|
Rais Thabo Mbeki wa Afrika ya kusini tarehe 12 alimaliza usuluhishi wa kidiplomasia nchini Cote D'ivoire. Kutokana na kuwa wawakilishi wa jeshi la upinzani la zamani la chama cha New Forces kukataa kushiriki kwenye mkutano maalum wa serikali ya maafikiano ya kitaifa ya Cote D'ivoire uliopendekezwa na rais Mbeki, hivyo juhudi za usuluhishi wa Mbeki hazikupata maendeleo halisi na mchakato wa amani ya Cote D'ivoire.
Baada ya kushiriki kwenye mkutano wa kwanza wa wakuu wa Baraza la amani na usalama la Umoja wa Afrika uliofanyika nchini Gabon, Rais Mbeki alifika kwenye mji mkuu wa Cote D'ivoire tarehe 11. Madhumuni ya ziara yake ni kutathmini hali ya maendeleo ya utekelezaji wa "Makubaliano ya amani ya Marcoussis" wa pande mbalimbali, na kutaka kuzikusanya pande mbalimbali zikae pamoja kufanya mazungumzo, ili kutafuta kwa pamoja njia ya kutatua mgogoro. Kwa nyakati tofauti alikutana na rais Gbabo na waziri mkuu Seydou Diarra wa Cote D'ivoire, na kuhudhuria mkutano maalum ulioitishwa na serikali ya maafikiano ya kitaifa ya Cote D'ivoire, lakini wawakilishi wa jeshi la upinzani la zamani walikataa kuhudhuria mkutano huo kwa kisingizio kuwa usalama wao haukuhakikishwa.
Hii ni mara ya tatu kwa Mbeki kwenda Cote D'ivoire kufanya usuluhishi katika muda wa miezi miwili ya hivi karibuni. Mwezi Novemba mwaka jana, jeshi la serikali ya Cote D'ivoire na jeshi la upinzani la zamani yalifanya mapambano ya kijeshi na jeshi la Ufaransa nchini Cote D'ivoire, hivyo hali ya nchi hiyo ilizidi kuwa mbaya kwa haraka. Akikabidhiwa jukumu na Umoja wa Afrika na Umoja wa uchumi wa nchi za Afrika ya magharibi, rais Mbeki akiwa msuluhishi alifanya usuluhishi nchini Cote D'ivoire, na kufikia maoni ya pamoja na vikundi mbalimbali vya Cote D'ivoire kuhusu kazi ya kunyang'anya silaha kutoka kwa vikundi mbalimbali na kufanya mageuzi ya kisiasa yaliyowekwa kwenye utekelezaji wa makubaliano ya amani. Baadaye, bunge la taifa la Cote D'ivoire lilijadili na kupitisha "mswada wa marekebisho ya katiba" wa serikali kuhusu haki za raia na wagombea wa uchaguzi mkuu, lakini jeshi la upinzani la zamani la New Forces bado lilikataa kusalimisha silaha, na kukataa kujiunga tena na serikali ya maafikiano ya kitaifa, na mchakato wa amani ya Cote D'ivoire ukawa unakwama siku zote.
Wachambuzi wanaona kuwa, jeshi la upinzani la zamani la New Forces kukataa mwaliko wa Mbeki wa kuhudhuria mkutano maalum wa serikali ya maafikiano ya kitaifa ya Cote D'ivoire ni mbinu yake ya kulipiza kisasi kwa Baraza la amani na usalama la Umoja wa Afrika kupitisha azimio kuhusu suala la Cote D'ivoire hivi karibuni.
Katika azimio hilo la Baraza la amani na usalama la Umoja wa Afrika kwanza limeainisha kuwa linaunga mkono Cote D'ivoire kupiga kura za maoni ya raia na kuona kuwa upigaji kura za maoni ya raia ni mbinu ya kutatua mgogoro wa nchi hiyo kwa hivi sasa. Chama cha the New Forces kimelalamika kabisa juu ya hatua hiyo, na kuona kuwa kufanya hivyo kutaufanya mchakato wa amani ya Cote D'ivoire urudi nyuma vibaya.
Kifungu cha 35 cha katiba ya Cote D'ivoire siku zote ni sababu kubwa ya mgogoro wa kisiasa wa nchini humo. Kifungu hicho kiliwahi kutomruhusu kiongozi wa chama cha upinzani Bwana Alassane Ouattara aliyekuwa waziri mkuu wa nchi hiyo kuwa mgombea wa rais. Bunge la Cote D'ivoire hivi karibuni lilifanya marekebisho na kumwezesha Bw Ouattara kupata nafasi ya kuwa mgombea. Lakini chama cha the New Forces kina wasiwasi kuhusu hadhi yake, hivyo kinapinga kupiga kura za maoni ya raia ili kutekeleza mswada wa marekebisho ya bunge la nchi hiyo.
Habari zinasema kuwa, Umoja wa Afrika umeamua kutuma mjumbe maalum kwenda Cote D'ivoire kuendelea na usuluhishi.
Idhaa ya kiswahili 2005-01-13
|