|
Tarehe 20 mwezi huu rais George Bushi wa Marekani ataanza kipindi chake cha pili cha utawala wa Marekani. Serikali ya Bush haitaacha sera yake ya kutenda mambo kwa upande mmoja tu ili kuimarisha nafasi yake ya "ubabe" duniani, na nchi nyingi za Ulaya zinatetea "dunia iwe ya pande nyingi zinazoshirikiana na kuzuiana". Kwa hiyo katika kipindi cha miaka minne ijayo ya Bush jinsi uhusiano kati ya Marekani na Umoja wa Ulaya utakavyoendelea, ni suala la kuzingatiwa duniani.
"Matokeo ya vita dhidi ya Iraq" yataendelea kuathiri uhusiano kati ya Marekani na nchi za Ulaya. Mwaka 2003 vita dhidi ya Iraq vilivyoanzishwa na Marekani na Uingereza vilifanya uhusiano kati ya Ulaya na Marekani uwe katika hali mbaya, na baadaye katika muda wa mwaka mmoja hivi ingawa pande mbili zilijitahidi kuwasiliana ili kujaribu kuziba ufa uliotokea katika uhusiano, lakini hali ya kutoaminiana na kutengana haijabadilika. Baada ya jeshi la muungano kutoa madaraka kwa Iraq na baada ya serikali ya Iraq kuanzishwa, nchi wanachama wa NATO barani Ulaya zilikubali matakwa ya Marekani ya kupeleka maofisa kufundisha jeshi la usalama nchini Iraq. Lakini Ufaransa, Ujerumani, Ubilgiji, Ugiriki na Hispania zilitangaza wazi kuwa hazitatuma maofisa. Hii inamaanisha kuwa ufa uliosababishwa na vita vya Iraq unabaki pale pale. Nchi nyingi za Ulaya zinaona kuwa Marekani haina budi kubeba jukumu la hali mbaya ya usalama nchini Iraq. Hali ya Iraq haionekani kuelekea kuwa nzuri na Marekani itazama ndani ya matope bila kuweza kujitoa na mara kwa mara inaomba misaada kutoka nchi wanachama wa NATO, lakini "nchi wanachama wa zamani" wa NATO zinaendelea kushikilia msimamo wa kupinga kupeleka askari nchini Iraq, na "nchi wanachama wapya" Poland, Hungary zinataka kuondoa askari wao kutoka Iraq baada ya kuisaidia Marekani kwa mwaka moja.
Pili, Marekani na Ulaya zinahitilafiana katika masuala kuhusu mchakato wa amani ya Mashariki ya Kati, uuzaji wa silaha kwa China na suala la nyuklia la Iran. Marekani inaipendelea Israel katika matatizo ya Mashariki ya Kati na kuiunga mkono katika "mpango wa vitendo vya upande mmoja", ikiona kuwa maendeleo yoyote ya mazungumzo ya amani hayatapatikana bila Palestina kuisambaratisha vikundi vyenye silaha, lakini nchi za Ulaya zinashutumu hatua za Israel na kwa mara nyingi zinataka Israel ibomoe ukuta wa kutenganisha sehemu na kuunga mkono kikamilifu juhudi za Palestina kujenga taifa. Kuhusu suala la uuzaji wa silaha kwa China, nchi za Ulaya zimekuwa na msimamo mmoja na itazamamiwa kuwa katika kipindi cha Luxembourg kuwa mwenyekiti wa zamu zitaondoa kabisa marufuku ya kutoiuzia China silaha. Lakini huku Marekani inazuia kila iwezalo msimamo wa kuiuzia China silaha, ikisema kuwa silaha zitakazouzwa kwa China zitakuwa tishio kubwa kwa Marekani na Taiwan. Kuhusu suala la nyuklia la Iran, Marekani inaona kuwa Iran haitaacha mpango wa kusafisha uranium, msimamo huo unapingwa na nchi za Ulaya. Hizo ni hitilafu kati ya Marekani inayotetea kutenda mambo kwa upande mmoja na nchi za Ulaya zinazotetea kutenda mambo kwa pande mbalimbali pamoja. Uhusiano mzuri kati ya nchi za Ulaya na Marekani uliopatikana baada ya vita vya pili vya dunia umeanza kulegea.
Wachambuzi wanaona kuwa katika kipindi cha pili cha rais Bushi wa Marekani, shughuli za kujaribu kuziba ufa katika uhusiano kati ya Marekani na nchi za Ulaya zitaendelea kufanyika, lakini kutokana na migongano mikubwa uhusiano huo hautaweza kurudi kama hapo awali, bali utakuwa uhusiano unaongozwa na maslahi binafsi wenye ushirikiano na mapambano.
Idhaa ya kiswahili 2005-01-20
|