Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-01-19 21:05:43    
Yushchenko ataapishwa kuwa Rais wa Ukraine

cri

    Mahakama kuu ya Ukraine jana ilitoa amri kufuta hukumu iliyotolewa na mahakama hiyo tarehe 11 kuhusu kupiga marufuku kutangaza matokeo ya uchaguzi mkuu wa Ukraine. Hukumu hiyo imetandika njia kwa rais mteule Bw.Viktor Yushchenko kushika madaraka rasmi.

    Mahakama kuu ya Ukraine ilitoa hukumu hiyo baada ya kupitia ombi la mwakilishi wa Bw. Yushchenko kuhusu kufuta upigaji marufuku dhidi ya kutangaza matokeo ya uchaguzi mkuu wa Ukraine. Rais mteule wa Ukraine Bw. Yushchenko aliviambia vyombo vya habari kuwa bunge la Ukraine na gazeti la serikali ya Ukraine tarehe 20 zitatangaza matokeo ya duru jipya la pili la upigaji kura la uchaguzi mkuu wa nchi hiyo. Baada ya hapo, mtu atakayeshinda kwa mujibu wa matokeo hayo anaweza kufanya sherehe ya kuapisha. Hivyo Bw. Yushchenko aliyeshinda katika duru jipya la pili la upigaji kura atashika rasmi wadhifa wa urais.

    Tarehe 31 mwezi Oktoba mwaka jana, duru la kwanza la upigaji kura la uchaguzi mkuu wa Ukraine lilifanyika, na huo ulikuwa ni uchaguzi wa nne tokea Ukraine ipate uhuru mwaka 1991. Lakini hakuna mgombea yeyote aliyepata zaidi ya asilimia 50 ya kura, hivyo waziri mkuu wa Ukraine Bw. Viktor Yanukovych aliyepata kura nyingi zaidi na mgombea wa kundi la upinzani Bw. Yushchenko walitakiwa kugombea urais katika duru la pili la upigaji kura.

    Tarehe 21 mwezi Novemba, duru la pili la upigaji kura lilifanyika nchini Ukraine. Baadaye tume ya uchaguzi ya Ukraine ilitangaza kuwa Bw. Yanukovych alishinda, lakini Bw. Yushchenko alipinga matokeo hayo na kudai kuwa kulikuwa na udanganyifu katika uchaguzi mkuu. Waungaji mkono wa pande mbili walikuwa wakifanya maandamano na mikusanyiko mikubwa, na kusababisha msukosuko wa kisiasa nchini humo. Baadaye Mahakama kuu ya Ukraine ilitoa hukumu kuwa matokeo ya upigaji kura wa tarehe 21 mwezi Novemba hayakufanya kazi, na kuthibitisha kufanya upya duru la pili la upigaji kura tarehe 26 mwezi Desemba.

    Tarehe 10 mwezi huu tume ya uchaguzi ilitangaza rasmi matokeo ya duru la pili la upigaji kura, yaani Bw. Yushchenko ameshinda. Lakini Bw. Yanukovych na waungaji mkono wake walitoa mashaka dhidi ya matokeo hayo, na kuiomba mahakama kuu kupiga marufuku kutangazwa kwa matokeo hayo. Tarehe 11, mahakama kuu ilitoa hukumu ya kupiga marufuku kutangazwa kwa matokeo hayo. Tarehe 14 makao makuu ya ugombeaji wa Bw. Yanukovych yaliishitaki tume ya uchaguzi, na kuiomba mahakama kuu ifute matokeo ya duru jipya la upigaji kura.

    Hata hivyo, maoni ya raia yanaona kuwa, kutakuwa na uwezekano mdogo kwa mahakama kuu kutoa hukumu itakayomsaidia Bw. Yanukovych.

    Wachambuzi wanasema kuwa, uchaguzi huo uliokuwa na matatizo mengi umeonesha mvutano mkali kuhusu Ukraine kati ya upande wa Marekani na nchi za magharibi na upande wa Russia na nchi nyingine za Umoja wa Jamhuri huru, na kuonesha ufarakanishaji wa kisiasa nchini Ukraine. Watu wanatumai kuwa pande mbili za Ukraine zitayapa kipaumbele mambo makuu ya taifa, kuondoa tofauti kati yao na kuifanya Ukraine iendelee kwa utulivu.

Idhaa ya Kiswahili 2005-1-19