Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-01-13 11:10:45    
Wachina watoa misaada kwa watu wa nchi zilizokumbwa na maafa ya dhoruba lililosababishwa na tetemeko la ardhi

cri
Baada ya kusikia tangazo la kuwahamasisha wateja walio dukani kuchangia fedha kwa ajili ya watu wa nchi zilizokumbwa na maafa ya dhoruba lililosababishwa na tetemeko la ardhi kwenye bahari ya Hindi, watu mia kadhaa walikuwa wamepanga mstari wa kuchangia fedha. Yuan 50 na yuan 100 zilizotolewa na wateja ziliwekewa kwenye sanduku la kuchangia fedha. Maafa yaliyotokea tarehe 26 Desemba mwaka jana yaliwahuzunisha sana wachina, watu wa sekta mbalimbali wametoa michango ya fedha au vitu kwa hiari kwa watu wa nchi zilizokumbwa na maafa hayo.

Tarehe 31 Desemba ya mwaka jana, waziri mkuu wa China Bwana Wen Jiabao alikutana na mabalozi wa nchi zilizoathirika na maafa na wajumbe wa mashirika ya kimataifa nchini China. Katika mkutano huo, balozi wa Sri Lanka nchini China Bwana Nihal Rodrigo alieleza kuwa: "mchana wa siku ile, wanafunzi wawili wa shule ya sekondari ya chini ya Beijing walikuja kwenye ubalozi wa Sri Lanka, na kuomba kuchangia yuan mia nne kwa watu waliokumbwa na maafa wa Sri Lanka. Balozi Rodrigo alitiwa moyo sana na shughuli hiyo. Alisema kuwa, tangu kutokea maafa ya tetemeko la ardhi na dhoruba lililosababishwa na tetemeko hilo, serikali ya China na watu wake wametoa misaada mingi na ya dhati kwa nchi zilizoathirika na maafa hayo.

Wanafunzi hao wawili wote ni wa kidato cha tatu cha sekondari ya chini. Mmoja wa wanafunzi hao anayeitwa Fu Jin mwenye umri wa miaka 14, alipohojiwa na mwandishi wetu wa habari alisema kuwa:

"Tulipopata habari kuwa nchi kadhaa zimekumbwa na maafa, tulifikiria kutoa mchango kwa njia fulani kwa watu waliokumbwa na maafa. Tulipata simu ya ubalozi wa Sri Lanka nchini China, siku ya pili, tulikwenda katika ubalozi wa Sri Lanka. Hii ni mara yangu ya kwanza kukutana na wanadiplomasia, tulikaribishwa vizuri."

Licha ya kuchangia fedha, wanafunzi hao wawili pia walimwandikia barua rais wa Sri Lanka Bibi Chandrika Bandaranaike Kumaratunga. Walimwambia kuwa, wanawahurumia sana watu wa Sri Lanka waliokumbwa na maafa. Wanaamini kuwa, kutokana na misaada ya nchi mbalimbali duniani, wananchi wa Sri Lanka wataweza kuyashinda matatizo yoyote. Pia walisema wanapenda kujifunza lugha ya Sri Lanka ili waweze kuwasiliana na watu wa Sri Lanka bila matatizo.

Hivi sasa katika mitaa, idara na shule mjini Beijing vimewekwa vituo vya kutoa michango kwa ajili ya kuwasaidia watu wa nchi zilizoathirika na maafa.

Kutoa mchango kwa watu waliokumbwa na maafa ni desturi nzuri ya watu wa China, dhoruba lililosababishwa na tetemeko la ardhi katika bahari ya Hindi limesababisha vifo vya watu laki 1.5. Baada ya kutokea kwa maafa hayo, wakazi wa mji wa pwani wa Dalian walitangulia kutoa mchango. Bibi Liu Junfang ni mfanyakazi mstaafu. Japokuwa yeye si tajiri, lakini alitoa yuan 500, alisema:

"Nilisikitika sana nilipopata habari kutoka kwenye magazeti kuwa, watu wengi waliokumbwa na maafa hayo hata hawana maji ya kunywa, nilishaurianaa na mume wangu, na tukaamua kutoa mchango kidogo."

Watu wengi wa China walisherehekea mwaka mpya wa 2005 kwa kutoa mchango wa fedha au vitu kwa watu wa nchi zilizokumbwa na maafa. Imefahamika kuwa, karibu miji mikubwa yote nchini China imeweka vituo vya utoaji misaada kwa watu waliokumbwa na maafa. Chama cha msalaba mwekundu cha China na shirikisho kuu la utoaji michango la China na matawi yake katika miji mbalimbali yameweka vituo vya kupokea michango kwenye mitaa yenye watu wengi wanaopitapita. Kati ya watoaji michango, kuna makarani, wanafunzi, wafanyakazi na vibarua kutoka vijijini.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa tarehe 9 na "Ofisi ya uratibu wa utoaji misaada wa wachina kwa nchi zilizokumbwa na maafa" katika wizara ya huduma za raia ya China, jumla ya michango iliyopokelewa na chama cha msalaba mwekundu cha China na matawi yake yaliyoko katika sehemu mbalimbali kutoka kwa watu mbalimbali kwa ajili ya nchi zilizoathirika katika maafa hayo, imefikia yuan za renminbi milioni 124.83, sawa na dola za kimarekani milioni 15.2.

Habari nyingine zinasema kuwa maonesho ya michezo ya sanaa yaliyoandaliwa na Radio China Kimataifa pamoja na vyombo 24 vya habari vya Beijing kwa kushirikiana na tawi la chama cha msalaba mwekundu la Beijing, yalifanyika tarehe 9 hapa Beijing. Fedha zilizopatikana kutokana na tikiti zilizouzwa zitatolewa kama zawadi kwa nchi zilizokumbwa na maafa.

Licha ya China bara, watu wa Hong Kong, Macao na Taiwan pia wametoa michango mikubwa kwa njia mbalimbali. Hadi kufikia usiku wa kuamkia tarehe 8, michango iliyotolewa na wakazi wa Hong Kong inakaribia dola za Hong Kong milioni 700, kiasi hicho ni sawa na kila mkazi wa Hong Kong ametoa mchango wa dola za Hong Kong 100.

Katika kukabiliana na maafa makubwa yaliyotokea katika bahari ya Hindi, harakati ya wachina kutoa misaada kwa watu wa nchi zilizoathirika katika maafa hayo imeanza na itaendelea. Hivi sasa, simu za chama cha msalaba mwekundu cha China, shirikisho kuu la utoaji misaada la China na za mashirika mengine yanayopokea misaada zinalia siku nzima. Serikali ya China na watu wake wameonesha kwa vitendo halisi kuwa, China inapenda kutekeleza jukumu lake ipasavyo katika kuleta ustawi na maendeleo ya duniani.

Idhaa ya kiswahili 2005-01-13