Oktoba mwaka jana, duru la kwanza la upigaji kura katika uchaguzi mkuu lilifanyika nchini Ukraine. Kwa sababu katika duru hilo, wagombea wote hawakupata nusu ya kura zilizohitajiwa, duru la pili lilifanyika tarehe 21 mwezi Novemba. Tume kuu ya uchaguzi ya Ukraine ilitangaza siku ya pili kuwa, mgombea wa urais ambaye pia ni waziri mkuu wa nchi hiyo Bw. Viktor Yanukovich alishinda kwenye uchaguzi mkuu huo. Chama cha upinzani cha Ukraine kinachoongozwa na mgombea wa urais Bw. Viktor Yushchenko pamoja na Marekani na nchi za Ulaya zilitilia shaka matokeo hayo, na kushutumu tume hiyo kwa kukiuka taratibu katika upigaji kura. Lakini serikali ya Russia ilikubali matokeo hayo.
Katika hali ambayo kulikuwa na maoni yenye migongano kuhusu matokeo hayo ya uchaguzi mkuu nchini na nje ya Ukraine, hali ya kisiasa nchini humo ilikuwa mbaya.
Mahakama kuu ya Ukraine tarehe 3 mwezi Desemba ilitangaza kuwa matokeo ya duru hilo la upigaji kura hayakubaliki kisheria kutokana na kukiukwa kwa taratibu, na kutangaza kufanyika duru jipya la upigaji kura. Kwa mujibu wa hukumu hiyo, duru la pili la upigaji kura katika uchaguzi mkuu lilifanyika tarehe 2 mwezi Desemba mwaka jana. Kutokana na matokeo ya kwanza yaliyotolewa tarehe 28 na tume kuu ya uchaguzi ya Ukraine, Bw. Yushchenko alimshinda Yanukovisch kwa karibu asilimia 8 ya kura zote. Lakini wakati huo, tume hiyo haikutangaza kuwa Yushchenko amechaguliwa kuwa rais.
Baadaye, ingawa Yanukovich alikata rufani, lakini kutokana na shinikizo kutoka pande mbalimbali, alitangaza tarehe 31 mwezi Desemba kuwa ameamua kujiuzulu uwaziri mkuu. Rais Kuchma tarehe 5 mwezi huu alikubali rasmi ombi lake la kujiuzulu, na kumteua naibu waziri mkuu wa kwanza wa zamani Bw. Nikolai Azarov kuwa kaimu waziri mkuu.
Wachambuzi wa kimataifa wanaona kuwa, uamuzi wa rais Kushima unaathiri kwa kiasi kikubwa kama matokeo hayo ya uchaguzi yanaweza kufanya kazi au la. Kwa hiyo, serikali ya Ukraine itabadilishwa muda mfupi ujao.
Kutokana na utulivu wa hali ya kisiasa nchini Ukraine, naibu mwenyekiti wa kwanza wa Baraza la Chini la Bunge la Russia Bw. Lyubovi Sliska ambaye alisimamia duru la pili la upigaji kura kwenye uchaguzi mkuu wa Ukraine alisema kuwa, wapigaji kura na wagombea wa urais wa nchi hiyo wamechoka na mgogoro huo wa kisiasa ulioendelea kwa muda mrefu, wana matumaini makubwa ya kurejesha utulivu. Aidha, wachambuzi wa Ukraine pia wanaona kuwa, mswada wa mageuzi ya kisiasa uliopitishwa na bunge la Ukraine tarehe 8 mwezi Desemba mwaka jana umegawanya upya madaraka kati ya bunge, serikali na rais, hii inasaidia kutuliza hali ya nchini humo.
Kutokana na athari za Russia na nchi za magharibi kwa Ukraine katika siku za usoni, wachambuzi wanaona kuwa, ingawa baada ya Yushchenko anayependelea Ulaya kushika madaraka, sera za kidiplomasia zitalenga kuharakisha mchakato wa kujiunga na Umoja wa Ulaya na shirika la NATO, lakini pia alieleza kwa mara nyingi kuwa, ataimarisha uhusiano wa kirafiki kati ya Ukraine na Russia. Zaidi ya hayo, Ukraine inaitegemea Russia kwa kiasi kikubwa katika sekta za maliasili, uchumi na biashara, kwa hivyo maendeleo ya uhusiano kati ya nchi hizo mbili huenda yakapungua, lakini siyo kwa kiasi kikubwa. Vyombo vya habari vinaona kuwa, bado haieleweki jinsi serikali mpya ya Ukaine itakavyoundwa na mwelekeo gani wa sera zake za kisiasa na kiuchumi utakaochukuliwa.
Idhaa ya Kiswahili 2005-01-06
|