Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-01-20 20:14:21    
Israel yarejesha mawasiliano na mamlaka ya utawala wa Palestina

cri

    Baraza la usalama la Israel jana liliamua kurejesha mawasiliano na mamlaka ya utawala wa Palestina. Wakati huo, waziri wa mambo ya nje wa Palestina Bw. Shaath siku hiyo alisema kuwa, mwenyekiti wa mamlaka ya utawala wa Palestina Bw. Mahmoud Abbas anatarajiwa kufikia makubaliano na makundi ya wanamgambo wa Palestina kuhusu suala la kusimamisha vita katika muda mfupi ujao. Hali ya wasiwasi kati ya Palestina na Israel iliyokuwepo kwa siku kadhaa hatimaye imeanza kupungua.

    Jana, wajumbe wa baraza la usalama la Israel, wakiwa ni pamoja na waziri mkuu wa Israel Bw. Ariel Sharon, naibu mawaziri wakuu wa nchi hiyo Bw. Ehud Olmert na Bw. Shimon Peres, waziri wa ulinzi wa nchi hiyo Bw. Shaul Mofaz na waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo Bw. Silvan Shalom, walifanya majadiliano kuhusu hali ya hivi sasa ya usalama kati ya nchi hizo mbili, mkutano huo pia uliamua kuendelea kuweka shinikizo kubwa la kijeshi kwa Palestina, ili jeshi la Israel liweze kufanya oparesheni kubwa kwenye ukanda wa Gaza, kama mamlaka ya utawala wa Palestina ikishindwa kuzuia wanamgambo wa nchi hiyo kuishambulia Israel.

    Habari kutoka Israel zinasema kuwa, jana maofisa wa usalama wa Palestina walifanya majadiliano na maofisa wa kituo cha ukaguzi cha Israel kilicho kwenye mpaka wa Israel na ukanda wa Gaza, kuhusu njia ya kuzuia wanamgambo wa Palestina wasishambulie kwa makombora sehemu ya kaskazini ya ukanda wa Gaza.

    Maofisa wa Israel walisema kuwa, sababu za uamuzi wa Israel wa kurejesha mawasiliano na Palestina ni kuwa shinikizo la kijeshi na kisiasa lililowekwa na Israel siku hizi limeanza kuleta manufaa. Kwa upande mwengine, Katika siku za karibuni, mamlaka ya utawala wa Palestina ilifanya juhudi kubwa kuzuia wanamgambo wa nchi hiyo wasishambulie Israel. Bw. Abbas alikwenda ukanda wa Gaza kufanya mazungumzo na makundi ya wanamgambo wa nchi hiyo kuhusu kusimamisha vita; Palestina pia imeunda kikosi maalum cha kuzuia mashambulizi dhidi ya Israel na kupanga kukipeleka kikosi hicho kwenye sehemu ya mpakani mwa Israel na Gaza.

    Lakini wachambuzi wameainisha kuwa, uamuzi wa Israel wa kurejesha mawasiliano na Palestina kwa kiwango kikubwa ni kwa ajili ya kulinda maslahi ya nchi hiyo yenyewe. Israel haiwezi kuboresha mazingira ya usalama kwa mbinu ya kijeshi tu. Ili kupambana na makundi wa wanamgambo wa Palestina, Israel iliwahi kufanya oparesheni za kijeshi mara nyingi kwenye ukanda wa Gaza, lakini mafanikio hayakupatikana. Mashambulizi ya makombora bado ni tishio kubwa kwa makazi ya kiyahudi kwenye ukanda wa Gaza na miji ya kusini ya Israel, na kuifanya serikali ya Israel ibebe lawama kubwa nchini na duniani.

    Aidha, ili kuzuia ukanda wa Gaza kisiwe kituo cha makundi ya wanamgambo wa Palestina baada ya Israel kuondoa jeshi kwenye sehemu hiyo, kwa upande mmoja, serikali na jeshi la Israel linachukua hatua za kijeshi kuwasaka wanamgambo wa Palestina na kuviteketeza viwanda vyao vya kutengeneza silaha; kwa upande mwengine, Israel inatumai kuwa Palestina inaweza kuyadhibiti makundi hayo na kuzuia mashambulizi dhidi ya Israel kwenye ukanda wa Gaza. Wachambuzi wanaona kuwa, ushirikiano wa kiujenzi na Palestina kuhusu kulinda usalama unalingana na maslahi ya kimsingi ya Israel.

    Wakati huohuo, Bw. Sharon pia anakabiliwa na shinikizo kubwa kutoka kwa jumuiya ya kimataifa. Ingawa hali ya wasiwasi ya siku hizo kati ya nchi hizo mbili imeweka vikwazo kwa mpango wa kurejesha mchakato wa amani, lakini jumuiya ya kimataifa bado inatumai kusukuma mbele mchakato huo na kutaka Israel ijizuie na kumpa Bw. Abbas muda wa kutosha kushughulikia migogoro ya ndani ya Palestina na kuimarisha utawala wake. Marekani ilipokubali Israel kusimamisha mawasiliano na Palestina, pia ilisisitiza kuwa inatumai uamuzi huo ni wa muda mfupi tu. Kwa udhahiri, kutokana na mazingira hayo ya kimataifa, si busara kwa Israel kushikilia kukatisha mawasiliano na Palestina.

Idhaa ya Kiswahili 2005-01-20