Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-01-18 20:48:10    
Mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu kupunguza maafa duniani wafanyika mjini Kobe, Japan

cri

    Mkutano wa wa Umoja wa Mataifa kuhusu kupunguza maafa duniani umefunguliwa leo mjini Kobe, Japan. Hii ni mara ya pili kwa mkutano wa aina hiyo kufanyika katika miaka kumi iliyopita. Wataalamu na wawakilishi kutoka nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa, idara zinazohusika za Umoja wa Mataifa na mashirika mengine watakumbusha uwezo wa binadamu wa kukabiliana na maafa mbalimbali katika miaka 10 iliyopita, na kubuni mkakati mpya wa kimataifa wa kupunguza na kukinga maafa.

    Kufuatana na maendeleo ya jamii, mazingira ya maisha na kazi ya binadamu vinaboreshwa siku baada ya siku. Lakini wakati huo huo, hasara zinazoletwa na maafa za kimaumbile pia zimekuwa kubwa zaidi. Kutokana na sababu hiyo, mwaka 2000 Umoja wa Mataifa ulianzisha mkakati wa kupunguza maafa duniani, kufanya tathmini kuhusu hali ya maafa na kutunga mpango wa kukinga maafa duniani kila baada ya miaka 10.

    Mkutano huo wa kupunguza maafa umefunguliwa baada ya tetemeko la ardhi na dhoruba kubwa lililosababishwa nalo kutokea katika Bahari ya Hindi. Hivyo kuanzisha mfumo wa tahadhari ya dhoruba katika Bahari ya Hindi kumekuwa ajenda muhimu ya mkutano huo. Baada ya dhoruba lililosababishwa na tetemeko la ardhi kutokea katika Bahari ya Hindi, Umoja wa Mataifa uliweka suala hilo katika mkakati wa uokoaji wa maafa. Na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni wa Umoja wa Mataifa pamoja na idara ya hali ya hewa ya Japan, pia watafanya mkutano maalumu katika kipindi cha mkutano huo, ili kuwashirikisha wataalamu wa pande husika, mashirika ya kimataifa na nchi zinazotoa misaada kusukuma mbele mfumo wa tahadhari ya dhoruba baharini na kujaribu kupata uungaji mkono wa mkutano wa kupunguza maafa.

    Ofisa wa Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa, hatua ya mwanzo ya ujenzi wa mfumo wa tahadhari ya maafa katika Bahari ya Hindi unahitaji dola za kimarekani milioni 30. Na licha ya hayo, dola za kimarekani milioni 1 hadi 2 zinahitajika kila mwaka ili kutunza vifaa vya mfumo huo. Anatumai kuwa misaada ya jumuiya ya kimataifa itakidhi mahitaji hayo.

    Hivi sasa mfumo pekee wa tahadhari ya maafa duniani uko katika Bahari ya Pasifiki. Ulianzishwa na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni wa Umoja wa Mataifa mwaka 1968. Hakuna mfumo wa tahadhari ya maafa hayo katika Bahari ya Hindi kwa sababu maafa hayo hayakutokea mara kwa mara kama Bahari ya Pasifiki, hakuna rekodi ya maafa hayo katika sehemu hiyo katika miaka mamia kadhaa iliyopita. Lakini maafa yaliyosababisha vifo vya watu laki 1.7 yamewafanya watu wengi kutambua kuwa mfumo wa tahadhari ya maafa katika Bahari ya Hindi unahitaji kujengwa. Mkurugenzi mtendaji wa Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni wa Umoja wa Mataifa Bw. Chiro Matsuura amesema kuwa, kikundi cha tahadhari ya maafa ya Bahari ya Pasifiki kina maarifa ya miaka zaidi ya 30, na kinaweza kutoa uungaji mkono wa kiteknolojia kwa ujenzi na kazi ya mfumo wa tahadhari ya maafa katika Bahari ya Hindi. Lakini bado kuna maoni tofauti kuhusu kama mfumo wa tahadhari utafanya kazi vizuri. Baadhi ya watu wanaona kuwa, ni rahisi kwa mfumo huo kutoa tahadhari isiyo sahihi, na kusababisha watu waondoke kwenye makazi yao bila ya maafa yoyote na kuleta hasara kubwa ya kiuchumi.

    Habari zinasema kuwa, mkutano wa kupunguza maafa utajenga utaratibu wa kusawazisha pande husika wa mfumo wa tahadhari ya maafa ya Bahari ya Hindi kwa kuharakisha maendeleo ya kazi mbalimbali na kuboresha matumizi ya fedha, ili kujaribu kujenga mfumo huo katika Bahari ya Hindi kabla ya mwezi Juni mwakani na kujenga mfumo wa tahadhari ya dhoruba linalosababishwa na tetemeko la ardhi duniani kabla ya mwezi Juni mwaka 2007.

Idhaa ya Kiswahili 2005-01-18