Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-01-14 14:19:43    
Tume ya uchaguzi mkuu wa Jamhuri Huru ya Abukhaziya ya Georgia yatangaza matokeo

cri
Tume ya uchaguzi mkuu wa Jamhuri huru ya Abkhaziya jana ilitangaza kuwa Bw. Sergei Bagapsch ameshinda kabisa katika uchaguzi uliofanyika juzi. Vyombo vya habari vinaona kuwa matokeo hayo yataathiri hali ya siasa ya kanda hiyo.

Abukhaziya iko katika sehemu ya kaskazini ya Georgia karibu na Bahari Nyeusi na inapakana na Russia kwa upande wa kusini, ni kituo muhimu cha viwanda na sehemu ya utalii katika nchi ya Georgia. Abkhaziya ilijitangazia uhuru wake mwaka 1992, kisha migogoro ikatokea kati yake na serikali kuu ya Georgia. Mwaka 1993 pande mbili zilikubaliana kusimamisha vita na kuanza mazungumzo ya amani kuhusu tatizo hilo la Abkhaziya, lakini mazungumzo yalikuwa magumu na tatizo hilo halijatatuliwa hadi sasa. Ingawa Abkhaziya ilijitangazia kuwa jamhuri huru, lakini haijatambuliwa na nchi yoyote duniani, na uhusiano wake na Russia ni wa karibu.

Uchaguzi mkuu wa Abukhaziya uliwahi kufanyika Oktoba 3 mwaka jana, lakini kwa sababu kura za wagomgea wawili wa urais zililingana, hali ya wasiwasi ilizuka nchini. Kutokana na mazungumzo, mwishowe mkataba wa maelewano ya kikabila ulipatikana Desemba 12 mwaka jana, na kuweka msingi wa uchaguzi huo kufanyika tena.

Baada ya Sergei Bagapsch kutangazwa kuwa rais wa jamhuri hiyo, mara rais wa Georgia alipinga uhalali wa matokeo ya uchaguzi huo na kusisitiza kuwa atarudisha mamlaka kwa Abukhaziya. Waziri wa mambo ya nje wa Russia alisema kuwa Russia itahimiza pande mbili kurudisha mazungumzo mapema iwezekanavyo na kutumai kuwa hali ya kisiasa ya Abukhaziya itakuwa ya utulivu. Wachambuzi wanaona kuwa kutokana na misimamo ya pande mbili kutobadilika, ni vigumu kubashiri kuwa mazungumzo ya pande mbili yatafanyika lini na yatakuwa na matokeo gani.

Wachambuzi wanasema, kutokana na mchanganyiko wa matatizo ya kikabila na ya kimataifa, migogoro kati ya Abukhaziya na Georgia ni ya utatanishi. Tokea Georgia ipate uhuru, migongano ya kikabila imekuwa mikali. Kwa upande mmoja Abkhaziya ni sehemu muhimu kwa Georgia katika mambo ya siasa na uchumi, kwa hiyo Georgia itang'ang'nia mamlaka yake kwa Abukhaziya. Kwa upande mwingine, Abukhaziya imejitenga na utawala wa serikali ya Georgia hata zaidi ya miaka kumi, serikali mpya ya Abkhaziya haiwezi kuacha siasa yake ya kuikaribia Russia na kuipinga Georgia. Bw. Sergei Bagapsch alipohojiwa na waandishi wa habari wa "Sauti ya Russia" alisema kuwa viongozi wapya wa Abukhaziya watafanya mazungumzo ya kisiasa na Georgia kwa usawa, urafiki na wakiwa na mamlaka, huku alisisitiza kuwa mazungumzo hayo ni baina ya nchi na nchi, na alionya kuwa Georgia isijaribu kutatua tatizo kwa nguvu za kijeshi. Alipogusia uhusiano kati nchi yake na Russia alisisitiza kuwa ushirikiano wa kiuchumi unapaswa kuwekwa kimkataba. Mazingira ya kisiasa nje ya Abukhaziya yanaonesha kuwa nchi za Russia, Georgia na nchi za Ulaya na Marekani pia zinaathiri hali ya kisiasa humu nchini Abukhaziya.

Tokea mwezi Januari mwaka jana rais Mikhail Saakashvili aliposhika hatamu ya serikali nchini Georgia, amekuwa akishughulika na kurudisha mamlaka na muungano wa taifa. Katika majira ya joto mwaka jana, jeshi la Georgia liliwahi kufunga kabisa bandari ya Abukhaziya, na iliwahi kutokea tukio la jeshi la Georgia kuifyatulia risasi meli ya mizigo ya Uturuki na meli ya watalii ya Russia wakati meli hizo zilipoondoka bandari ya Abukhaziya, tukio ambalo lilileta hali ya wasiwasi kati ya Georgia na Russia.

Vyombo vya habari vinaona kuwa kutokana na matokeo ya uchaguzi huo wa Abukhaziya, nia ya Georgia kurudisha mamlaka kwa Abukhaziya itakuwa imara zaidi, na Abukhaziya itazidi kugongana nayo ili kulinda serikali yake. Safari ya kutatua tatizo kati ya Abukhaziya na Georgia itakuwa ndefu na ngumu.

Idhaa ya kiswahili 2005-01-14