|
Leo zikiwa zimebaki siku 17 kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa Iraq kufanyika tarehe 30 mwezi huu, mashambulizi ya kimabavu, mauaji ya kisiri na matukio ya utekaji nyara nchini humo bado yanaongezeka. Habari kutoka gazeti la Al-Ahram la Misri jana zilisema kuwa, kutokana na hali mbaya ya usalama nchini Iraq, waziri wa mambo ya nje wa serikali ya mpito ya nchi hiyo Bw. Hoshyar Zebari alisema kuwa, "uchaguzi huo hautakamilika wala hautafanyika bila tatizo lolote". Kabla ya hapo, waziri mkuu wa serikali ya mpito ya Iraq Bw. Iyad Allawi pia alikiri kuwa, hali ya usalama ya hivi sasa kwenye sehemu kadhaa nchini humo haitaweza kuhakikisha usalama wa wananchi wakati wa kupiga kura.
Bw. Zebari alisema kuwa, mikoa 14 kati ya mikoa yote 18 ya Iraq itaweza kufanya upigaji kura bila tatizo, lakini bado kuna tatizo katika mikoa 4 mingine. Pamoja na hali hiyo, Bw. Zebari pia anaona kuwa uchaguzi huo hautaahirishwa.
Serikali ya Marekani na serikali ya mpito ya Iraq zinaendelea kushikilia kufanya uchaguzi mkuu kama ilivyopangwa. Serikali ya Marekani inachukua tukio hilo kama ni alama ya mafanikio ya sera ya Marekani kwa Iraq, na Serikali ya Allawi inachukua tukio hilo kama upimaji wa heshima yake na uwezo wake wa kutawala, na kujitahidi kuathri matokeo ya uchaguzi huo kwa hadhi yake na kubadilisha serikali ya mpito kuwa serikali halali itakayochaguliwa na raia. Ili kuhakikisha uchaguzi huo unafanyika kama ilivyopangwa, Marekani iliongeza jeshi nchini humo na idadi ya askari wa Marekani nchini humo imefikia laki 1.5, ambayo ni kubwa kabisa baada ya vita vya Iraq. Licha ya hayo, Marekani pia iliongeza nguvu ya kupambana na makundi ya wanamgambo wanaoipinga Marekani nchini humo. Serikali ya mpito ya Iraq ilitangaza kuongeza muda wa hali ya hatari ya nchi na kuchukua hatua za kuongeza jeshi na polisi na kufunga mpaka wa Iraq na Syria, ili kuboresha hali ya usalama nchini humo. Aidha, serikali ya mpito ya Iraq pia iliwasiliana na wa-Suni wanaoupinga uchaguzi mkuu kupitia njia mbalimbali, na kujaribu kuwashawishi kubadilisha msimamo wao.
Lakini juhudi za serikali ya Marekani na serikali ya mpito ya Iraq hazikupata mafanikio. Idadi ya vifo na majeruhi ya askari wa Marekani na polisi wa Iraq inaongezeka kwa kiasi kikubwa, na maofisa wengi wa vyeo vya juu na watumishi wa uchaguzi huo wanauawa. Makundi mengi ya kijeshi nchini humo yamekuwa yakitoa tishio la kuwaua wajumbe wa tume ya uchaguzi katika ngazi mbalimbali na kuonya kuwa, wapigaji kura watakuwa shabaha za wauaji maalum wanaotumia bunduki kama watashiriki kwenye uchaguzi. Kutokana na hali hiyo, watumishi wengi wameamua kujiuzulu. Watumishi wote wa tume ya uchaguzi ya mkoa wa al-Anbar walitangaza kujiuzulu tarehe 11, na watumishi waliobaki wanaweza tu kufanya kazi ya maandalizi ya uchaguzi huo kisirisiri. Kutokana na wasiwas wa kushambuliwa, vituo vingi vya upigaji kura bado havijaanzishwa.
Mbali na tishio la makundi ya wanamgambo wanaoipinga Marekani, upingaji wa wa-Suni pia unafanya watu wengi kuingiwa na wasiwasi kuhusu mustakbali wa uchaguzi huo. Wa-Suni wanachukua asilimia 20 ya idadi ya watu wote wa Iraq, kama hawatashiriki kwenye uchaguzi huo, kiwango cha uwakilishi na uaminifu cha uchaguzi huo kitapungua kwa kiasi kikubwa, hata kuweza kufarakanisha jamii ya Iraq. Baadhi ya vyama vya wa-Suni vinavyopinga uchaguzi mkuu vimeonya kuwa, kama uchaguzi huo utafanyika kwa lazima, hawatakubali matokeo ya uchaguzi huo wala uhalali wa bunge la umma litakalochaguliwa na katiba litakayoitunga.
Wachambuzi wanaona kuwa, kama uchaguzi mkuu wa Iraq ukifanyika kwa lazima, itakuwa ni vigumu kwa uchaguzi huo kuleta utulivu kwa Iraq na pia itakuwa ni vigumu kwa serikali ya Marekani kujiondoa kutoka kwenye usumbufu wa suala la Iraq.
Idhaa ya Kiswahili 2005-01-13
|