Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-01-13 18:26:35    
Baraza la kwanza la kutafuta namna ya kuokoa nishati kwa ajili ya maendeleo ya viwanda lafanyika mjini Beijing

cri
"Nishati iliyookolewa" hivi sasa imekuwa "nishati ya aina ya tano" inayokubalika nchini China, licha ya nishati ya makaa ya mawe, nguvu ya umeme, mafuta na gesi asilia. Tarehe 27 mwezi uliopita, baraza la kwanza la kutafuta jibu la kuokoa nishati kwa ajili ya maendeleo ya viwanda nchini China lilifanyika katika ukumbi mkuu wa umma mjini Beijing. Lengo la baraza hilo ni kufanya uchambuzi wa uchumi wa China na kutafuta jibu la namna ya kutumia nishati kibusara na kuendeleza uchumi kwa kuokoa nishati nchini China.

Naibu mkuu wa Taasisi ya Nishati ya Kamati ya Maendeleo na Mageuzi ya China Bw. Dai Yande aliwaambia waandishi wa habari, akisema "Pamoja na maendeleo ya uchumi matumizi ya nishati pia ni makubwa nchini China". Mwaka 2003 ongezeko la uchumi wa China lilitumia asilimia 50 ya saruji, asilimia 34 ya chuma cha pua, asilimia 30 ya makaa ya mawe na asilimia 13 ya nguvu ya umeme duniani. Kwa hiyo kuokoa matumizi ya nishati katika ongezeko la uchumi na kuongeza tija ya matumizi ya nishati ni jambo la lazima. Ikiwa China itaendelea kwenye njia hiyo hiyo ya zamani, matumizi makubwa ya nishati hayawezi kukubalika, hivi sasa njia pekee ya kuendeleza uchumi ni kuwa na matumizi madogo ya nishati na tija kubwa ya kazi. Bw. Dai Yande alisema, viwanda vyenye matumizi makubwa ya nishati na vinavyoleta uchafuzi mkubwa wa mazingira, na kupata tija ndogo ya kazi na thamani ndogo ya bidhaa zinazozalishwa, hakika havina nguvu ya ushindani na mwishowe vitashindwa, na sasa njia hiyo ya kizamani ya kuendeleza uzalishaji wa viwanda kwa kutumia nishati nyingi imekwisha leta uchafuzi na uharibifu mkubwa wa mazingira, hali hiyo hailingani kabisa na lengo la maendeleo ya uchumi na jamii.

China ni nchi inayotumia nishati nyingi na maendeleo madogo ya uchumi. Ikilinganishwa na matumizi makubwa ya nishati, thamani iliyozalishwa kwa kila kilo ya makaa ya mawe ni dola ya Kimarekani 0.36 tu, wakati hapa duniani kila kilo ya makaa ya mawe inazalisha thamani ya dola ya Kimarekani 1.86 kwa wastani. China bado haijabadilisha njia ya kizamani ya matumizi mabaya ya nishati, uchafuzi unaosababishwa na matumizi ya nishati na kutumia gharama kubwa ya kuondoa uchafuzi.

Imefahamika kuwa Baraza hilo la Kwanza la Kutafuta namna ya Kuokoa Nishati kwa ajili ya Maendeleo ya Viwanda lilifanywa na Shirikisho la Kuokoa Nishati la China na Shirikisho la Uchumi wa Viwanda la China kwa lengo la tija kubwa ya matumizi ya nishati, maendeleo ya uchumi na mustakbali wa nishati nchini China, mambo yanayozungumzwa katika baraza hilo yanahusu sera za kubana matumizi ya nishati, usalama wa nishati, kuanzisha mfumo mpya wa kuokoa nishati na teknolojia mpya ya kuokoa nishati na kueneza teknolojia mpya, na kutoa nyanja ya kupashana habari kuhusu teknolojia mpya na mahitaji ya zana za kuokoa nishati. Imefahamika kuwa kwenye baraza hilo kulikuwa na mijadala sita na mkutano wa wajumbe wote.

Idhaa ya kiswahili 2005-01-11