Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-01-06 21:52:16    
Mji wa Beijing

cri

    Beijing ni mji mkuu wa Jamhuri ya Watu wa China. Si kama tu mji huo ni kituo cha kisiasa nchini China, bali pia ni kituo cha utamaduni, sayansi, elimu na mawasiliano. Mji huu uko kaskazini mwa Tambarare ya Huabei. Katika upande wa magharibi, kaskazini na mashariki ya mji huo kuna milima, na katika upande wa kusini mashariki ni tambarare. Hali ya hewa ya Beijing ni ya kanda ya fufutende. Kuna majira manne, majira ya spring huwa ni mafupi, katika majira ya joto mvua hunyesha, majira ya baridi huwa ni marefu na kuna baridi kali, na katika majira ya mpukutiko hali ya hewa huwa ni ya kupendeza.

    Mji wa Beijing ulianza kujengwa kuanzia Enzi ya Zhou ya Magharibi, wakati huo uliitwa Ji, na katika Enzi ya Madola ya Kivita ulikuwa mji mkuu wa Dola la Yan. Katika miaka elfu 1 baadaye, Mji wa Ji ulikuwa kituo muhimu cha kijeshi na kibiashara katika sehemu ya kaskazini mwa China. Kuanzia mwanzoni mwa karne ya 10, ulikuwa mji mkuu wa pili wa Enzi ya Liao na kuitwa Yanjing. Kwa sababu ulikuwa mji mkuu wa Enzi za kimwinyi za Jin, Yuan, Ming na Qing kuanzia mwaka 1115 hadi 1911, utamaduni wa mji huo ni mkubwa, kuna urithi mwingi wa kihistoria ambao ni maarufu duniani. Mjini Beijing kuna Roshani ya Tian'anmen ambayo ni alama ya Beijing na pia ni alama ya China, Uwanja wa Tian'anmen ambao ni uwanja mkubwa zaidi duniani, pia kuna kasri kubwa la kifalme, ukuta mkuu wa Badaling ambao ni ajabu duniani, hekalu la Tiantan, bustani ya kifalme ya Yiheyuan, pamoja na makaburi makubwa ya kifalme ya Enzi ya Ming. Miongoni mwa urithi huo, kasri la kifalme, ukuta mkuu na masalio ya sokwe mtu wa Beijing huko Zhoukoudian vimewekwa kwenye orodha ya urithi wa kiutamaduni duniani na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa.

    Tangu Beijing uwe mji mkuu wa Jamhuri ya Watu wa China mwaka 1949 sura yake Beijing imebadilika kwa kiasi kikubwa. Zamani uwanja wa Tian'anmen ulikuwa ni uwanja wa kifalme ambao raia wa kawaida hawakuruhusiwa kuingia. Hivi sasa uwanja huo umekuwa sehemu ambayo wakazi wa Beijing wanatembea, kufanya mikutano, kujiburudisha na kupumzika. Kando ya uwanja huo kuna ukumbi mkuu wa mikutano ya watu wa China, jumba la makumbusho la histoira ya China, jumba la makumbusho la mapinduzi ya China, mnara wa mashujaa wa China, na ukumbi wa makumbusho wa hayati mwenyekiti Mao. Kaskazini ya uwanja huo kuna barabara ya Chang'an ambapo kando yake kuna majengo mengi ya kisasa. Tangu miaka ya 80 karne iliyopita, ujenzi wa mji huo umepata maendeleo makubwa. Hoteli kubwa zaidi ya 200 na maduka makumi kadhaa ya ngazi ya juu yamesambaa katika eneo hilo. Maktaba ya kitaifa, kituo cha biashara ya kimataifa, kituo cha maonesho ya kimataifa, jumba la maonesho ya sanaa la China na kituo cha magharibi cha garimoshi cha Beijing vimejengwa mjini Beijing. Na ujenzi wa barabara, madaraja na sehemu mpya ya mji wa Beijing umeufanya mji huo kuwa wa kisasa zaidi. Hivi sasa ukitazama kutoka kilele cha mlima katika bustani ya Jinshan mjini Beijing, utagundua kuwa majengo marefu yamesambaa mjini Beijing, na kuleta mandhari nzuri mpya ya mji huo.

Idhaa ya Kiswahili 2005-01-06