|
Mkutano wa kimataifa kuhusu maafa yaliyosababishwa na tetemeko la ardhi katika bahari ya Hindi ulifanyika jana huko Geneva. Kwenye mkutano huo nchi mbalimbali zilijadiliana na kuafikiana wazo la namna moja kuhusu kutimiza ahadi ya kutoa misaada ya fedha, Mkutano huo umeonesha moyo wa ushirikiano mkubwa wa binadamu katika dhiki na faraja.
Mawaziri na wajumbe 250 kutoka nchi zaidi ya 80 wamehudhuria mkutano huo.
Baada ya maafa kutokea katika nchi za pwani za bahari ya Hindi, jumuiya ya kimataifa ilianza harakati za kutoa misaada. Hadi hivi sasa misaada ya fedha iliyoahidiwa imefikia dola za Kimarekani zaidi ya bilioni 4. Lakini kabla ya hapo hali ya kughairi kutekeleza ahadi iliwahi kutokea mara nyingi. Mathalan, Desemba mwaka 2003 tetemeko la ardhi lilitokea nchini Iran, na jumuiya ya kimataifa iliahadi misaada ya fedha dola za Kimarekani milioni 115, na Umoja wa Mataifa mwishowe iliamua kuhitaji milioni 33 tu kwa kuzingatia hali ilivyo. Hata hivyo hadi sasa dola za Kimarekani milioni 17 tu zimefikishwa mikononi mwa waathirika, na mfano mwingine ni kwamba, mpango wa Umoja wa Mataifa wa kukusanya misaada ya kibinadamu kila mwaka pia mara nyingi huwa ni mpango wa maneno matupu. Kutokana na hali hiyo, baadhi ya mashirika ya Umoja wa Mataifa yalikuwa na wasiwasi kwamba hali ya kughairi kutekeleza ahadi inaweza kutokea tena.
Lakini matokeo yaliyopatikana katika mkutano huo yameufurahisha Umoja wa Mataifa bila kutegemea. Baada ya mkutano kumalizika mwenyekiti wa mkutano huo Bw. Jan Egeland aliwaambia waandishi wa habari akisema kwamba matokeo ya mkutano huo yanatia moyo, kwamba nchi nyingi zimeahidi kutekeleza ahadi ya kutoa misaada mapema iwezekanavyo, na pia alitangaza kuwa misaada ya fedha dola za Kimarekani milioni 717 iliyoahidiwa itatimizwa katika muda mfupi ujao. Bw. Egeland alisema, kwenye mkutano katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Kofi Annan aliitaka 73% ya misaada ya fedha ihakikishwe, na asilimia nyingine iliyobaki itimizwe si zaidi ya muda wa nusu mwaka. Kwa furaha Bw. Egeland alisema "Hiki ni kiasi kikubwa kabisa cha misaada ya fedha kukusanywa na Umoja wa Mataifa katika muda mfupi", na kwamba "harakati hiyo imefungua ukurasa mpya katika mshikamano wa kimataifa".
Kwenye mkutano huo nchi mbalimbli zilitoa ushauri na zilifikia maafikiano kimawazo kuwa kwanza, Umoja wa Mataifa uwe uongozi wa kuratibu misaada hiyo kwani una uzoefu wa kutosha katika kupanga na kufanya mapambano dhidi maafa. Pili, kazi ya mapambano dhidi ya maafa na ukarabati lazima iwe katika hali ya utaratibu na yenye tija kubwa bila kukoma. Tatu, ni haja ya kuanzisha mfumo wa uchunguzi na utabiri wa maafa ya kimaumbile katika nchi zinazoendelea. Nne, misaada ya kimataifa inapaswa ilingane na mahitaji ya nchi zilizoathirika na kuheshimu maoni yao ya kupeleka kwanza misaada kwenye sehemu zilizochaguliwa. Waziri wa fedha wa Sri Lanka, nchi iliyoathirika na janga hilo, Bw. Sarath Amunugama aliwaambia waandishi wa habari akisema kuwa anaridhishwa na matokeo ya mkutano huo.
Mjumbe wa serikali ya China, ambaye pia ni naibu waziri wa mambo ya nje Bw. Shen Guofang alieleza kuwa hali ya kutoa misaada mikubwa haijawahi kutokea nchini China. Alisema, hadi tarehe 7 misaada ya serikali na ya raia ya China jumla imekuwa dola za Kimarekani zaidi ya milioni 133, na misaada ya raia inaendelea kuongezeka. Hadi mwishoni mwa mwezi huu misaada ya mali na fedha itatimizwa zaidi ya nusu, na serikali ya China kwa haraka ilipeleka vikundi vyake vya matibabu. Zaidi ya hayo serikali ya China imeamua kufuta madeni yote yaliyofika kipindi cha kulipwa ya serikali ya Sri Lanka.
Idhaa ya kiswahili 2005-01-12
|