|
Nchi zilizoathirika na maafa makubwa ya dhoruba lililosababishwa na tetemeko la ardhi kwenye bahari ya Hindi zimeingia katika kipindi cha ukarabati. Kutokana na makadirio, ukarabati huo pengine unahitaji muda wa miaka mitano hadi miaka 10 kabla kukamilika, na gharama za ukarabati zitazidi dola za Kimarekani bilioni 10. Wachambuzi wanaona kuwa kazi ya ukarabati ni ngumu na kabambe, nchi yoyote haiwezi kufanya kazi hiyo peke yake, kwa hiyo misaada ya jumuiya ya kimataifa ni ya lazima.
Ukarabati huo kwa ufupi unahitaji kazi za aina tatu zifuatazo:
Kwanza kabisa, wananchi walioathirika warudi katika maisha ya kawaida, ikiwa ni pamoja na mahitaji ya lazima ya kimaisha na pia wawe na afya kisaikolojia. Wataalamu wanaona kuwa kuondoa hofu ya maafa iliyopo akilini mwao kunahitaji juhudi za miaka mingi. Isitoshe, kazi ya kufufua uchumi pia ni muhimu sana, na hasa sekta ya utalii katika nchi zilizoathirika, kwani sekta hiyo ni mhimili muhimu wa uchumi katika nchi hizo.
Pili, ni kazi ya kuanzisha mfumo wa utabiri wa dhoruba la bahari. Kutokana na kuwa kabla ya hapo maafa kama hayo hayakuwahi kutokea katika bahari ya Hindi, mfumo kama huo wa utabiri haukuanzishwa. Maafa hayo yaliyosababishwa na tetemeko la ardhi katika bahari ya Hindia yamezifanya nchi za mwambao kutambua umuhimu wa utabiri huo. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Kofi Annan pia alisisitiza kuwa kuanzisha mfumo huo ni jambo la kipaumbele.
Tatu, ni "kukarabati" kimawazo, yaani binadamu wawe na mawazo ya kuzingatia mazingira. Wataalamu wanaona kuwa shughuli za binadamu za kuharibu mazingira ni sababu muhimu ya kuleta hasara kubwa ya mali na maisha ya binadamu. Mahoteli mengi yamejengwa pwani, na watu wanajazana. Kwa kawaida, katika sehemu karibu na ukingo wa bahari kuna miamba na mimea ambayo inaweza kuzuia ukali wa dhoruba, lakini kutokana na shughuli za binadamu vizuizi hivyo vimepungua. Ni sawa kusema kuwa maafa ya dhoruba lililosababishwa na tetemeko la ardhi kwenye bahari ya Hindi, sio onyo kwa nchi zilizoathirika tu, bali pia kwa dunia nzima. Binadamu hawawezi kukwepa au kupunguza maafa bila kuhifadhi maumbile na kuitunza dunia.
Lakini hali ilivyo sasa inaonesha kuwa kutimiza lengo hilo ni vigumu.
Kwanza, misaada ya fedha inaweza kufikishwa kwenye mahali panapohitajika bila kuchelewa au la. Hivi sasa ahadi za misaada ya fedha za jumuiya ya kimataifa imefikia dola za Kimarekani bilioni 5, pamoja na ahadi hizo, nchi nyingi na mashirika mengi ya kimataifa yameahidi kupunguza na kusamehe madeni ya nchi zilizoathirika. Lakini wakati huo huo maoni ya vyombo vya habari yanaona kuwa tatizo lililopo sasa ni utekelezaji wa ahadi hizo. Kwani hapo zamani nchi fadhili zilizotoa ahadi kama hizo zilighairi kutoa misaada hiyo, kutokana na hali hiyo watu wanaomba jumuiya ya kimataifa, na hasa nchi wafadhili, benki ya dunia, benki ya maendeleo ya Asia, benki ya maendeleo ya Kiislamu pamoja na mashirika mengine ya fedha yatoe dhamana ya fedha ili nchi hizo kweli zipate fedha zilizoahidiwa.
Pili, Kazi ya ukarabati ni ya muda mrefu, lakini kazi hiyo sio rahisi kama ikiendelea bila kukatika. Ili kuhakikisha nchi zilizoathirika zinapata misaada mfululizo bila kukwama, mkutano wa viongozi wa Umoja wa Asia ya Kusini Mashariki uliofanyika tarehe 6 ulitaka katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa amteue mwakilishi atakayekuwa na jukumu la kuitisha mkutano wa nchi wafadhili ili kuhakikisha juhudi za jumuiya ya kimataifa zinaendelea bila kukwama.
Historia ya maendeleo ya ustaarabu ndio mapambano ya binadamu dhidi ya maafa ya kimaumbile. Kama waziri mkuu wa China Wen Jiabao alivyosema kuwa maafa ya dhoruba lililosababishwa na tetemeko la ardhi kwenye bahari ya Hindi sio tu maafa ya nchi husika bali pia ni ya binadamu wote. Kwa hiyo ukatabati hauwezi kufanikiwa bila biandamu kushirikiana katika wakati wa shida.
Idhaa ya kiswahili 2005-01-10
|