Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-01-11 11:07:58    
Barua 0109

cri
    Msikilizaji wetu Kaziro Dutwa S.L.P 209 Songea, Tanzania ametuletea barua akisema kuwa, amefurahi sana kupokea barua toka kwetu ikimjulisha kwamba tumepokea barua yake ya majibu ya shindano letu la chemsha bongo kuhusu ujuzi wa "Miaka 55 ya China Mpya". Anasema kwa kweli amefarijika kwa kiasi kikubwa isivyo kifani. Kwani hiyo imemwonyesha kwamba utaratibu wa kawaida hapa CRI bado haujabadilika; yaani kupokea barua ya msikilizaji na kumtumia barua ya majibu mara moja.

    Anasema kuwa, hivi kwa sababu amekuwa akituma barua nyingi zenye michango mbalimbali kwa CRI ikiwemo: Makala juu ya vipindi mbalimbali alivyosikiliza, maoni, salaam na mengine mengi lakini ni sehemu ndogo sana iliyosomwa au kujibiwa kwa barua kwa kweli hii imekuwa ikimvunja moyo sana hadi kufikiria kukata tamaa, kwani michango yote anayotoa imekuwa ikimgharimu muda na pesa ili kukidhi haja yake ya kusikia salaam au barua zake zikipeperushwa hewani na CRI, na kwa kweli hiyo ndiyo furaha yake kubwa sana.

    Anasema pamoja na yote hata lakini amekuwa akipiga moyo konde na kujikongoja kuandika, akiweka matumaini yake kwamba iko siku tatizo hili litakoma japo haelewi ni lini na kifua mbele atasikia barua na kadi zake za salaam zikirushwa hewani kupitia mitambo bora ya CRI.

    Hapa tunapenda kumwambia Bwana Dutwa kuwa, kweli tunajua sana kuwa yeye ni msikilizaji wetu na rafiki yetu wa tangu zamani, na ametuletea barua nyingi na kutoa maoni mara kwa mara. Kwa kawaida, yeye na wasikilizaji wengine hututumia vizuri maoni na mapendekezo, hivyo kila tukipata barua yake huwa tujitahidi kuzichagua na kuzisoma, kwani kweli tunaona barua zake huandikwa vizuri, na tunapenda kuzisoma ili kuwafurahisha wasikilizaji wetu pia. Lakini huenda inawezekana kwa sababu moja au nyingine, kwa wakati fulani yeye labda anakuwa na shughuli na kukosa fursa ya kusikia tukisoma barua zake hewani. Tunapenda kuwaambia wasikilizaji wetu wengine wote kuwa tunathamini sana juhudi na michango yenu kwetu, na tunajitahidi kufanya kila tunaloweza kuwapa nafasi sawa ili msikike hewani.

    Lakini kwa hali halisi, kutokana na kutokuwa na nguvu kazi ya kutosha katika idara yetu huenda hatukujibu barua zake ipasavyo. Hata hivyo siku hizi katika idhaa ya Kiswahili ya Radio China kimataifa, wengi wa wafanyakazi ni vijana ambao walianza kazi katika idhaa yetu mwezi Agosti mwaka 2004, ambao bado wanatakiwa kufanya juhudi kujifunza mengi. Hivyo tunaomba wasikilizaji wetu waweze kutuelewa na kutokata tamaa, kama wakati fulani wanahisi kuwa hatujawahudumia vizuri kutokana na sababu fulanifulani. Lakini kwa kweli tuna nia ya dhati ya kumfurahisha kila msikilizaji wetu, kwa hiyo tunaomba mtuelewe.

    Bwana Dutwa anasema, Mwaka 2004 umemalizika, na mawio ya jua la mwaka mpya wa 2005 unaangaza dunia, tuombeane heri tuuone na kuupokea mwaka huo mpya wa Kichina ambao hujiri mwezi wa Februari kwa kalenda ya kichina, japo hana hakika sana mwaka huu utakuwa ni mwaka wa mnyama gani. Anasema vyovyote iwavyo bila shaka utakuwa ni mwaka wa heri na fanaka kwa CRI na kwa wasikilizaji wote, pia kwa dunia yote na uwe wa utulivu na uje na ufumbuzi wa dhati wa mizigo yote inayoielemea dunia kwa sasa yaani ile ya magonjwa katili ya malaria na Ukimwi, magonjwa ambayo licha ya juhudi kubwa ya binadamu kujiepusha nayo, yamezidi kushika kasi na kuota mizizi katika miili na mioyo ya binadamu, yakiwaacha baadhi ya binadamu hasa nchi zilizo kusini mwa Sahara wakiwa wamekata tamaa ya maisha kwani hawana uhakika wa maisha yao ya kesho!

    Tunapenda kumuarifu Bw Kaziro Dutwa na wasikilizaji wetu wengine kuwa mwaka mpya ujao wa jadi kwa kalenda ya kichina, utakuwa mwaka wa kuku na utaanza tarehe 9 mwezi Februari. Tutawaletea wasikilizaji wetu maelezo mengine kuhusu mwaka wa kuku, wakati wa kusherehekea mwaka mpya wa jadi msikose kutusikiliza.

    Bwana Dutwa pia anasema kuwa katika baadhi ya mambo, Mwaka 2004 umekuwa ni wa kukatisha tamaa na kuondoa matumaini kabisa kwa binadamu wapendao amani. Baadhi ya matukio yameifamnya hadhi ya Umoja wa Mataifa idhalilishwe na kubezwa kabisa, hivyo dunia imejikuta kuyumba kwa chombo huru kinachosimamia maslahi au haki za binadamu mmoja mmoja au taifa.

    Bwna Kaziro Dutwa pia amegusia baadhi ya Mambo yaliyotokea duniani kuhusiana na tatizo la ugaidi hadi kufikia baadhi ya nchi kutajwa kuwa ni "Nchi ambazo ni mhimili wa Uovu!", yeye anasema kuwa hili ni jina la kudhalilisha na kughadhabisha. Hapa anasema tangazo kama hilo linaweza kuonekana kama ni vita dhidi ya nchi hizo ambazo zina haki ya kujitawala na kufuata sera zao kulingana na mazingira ya nchi na watu wao. Kauli hii iliamsha hisia za chuki kwa baadhi ya watu na kutaka kulipiza kisasi.

    Bwana Dutwa anasema , Marekani ilivamia na kuzikalia nchi mbili kwa mpigo yaani Afghanistan na Iraq bila idhini ya Umoja wa Mataifa kitendo ambacho kinaonesha udhalilishaji kwa chombo muhimu kabisa ambacho kilikuwa ni kimbilio la wanyonge hapo nyuma na ambacho kiliwekwa na jamii ya kimataifa ili kulinda maslahi na haki za binadamu. Lakini Marekani ilifanya hivyo bila kujali umoja wa mataifa.

    Bwana Kaziro Dutwa anaendelea kuzungumzia vita dhidi ya ugaidi kwa kusema Osama Bin Laden ambaye alifuatwa huko Afghanistan haonekani! Anauliza Je, hii ni kweli au mazingahombwe? Anasema silaha hatari zilizokuwa zikitafutwa Iraq zimepotea, gaidi hatari amepotea, na amani duniani imepotea. Je tunafahamu vyote hivyo vimepotelea wapi?

    Anamaliza kwa kuuliza nyoka mwenye sumu kali akipotelea kwenye chumba cha giza kwa uzembe je, chumba hicho kitakalika? Anasema nchi maskini zinatapatapa karibu kukata roho kwa kusongwa na magonjwa na umaskini, hivi kelele zao za kutaka usaidizi zitazaa nini iwapo nyoka aliyepotelea gizani hajapatikana?

Idhaa ya kiswahili 2005-01-11