|
Japokuwa zimebaki wiki mbili tu kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu nchini Iraq, lakini hali ya usalama ya nchi hiyo bado haina dalili yoyote ya kuboreshwa. Mapambano makali kati ya Marekani na serikali ya muda ya Iraq na vikundi vya wanamgambo vya Iraq yanaendelea kupamba moto. Tarehe 17, matukio ya kimabavu yaliyotokea nchini Iraq yalisababisha vifo vya watu kumi kadhaa. Iraq iliyochoshwa na vurugu za kivita ilipita siku nyingine ya kumwaga damu.
Jeshi la Marekani nchini Iraq jana lilitangaza kuwa, katika saa 24 zilizopita, katika operesheni yake ya kijeshi dhidi ya Mosul, mji mkubwa kabisa katika sehemu ya kaskazini ya Iraq, jeshi la Marekani liliwaua wanamgambo wasiopungua 7 na kuwakamata wengine 12. Hivi sasa jeshi la Marekani na jeshi la usalama la Iraq yanakusanya wanajeshi zaidi ya 12,000 katika mji wa Mosul na sehemu zilizo karibu ili kulinda uchaguzi mkuu ufanyike kwa wakati. Mkoa wa Nineveh ni mmoja ya mikoa minne yenye hali mbaya sana ya usalama nchini Iraq, wajumbe wa tume ya uchaguzi mkuu wa mkoa huo walijiuzulu kwa pamoja kutokana na tishio la wanamgambo wanaoipinga Marekani, na kazi ya uandikishaji wa wapiga kura bado haijaanza katika mkoa huo. Katika sehemu karibu na Fallujah, ambayo ni makao makuu ya wanamgambo wanaoipinga Marekani wa waislamu wa madhehebu ya suni, jeshi la usalama la Iraq lilifanya msako mkubwa katika siku mbili zilizopita na kuwaua wanamgambo wasiopungua 35, na kuwakamata wengine 64, na katika operesheni nyingine ya kijeshi pia liliwakamata wanamgambo 60 wanaoipinga Marekani.
Lakini mashambulizi ya wanamgambo wanaoipinga Marekani hayakusimamishwa hata siku moja. Tarehe 17, katika miji ya Baquba, Baiji, Baghdad, Ramadi na Fallujah, wanamgambo walifanya mashambulizi dhidi ya jeshi la Marekani nchini Iraq na jeshi la ulinzi na askari polisi wa Iraq. Mbali na hayo shule zilizowekwa vituo vya kupigia kura katika miji kadhaa pia zilishambuliwa, na wafanyakazi wanaoshiriki kwenye kazi ya uchaguzi mkuu wanaendelea kutishiwa.
Ili kukabiliana na hali mbaya ya usalama nchini Iraq, amiri jeshi wa jeshi la Marekani nchini Iraq Jenerali George W. Casey jana alipaswa kukiri kuwa, mashambulizi ya kisilaha hayawezi kuzuiliwa wakati wa uchaguzi mkuu. Naibu waziri mkuu wa serikali ya muda ya Iraq anayeshughulikia mambo ya usalama Bwana Barham Saleh jana hiyo pia alisema kuwa, serikali yake iko tayari kukabiliana na changamoto kubwa ya usalama, lakini kwa vyovyote uchaguzi mkuu utafanyika kwa wakati. Alisema kuwa, uchaguzi wenye dosari ni bora kuliko kutofanya kabisa uchaguzi, serikali inayochaguliwa na raia itakuwa nzuri zaidi kuliko serikali iliyoteuliwa na Marekani.
Wachambuzi wanaona kuwa, japokuwa kuna vikwazo vya usalama na upinzani mkali wa madhehebu ya suni, lakini uchaguzi mkuu utafanyika kama ulivyopangwa. Kwa upande mmoja kufanya uchaguzi mkuu nchini Iraq kwa wakati ni ishara ya kama serikali ya Marekani na serikali ya muda ya Iraq zinaweza kudhibiti au la hali ya Iraq na kama sera yao ilivyo sasa ni sawa au la. Marekani inatumai kuficha makosa yake ya kuanzisha vita dhidi ya Iraq kwa kufanya uchaguzi huo, na kujaribu kujinasua katika hali yenye matatizo makubwa nchini Iraq baada ya uchaguzi mkuu. Kwa upande mwingine, idadi kubwa ya watu wa Iraq wanatumai kuwa, uchaguzi huo utafanyika kwa mafanikio. Hivyo kama serikali ya muda ya Iraq ikiahirisha uchaguzi mkuu huo, itapingwa na watu wengi zaidi. zaidi ya hayo, nchi nyingi duniani pia zinatumai kuwa uchaguzi mkuu wa Iraq utafanyika kwa wakati na kwa mafanikio, ili watu wa Iraq waweze kuchagua serikali yenye uwakilishi na heshima, na kutimiza lengo la watu wa Iraq kuiendesha Iraq.
Idhaa ya kiswahili 2005-01-18
|