Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-01-18 15:53:21    
Barua 0118

cri
Msikilizaji wetu Gulam Haji Karim wa sanduku la posta 97 Zanzibar Tanzania ametuletea barua na kadi ya kututakia heri katika ya sikukuu ya Krismas na mwaka mpya akisema kuwa, ameamua kutumia fursa hii pia, kutuoa salamu za heri ya mwaka mpya wa 2005 kwa wananchi wa China pamoja na wasikilizaji na watangazaji wa idhaa ya kiswahili ya Radio China kimataifa. Anasema tuombe kwa pamoja mwaka 2005 uwe mwaka wa salama na amani duniani kote, na uwe mwaka wa furaha na baraka.

Pia anatoa shukrani zake za dhati kwa Radio China Kimataifa kwa kumtumia gazeti la China Today la mwezi Novemba mwaka 2004. Anasema kwenye gazeti hilo amepata kujua mengi ukiwemo ushindi wa medali 32 za dhahabu zilizopatikana katika michezo ya Olimpiki huko Athens, Ugiriki na maendeleo ya maandalizi makubwa ya michezo ya Olimpiki ya mwaka 2008 itakayofanyika Beijing, China.

Na katika barua yake nyingine msikilizaji wetu huyo Gulam Haji Karim, ametoa pongezi za maadhimisho ya miaka mitano tangu Macau kurudi nchini China. Anasema kuwa, kwa kutimiza miaka mitano kwa mtoto mtoro, yaani Macau, kurudi nyumbani kwao, na mzee wake yaani Jamhuri ya watu wa China kumpokea mtoto huyo na kumlea vizuri na kumtunza, miaka mitano si mingi kwa mtoto kukua. Lakini katika kipindi hicho mtoto Macau chini ya uongozi wa mzee wake Jamhuri ya watu wa China amekuwa na maendeleo mazuri. Anawapongeza mzee na mtoto wake kwa kuelewana, kushirikiana katika kujijengea maendeleo yao pamoja kwa jumla na wananchi wake.

Msikilizaji wetu Abdillahi Shaaban wa sanduku la posta 1304 Kakamega Kenya ametuletea barua akianza kwa salamu. Pia anasema angependa kushukuru sana mungu kwa kutuwezesha kufahamiana kwa barua na anaomba urafiki kati yake na Radio China kimataifa udumu, na kutushukuru kwa kumtumia kadi ya ujulisho wa mpango wa tovuti ya idhaa ya kiswahili ya Radio China kimataifa.

Bwana Shaaban mbali na shukrani hizo ana swali, anasema angependa kufahamu ni kwa nini siku hizi tunatumia kalenda ndogo sana, ambayo hata ikiwekwa ukuta huwezi kuona tarehe ukiwa mbali. Anasema tafadhari anaomba Kalenda ya mwaka 2005 iwe Kalenda kubwa kama zile ambazo tulikuwa tukituma katika miaka ya nyuma. Pia anasema kama kuna uwezekano angeomba apatiwea kofia, fulana na kalamu zenye alama ya CRI. Pia ametoa mapendekezo akisema angeomba muda wa matangazo uongezwe, na pia anaomba tutume wajumbe waende Kenya kuongea na KBC kwamba kuna nchi kadhaa zimetuma maombi ya nafasi kwa KBC, yeye anapenda sisi tukubaliwe kabla ya hapo.

Tunamshukuru sana msikilizaji huyo Bwana Abdillahi Shaban kwa barua yake ya dhati, tumetiwa moyo sana kwa maneno yake ya dhati ya kutumai Radio China kimataifa ipate nafasi ya kuongeza muda wake kwenye Kampuni ya KBC. Tunapenda kumwambia Bwana Shaaban na wasikilizaji wetu wengine kuwa, maofisa wetu wanaohusika wanafanya juhudi za kupata nafasi ya kuongeza muda wa idhaa yetu ya kiswahili katika Kampuni ya KBC, labda muda si mrefu baadaye tutafanikiwa.

Na kuhusu kalenda kuwa ndogo kama alivyosema, tunapenda kuwaambia wasikilizaji wetu kuwa, kutokana na matatizo ya kutuma vifurushi, Radio China kimataifa kwa sasa inapendelea kutengeneza kalenda ndogo kama hiyo ikiwa kama kadi ya kutakia heri ya mwaka mpya kwa wasikilizaji. Tunaomba wasikilizaji wetu mtuelewe kwa hilo, hili siyo suala ambalo idhaa ya kiswahili inaweza kulishughulikia, wahusika ni uongozi wa juu wa Radio China kimataifa.

Kadhalika, zawadi ndogo kama kofia, fulana na kalamu, kwa kawaida, kila yakifanyika mashindano ya chemsha bongo au uandikaji wa makala maalum, wasikilizaji kadha wa kadha wataweza kupata zawadi ndogondogo kama hizo, lakini kama uwezekano upo hatuwezi kusita kuwafurahisha wasikilizaji wetu, lakini mapendekezo yenu yote huwa tutayafikisha kwenye idara husika.

Idhaa ya kiswahili 2005-01-18