|
Wasikilizaji wapendwa, serikali ya Sudan na chama cha upinzani kinachojulikana kwa jina la chama cha ukombozi cha watu wa Sudan wamesaini mkataba wa amani tarehe 9 huko Nairobi, mji mkuu wa Kenya. Mkataba huo unahusu masuala mengi muhimu yakiwa ni pamoja na usimamishaji wa mapambano, kugawana madaraka na mali. Hiyo ni hatua iliiyochukuliwa kwa ujasiri na pande hizo mbili ya kumaliza vita vya wenywe kwa wenywe vilivyodumu kwa miaka 21, ambayo inaonesha pia kuwa vita vya wenywe kwa wenywe vilivyodumu kwa muda mrefu zaidi barani Afrika vimemalizika. Sasa tunawaletea maelezo kuhusu mkataba wa amani wa Sudan ambao ni mnara wa historia katika bara la Afrika.
Mkataba huo wa amani ya pande zote umefikiwa kwa shida kubwa. Tangu vita vya wenywe kwa wenywe vilipolipuka mwaka 1983, watu milioni 2 wameuawa, watu milioni 4 hawana mahali pa kujisitiri na kufanya Sudan kuwa moja ya nchi maskini kabisa duniani. Kutokana na juhudi za jumuia ya kimataifa, hususan umoja wa nchi za Afrika, baada ya kufanya mazungumzo kwa miaka 10, pande hizo mbili zimepania kumaliza vita hivyo na kukubali kufanya usuluhishi. Kutokana na mkataba huo, serikali ya Sudan itagawana madaraka ya serikali na chama cha ukombozi cha watu wa Sudan, na chama cha ukombozi cha watu wa Sudan, ambacho kimekuwa kikitaka kuanzisha nchi yao huru kusini mwa Sudan, kinakubali kujiendesha tu ndani ya nchi ya Sudan. Pande mbili zimekubali kulinda umoja wa taifa katika kipindi cha mpito cha miaka 6.
Kusainiwa kwa mkataba wa amani wa pande mbili kumeleta matumaini ya kuleta amani kamili nchini Sudan. Licha ya vita vya ndani kati ya kaskazini na kusini, suala la Darfur katika sehemu ya magharibi mwa Sudan pia ni suala linalofuatiliwa sana na jumuiya ya kimataifa. Suala kati ya sehemu ya kaskazini na kusini na suala la Darfur, yote yanahusiana na migongano ya kikabila na kidini na maslahi ya kiuchumi. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Kofi Annan alisema kuwa, kusainiwa kwa mkataba wa amani kati ya kaskazini na kusini ya Sudan kutaweza kuwa mfano wa kuigwa kwa utatuzi wa mgogoro wa Darfur. Yaani chini ya uongozi wa umoja wa Afrika, kutafuta uwiano wa maslahi unaoambatana na pande zote kwa kufanya mazungumzo ya amani.
Kusainiwa kwa mkataba wa amani si kama tu ni muhimu katika kulinda mamlaka na ukamilifu wa ardhi wa Sudan, bali pia kutahimiza utulivu na maendeleo ya bara la Afrika. Vita vya ndani vya Sudan vimesababisha vurugu ya kisiasa nchini humo, pia imehatarisha amani na utulivu wa nchi jirani. Kusainiwa kwa mkataba wa amani ya Sudan kumeondoa chanzo cha vurugu hiyo. Jambo linalofurahisha ni kuwa, viongozi wa nchi na mashirika ya Afrika wameshafahamu kuwa, kutokana na migogoro ya kisilaha, bara la Afrika limekuwa sehemu iliyo nyuma kabisa kiuchumi duniani, watu wa Afrika wanatarajia sana kuishi maisha mazuri katika hali ya amani. Nchi za Afrika zimeanza kujenga mazingira yenye amani na utulivu, na kuweka hali nzuri kwa maendeleo na usitawi wa Afrika. Kutokana na juhudi za pamoja za nchi za Afrika, sehemu nyingi zenye vurugu ya kijeshi barani Afrika sasa zimepunguza wasi wasi wa kisiasa, na bara la Afrika limeanza kufuata njia ya kujiendeleza.
Jambo linalofuatiliwa na jumuiya ya kimataifa ni kuwa, kusainiwa kwa mkataba wa amani ya Sudan ni jambo la kufurahisha, lakini jinsi ya kuhakikisha mkataba huo unatekelezwa kwa ufanisi bado ni changamoto kubwa inayoikabili serikali ya Sudan na chama cha ukombozi cha watu wa Sudan SPLM. Hivyo jumuiya ya kimataifa inapaswa kutoa misaada ili kuhimiza mkataba huo wa amani utekelezwe vizuri. Binadamu wanatumai kuwa, watu wa Sudan waliokumbwa na maumivu makali ya kivita wataweza kufurahia amani halisi.
Idhaa ya Kiswahili 2004-01-10
|