Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-01-21 14:34:49    
Mtoto wa Mandela afariki dunia kutokana na Ukimwi

cri
Tarehe 6 Januari mwaka huu, rais wa zamani wa Afrika ya kusini Bwana Nelson Mandela mwenye umri wa miaka 86 mwaka huu alitangaza kwa vyombo vya habari kuwa, mtoto wake wa kiume mwenye umri wa miaka 54 Bwana Makgatho Mandela siku hiyo alifariki dunia kutokana na ugonjwa wa Ukimwi.

Bwana Mandela aliongeza kuwa, licha ya mtoto wake wa kiume, katika ukoo wake huko mkoa wa East Cape, bado kuna jamaa watatu wengine ambao walifariki dunia kutokana na kuambukizwa Ukimwi. Alisema kuwa, lengo lake la kufanya hivyo ni kutaka kuongeza uwazi kuhusu suala la ukimwi. Alisema kama watu hawatakabiliana na hali halisi ya kimaisha, na wataficha ukweli kuhusu Ukimwi, basi binadamu hawezi kuufanya Ukimwi kama ugonjwa wa kawaida.

Habari hiyo ilifuatiliwa sana na vyombo vya habari na jamii nchini Afrika ya kusini na nchi nyingine za Afrika. Mjukuu wa Mandela katika mazishi ya baba yake yaliyofanyika tarehe 15 na kuwashirikisha elfu kadhaa ya watu alikiri kuwa, mama yake Bibi Zondi aliyefariki dunia mwaka mmoja uliotangulia pia alikufa kwa Ukimwi.

Bwana Mandela alieleza matumaini yake kuwa, binadamu wote watakuja kufahamu umuhimu wa kujadili hadharani suala la ukimwi, ili kuufanya ukimwi kama ugonjwa wa kawaida. Akidai kuwa, watu wangewasaidia ndugu zao walioambukizwa na ukimwi ili kuwasaidia wawe na matumaini ya kuishi duniani na kupambana na ugonjwa huo. Aliwataka watu wote wasiwe na unyenyepa kwa watu walioambukizwa Ukimwi.

Nchini Afrika ya kusini, ugonjwa wa ukimwi ni kama ugonjwa wa tauni unavyotisha watu, baadhi ya viongozi wa ngazi za juu hukataa kutangaza idadi kubwa ya watu waliokufa kutokana na Ukimwi nchini humo, na watu wengi wanakataa kuzungumzia suala hilo hadharani, lakini Bwana Mandela alitangaza kifo cha mtoto wake, akitumai kuwa kitendo chake kitaweza kuisaidia Afrika ya kusini kukabiliana na hali halisi ya kuwa na kiasi kikubwa cha watu walioambukizwa Ukimwi.

Baada ya Bw. Mandela kutangaza kifo cha mtoto wake, magazeti ya Afrika ya kusini, wanaharakati wa kukinga na kutibu ukimwi pamoja na viongozi wa vyama mbalimbali nchini humo kwa nyakati tofauti walionesha heshima kubwa kwa Mandela, wakimsifu kwa moyo wake wa kuvunja mwiko na kutangaza kwa vyombo vya habari kuwa, mtoto wake alifariki dunia kutokana na ukimwi. Vyombo vya habari vimesema kuwa, kitendo cha Mandela kimepambana na mwiko wa jamii na kinastahili kusifiwa. Kwa sababu hivi sasa tatizo kubwa kabisa linaloikabili kazi ya nchi hiyo ya kupambana na ukimwi ni unyenyepa na kujaribu kuficha ukweli kuhusu kuwa na Ukimwi.

Kama nchi nyingine, watu mashuhuri wa Afrika ya kusini hawataki kutangaza wazi kuwa yeye au jamaa zao wameambukizwa Ukimwi. Bwana Mandela amekuwa mmoja wa viongozi wachache wa Afrika ya kusini aliyethubutu kutangaza wazi kuwa jamaa zake waliambukizwa Ukimwi. Kiongozi wa kabila la wazulu ambaye pia ni mwenyekiti wa chama cha uhuru cha Inkatha cha Afrika ya kusini Bwana Mangosuthu Buthelezi alisema kuwa anamsifu Bw. Mandela kwa uamuzi wake wa kutangaza kifo cha mtoto wake akiongeza kuwa, ujasiri na moyo huo ni ishara ya yeye kuwa ni kiongozi mashuhuri. Alieleza imani yake kuwa, kitendo cha Mandela kitatoa mchango mkubwa katika kusaidia kuvunja kimya cha watu kwa suala la ukimwi na kuondoa unyenyepa dhidi ya watu walioambukizwa Ukimwi.

Idhaa ya kiswahili 2005-01-18