|
Baada ya tetemeko la ardhi na mawimbi makubwa yaliyosababishwa na tetemeko hilo kutokea tarehe 26 mwezi Desemba mwaka jana katika bahari ya Hindi, jumuiya ya kimataifa ikiwa na moyo wa kibinadamu ilifululiza kuzisaidia sehemu zilizokumbwa na maafa kwa njia mbalimbali katika kupambana na maafa na kufanya ukarabati. Lakini jambo lililofuatiliwa ni kuwa nchi zinazoendelea pamoja na Afghanistan na baadhi ya nchi za Afrika pia zilitoa michango yao. Ingawa michango hiyo siyo mikubwa, lakini imefafanua ipasavyo msemo uitwao "kutoa ni moyo na sio utajiri".
Habari zinasema kuwa wizara ya ulinzi ya Afghanistan tarehe 5 ilieleza kuwa ingawa Afghanistan ina shida, lakini Afghanistan ni mmoja wa jumuiya ya kimataifa. Watu wa Afghanistan wanatoa huruma kwa nchi zilizopatwa na hasara kubwa na kuzipelekea India na Sri Lanka madaktari 12 pamoja na misaada ya dawa na vitu. Baadhi ya nchi za Afrika pia zilifululiza kuwapatia watu waliokumbwa na maafa misaada ya dharura. Guinea Bissau ilitoa msaada wenye thamani ya dola za kimarekani laki 2, Senegal thamani ya Euro laki 1.5, Mauritius dola za kimarekani laki 2.5 na chama cha hilari nyekundu cha Morocco kiliahidi Euro elfu 23. Zaidi ya hayo, Vietnam, Laos, Cambodia, Tunisia na Albania pia zilitoa michango ya fedha na vitu.
China ikiwa nchi kubwa kabisa inayoendelea, imetoa michango mikubwa katika historia yake ya utoaji misaada. Baada ya kuchangia bidhaa zenye thamani ya dola za kimarekani milioni 2,63, China iliongeza mchango wenye thamani ya dola za kimarekani milioni 60 na kuamua kufuta madeni yote inayoidai Sri Lanka yaliyofikia muda wa kulipwa. Tarehe 6, waziri mkuu wa China Wen Jiabao alitangaza kwenye mkutano maalum uliofanyika mjini Djakarta, kuongeza tena mchango wa fedha taslimu ya dola za kimarekani milioni 20. Kabla ya hapo, vikundi vya madaktari na utoaji misaada vya China viliwasili katika sehemu zilizokumbwa na maafa na bidhaa mbalimbali pia zimefikishwa huko. Wakati huo huo, mashirika na watu binafsi wa China pia wamefululiza kuchangia fedha. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Kofi Annan alieleza kuwa katika kupambana na maafa hayo, sio tu serikali ya China ilifanya vitendo kwa haraka, wananchi wa China pia wameonesha upendo wao kwa watu waliokumbwa na maafa. Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Bw. Colin Powell pia alisifu vitendo vilivyofanywa na China katika kutoa misaada.
Kama waziri mkuu Wen Jiabao alivyoeleza kwenye mkutano huo maalum kuwa ingawa China ni nchi inayoendelea, lakini misaada iliyotolewa na China haina ubinafsi wala sio yenye masharti. Balozi wa China katika ofisi ya Geneva ya Umoja wa Mataifa Bw. Sha Zukang tarehe 6 alieleza kuwa China ni nchi inayoendelea, na misaada ya China ni ya nchi maskini kuzisaidia nchi maskini nyingine.
Tunaweza kusema kuwa nchi zilizotoa msaada usio na uchoyo zinastahili kusifiwa bila kujali ni nchi kubwa au ndogo, tajiri au maskini na katika hali hiyo, nchi maskini kuzisaidia nchi maskini kuna maana kubwa zaidi. Wachambuzi wanaainisha kuwa kuaminiana na kushirikiana kati ya nchi na nchi ni muhimu sana ili kupambana na changamoto kwa binadamu wote.
Idhaa ya kiswahili 2005-01-07
|