|
Katibu mkuu wa Ikulu ya Palestina Bw. al-Taib Abdel Rahim tarehe 9 alitangaza huko Ramallah, mji wa kando ya magharibi ya mto Jordan kuwa, kutokana na matokeo ya mwanzo, mgombea wa Fatah, kundi kubwa la chama cha ukombozi cha Palestina Bw. Mahmoud Abbas ameshinda katika uchaguzi mkuu wa Palestina, na kuwa mwenyekiti mpya wa mamlaka ya utawala wa Palestina. Bw. Abbas atakuwa kiini cha viongozi wa awamu mpya ya Palestina, na kuwa mrithi na mtangulizi wa kazi ya ukombozi wa taifa la Palestina.
Katika muda mrefu uliopita, Bw. Abbas mwenye umri wa miaka 69 mwaka huu alifanya mapambano ya kufa na kupona kwa ajili ya ukombozi na uhuru wa taifa la Palestina. Bw. Abbas alizaliwa katika familia iliyoendesha biashara ndogo huko Safed, kijiji kilichoko sehemu ya Palestina ambacho sasa kinadhibitiwa na Isarel. Alikimbilia Syria na kuwa mkimbizi kutokana na vita vya kwanza vya mashariki ya kati. Huko Damascus, mji mkuu wa Syria, Bw. Abbas alikuwa mwanafunzi hodari wa sheria, baada ya hapo alienda Urusi ya zamani na kupata shahada ya udaktari wa historia huko Moscow. Kama ilivyokuwa kwa vijana wengi wa wakati huo, matumaini makubwa ya kurejea nyumbani kwao yalimhimiza Bw. Abbas kujiunga na harakati za ukombozi wa Palestina. Mwaka 1965, baada ya kukutana na Bw. Yasser Arafat, Bw. Abbas aliacha kazi katika kampuni ya mafuta yenye mshahara mkubwa nchini Qatar, na kuanzisha Chama cha Ukombozi cha Palestina akiwa pamoja na Bw. Arafat, na kujiunga rasmi na kundi la Fatah lililokuwa likiongozwa na Bw. Arafat. Baada ya hapo, Bw. Abbas alikuwa akifuatana na Bw. Arafat kufanya mapambano kwa pamoja nchini Jordan, Lebanon na Tunisia.
Bw. Abbas anachukuliwa kama ni kiongozi anayeambatana na hali halisi. Katika miaka ya 70 ya karne iliyopita, alianza kutambua kuwa, haiwezekani "kuwafukuzia wayahudi baharini", tena Palestina itapata hasara isiyo na maana yoyote kwa kupambana na ndege za kivita na makombora ya Israel kwa kutumia baruti na na roketi za kienyeji. Bw. Abbas anaona kuwa, wapalestina wanapaswa kujipatia vitu vilivyopotezwa kwenye uwanja wa mapambano kwa kupitia mazungumzo, na wala sio kwa kufanya mapambano ya mabavu. Msimamo huo wa Bw. Abbas ulimfanya awe mwakilishi muhimu wa mazungumzo ya amani kati ya Palestina na Israel. Kutokana na idhini ya Bw. Arafat, alifanya mazungumzo ya siri na maofisa wa Israel huko Oslo, mji mkuu wa Norway, na kukihimiza Chama cha Ukombozi cha Palestina na Isarel kukubaliana. Aidha, mwaka 1993, nchini Marekani, Bw. Abbas na waziri wa mambo ya nje wa Israel wa wakati huo Bw. Shimon Peres walisaini Mkataba wa Oslo unaohusu kujiendesha kwa Palestina. Hayo ni matokeo ya kihistoria katika mchakato wa amani ya Mashariki ya Kati. Mwaka 1996, Bw. Abbas aliyeaminiwa sana na Bw. Arafat alichaguliwa kuwa katibu mkuu wa Kamati ya utendaji ya chama cha ukombozi cha Palestina, na kuchukuliwa kama ni mrithi wa Bw. Arafat. Lakini, kutokana na migongano kuhusu mgawanyo wa madaraka na sera dhidi ya Israel na Bw. Arafat, Bw. Abbas alitangaza kujiuzulu baada ya kushika wadhifa kwa miezi minne.
Baada ya kuumwa vibaya kwa Bw. Arafat mwishoni mwa mwezi Oktoba mwaka jana, Bw. Abbas alijitokeza akiwa katibu mkuu wa kamati ya utendaji wa Chama cha Ukombozi cha Palestina, na alichaguliwa kuwa mwenyekiti mpya wa kamati hiyo baada ya kufariki dunia kwa Bw. Arafat.
Kuhusu za ndani, Bw. Abbas anashikilia kufanya mageuzi ya kisiasa, kupambana na ufisadi, kuanzisha jamii inayofuata sheria, na kufanya mageuzi ya utaratibu wa usalama. Katika sera za nje, anatetea kutatua migogoro kati ya Palestina na Israel kwa njia ya mazungumzo ya amani, na kulinda kithabiti maslahi ya kimsingi ya Palestina katika masuala kuhusu hadhi ya Jerusalem, mamlaka ya kurejesha wakimbizi wa Palestina, na utawala wa ardhi zinazodhibitiwa na Israel. Jumuiya ya kimataifa inaona kuwa, ni uchaguzi wa kihistoria kumchagua Bw. Abbas kuwa mwenyekiti wa mamlaka ya utawala wa Palestina.
Idhaa ya Kiswahili 2005-01-10
|