Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-01-20 10:57:24    
Askari wa kulinda amani Bw. Li Tanshi na familia yake

cri
Tokea mwaka 1992 China ilipopeleka kikosi cha kwanza cha wanajeshi wa kulinda amani nchini Cambodia, wanajeshi 2800 na askari polisi 300 wa China wameshiriki katika harakati za kulinda amani za Umoja wa Mataifa. Mwaka jana, kikosi kingine cha kulinda amani cha China chenye watu 550 kilipelekwa nchini Liberia, Afrika ya magharibi. Bwana Li Tanshi aliyefanya kazi katika hospitali kuu ya jeshi la ukombozi wa umma la China mjini Beijing ni mmoja ya watu waliokuwepo kwenye kikundi hicho.

Mke wa Bwana Li Tanshi anaitwa Qu Lin, yeye pia anafanya kazi katika hospitali. Mwaka jana, jambo la kwanza alilofanya kila siku baada ya kurudi nyumbani ni kufungua kompyuta na kuangalia kama mume wake amemwandikia barua pepe au la. Alisema:

"Mara ya mwisho aliponiandikia barua pepe aliniambia kuwa atakwenda nje kutekeleza jukumu, na huenda ikamchukua siku 6 au 8, lakini sasa siku kumi zimeshapita, na bado sijapata habari yoyote kutoka kwake. Nimeanza kuwa na wasiwasi."

Kutokana na vurugu za kivita zilizodumu kwa miaka mingi, mawasiliano ya Liberia ni ya duni, hivyo Bwana Li huwasiliana na mke wake kupitia mtandao wa internet. Bibi Qu Lin alisema kuwa, hii ni mara yake ya kwanza kukaa mbali na mume wake kwa muda mrefu namna hii. Tangu mume wake aondoke China, moyo wake haukuweza kutulia hata siku moja.

Mtoto wao wa kiume Li Hechen ni mwanafunzi wa kidato cha pili katika sekondari moja ya Beijing. Yeye ni mwanafunzi hodari sana katika masomo yake, kila mwaka huwa na matokeo mazuri.

Sikukuu ya mwaka mpya wa kijadi inapokaribia, mwandishi wetu wa habari alijaribu kumpigia simu Bwana Li Tanshi kwa siku mbili mfululizo, hatimaye simu yake ya kupitia satilaiti ilipatikana, daktari Li alisema kuwa wanaishi na kuendelea na kazi vizuri.

"Baada ya kuchapa kazi kwa nusu mwaka, hivi sasa hali ya maisha ya kikosi cha kulinda amani cha China nchini Liberia, ni nzuri kuliko vikosi vingine vinavyolinda amani huko, ambacho kina jenereta, hospitali, na vifaa vya maji. Jeshi la kulinda amani la China limegawanyika katika vikosi vitatu vya wahandisi, madaktari na wachukuzi, wakiwa wanafanya kazi kubwa nchini Liberia."

Mwaka jana ulikuwa mwaka wa kwanza kwa askari wa China kutekeleza jukumu la kulinda amani nchini Liberia, hivyo kila kitu kilipaswa kujengwa na wao wenyewe kama vile kambi na hospitali. Mwanzoni kutokana na kutokuwa na mawasiliano ya barabara, kila kitu kilipaswa kusafirishwa kwa ndege mbali na maji, umeme na gesi, kila siku walikula biskuti na wakati fulani hawakuweza kupata maji yaliyochemshwa.

Katika nusu ya kwanza ya mwaka jana, wanajeshi wa China licha ya kupambana na matatizo ya aina mbalimbali, pia walifanya juhudi kuisaidia Liberia kukarabati barabara zenye urefu wa kilomita 660 iliyoharibika vibaya, kujenga madaraja 21, viwanja vitatu vya helikopta, kuwasafirisha watu zaidi ya elfu 60 na vifaa tani elfu 10. Akiwa daktari, jambo linalomfurahisha Bwana Li Tanshi ni kuwa, madaktari wa China walikuwa wanatoa matibabu kwa makamanda na askari na wakazi 3000. Alikumbuka kuwa, mtoto mmoja mwenye umri wa miaka 9 aliyejeruhiwa vibaya kwa risasi, alipopelekwa hospitali usiku wa manane alikuwa mahututi, madaktari wa China walijitahidi kwa kadiri wawezavyo kuokoa maisha yake. Wakazi wanaoishi karibuni waliandika barua nyingi kwa Umoja wa Mataifa, kuwashukuru madaktari wa China. Kutokana na kazi zao nzuri, wanajeshi wote wa kulinda amani wa China nchini Liberia walitunukiwa nishani ya heshima na amani ya Umoja wa Mataifa.

Liberia ilikuwa nchi tajiri, pato la wastani kwa kila mtu liliwahi kufika dola za kimarekani 3000, lakini vita vilivyodumu kwa miaka zaidi ya kumi vimeharibu vibaya nchi hiyo. Akiona hasara kubwa na madhara makubwa yaliyosababishwa na vita nchini Liberia, Bwana Li Tanshi aliona kihalisi umuhimu wa kuwa na amani na utulivu kwa ustawi na maisha mazuri ya wananchi. Akisema:

" Hivi sasa Liberia ni nchi maskini sana, wananchi wa nchi hiyo hawana uhakikisho wowote wa kimaisha, matokeo ya vita ni mabaya sana. Kama nisingekuja Liberia, nisingeweza kuona ugumu wa nchi kubwa kama China wa kudumisha utulivu, maendeleo endelevu na kustawi namna hii."

Bwana Li Tanshi alisema kuwa, yeye hana wasiwasi wowote kuhusu maisha ya mke na familia yake kutokana na ustawi na utulivu wa China.

Muda wa mwaka mmoja unakaribia kumalizika, Bwana Li na wanajeshi wengine wote wanatarajia kurudi nchini China mapema iwezekanavyo, familia zao pia zinawasubiri kwa hamu kubwa. Mtoto wa Bwana Li Tanshi anategemea baba yake arudi mapema ili waweze kucheza pamoja mpira wa meza na mpira wa vinyoya. Bibi Qu Lin alisema kuwa, mume wake anapenda kula tambi za aina ya kibeijing, akirudi tu watakwenda pamoja kula tambi hizo katika mkahawa maarufu mjini Beijing.

Idhaa ya kiswahili 2005-01-20