Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-01-21 16:02:22    
Mgogoro wa uchaguzi wa rais wa Ukraine watulia

cri

    Bunge la Ukraine jana lilipitisha azimio likitangaza kuwa sherehe ya kuapishwa kwa Rais Viktor Yushchenko itafanyika tarehe 23 mwezi Januari. Mgogoro wa uchaguzi wa rais wa Ukraine hatimaye umetulia.

    Uchaguzi wa rais wa Ukraine ulikabiliwa na matatizo mengi. Tarehe 31, mwezi Oktoba mwaka jana, duru la kwanza la upigaji kura katika uchaguzi wa nne wa rais tangu mwaka 1991 lilifanyika nchini humo. Kutokana na kutokuwa na mtu yeyote aliyeshinda moja kwa moja, kwa mujibu wa sheria ya Ukraine, waziri mkuu Bw. Viktor Yanukovych na kiongozi wa chama cha upinzani Bw. Viktor Yushchenko ambao walipata kura nyingi walipaswa kugombea tena nafasi ya urais katika duru la pili la upigaji kura.

    Ingawa tume ya uchaguzi ya Ukraine ilitangaza kuwa Bw. Yanukovych alishinda kwa kura nyingi kidogo katika duru la pili la upigaji kura lililofanyika tarehe 21 mwezi Novemba, lakini Bw. Yushchenko hakukubali matokeo hayo na kuishutumu tume hiyo kwa kukiuka utaratibu katika upigaji kura. Waungaji mkono wa pande mbili walikuwa wakifanya maandamano na mikusanyiko mikubwa na kusababisha hali ya kisiasa nchini humo kuwa mbaya. Baadaye mahakama kuu ya Ukraine ilitoa uamuzi kuwa matokeo hayo hayafanyi kazi na kuamua kufanyika kwa duru la pili la upigaji kura la uchaguzi wa rais tarehe 26 mwezi Decemba.

    Kwa mujibu wa takwimu za tume mpya ya uchaguzi ya Ukraine, Bw. Yushchenko alishinda katika duru jipya la upigaji kura. Upande wa Bw. Yanukovych pia haukukubali matokeo hayo na pande hizo mbili zilianza migongano tena. Baada ya mahakama kuu ya Ukraine kutoa hukumu kadhaa inayomsaidia Bw. Yushchenko, Bw. Yanukovych jana alisema kuwa anakubali hukumu ya mahakama kuu.

    Wachambuzi wanaona kuwa, ingawa mgogoro ya uchaguzi umetulia, lakini Bw. Yushchenko bado atakabiliwa na matatizo kadhaa katika mambo ya ndani na ya nje.

    Kuhusu mambo ya ndani, kuna tofauti kubwa kati ya sehemu ya mashariki na magharibi kuhusu kiwango cha maendeleo ya uchumi na mawazo kuhusu kutokana na sababu za kihistoria. Pia kuna tofauti kubwa katika msimamo wa kisiasa. Mgogoro huo wa uchaguzi  umeonesha tofauti na migongano hizo, na pia umeongeza tofauti na migongano hizo na kusababisha ufarakanishaji zaidi wa kisiasa katika jamii nchini humo. Hivyo baada ya Bw. Yushchenko kushika wadhifa wa urais atakabiliwa na kazi ngumu ya kulinda umoja wa taifa na makabila.

    Kuhusu mambo ya nje, nguvu za nje zimeingilia katika uchaguzi wa rais wa Ukraine. Upande wa Marekani na nchi nyingine za magharibi na upande wa Russia na nchi kadhaa za Umoja wa Jamhuri Huru zilikuwa zikishindana nchini Ukraine ambayo ni nchi muhimu ya Umoja wa Jamhuri Huru na ya Ulaya. Hii imeonesha kuwa katika mambo ya nje serikali ya Ukraine itakabiliwa na chaguo gumu.

    Ingawa Bw. Yushchenko anachukuliwa kuwa ni mwakilishi wa Waukraine wanaopendelea nchi za magharibi, lakini Ukraine na Russia zina uhusiano maalum wa kihistoria na kiuchumi, hivyo uhusiano kati ya nchi hizo mbili ni nyeti na muhimu sana. Russia ni nchi inayoipatia Ukraine nishati, pia ni soko kuu la bidhaa za Ukraine. Uhusiano kati ya nchi hizo mbili ukiwa mbaya, uchumi wa Ukraine bila shaka utaathiriwa na kuhatarisha utulivu wa kisiasa nchini humo.

    Lakini nchi za magharibi hazitaacha maslahi yao na hali nzuri kwao nchini Ukraine. Hali kadhalika, Ukraine pia ina mahitaji ya kuendeleza uchumi wake kwa kutegemea nguvu ya nchi za magharibi. Viongozi wapya wa Ukraine lazima wahakikishe uwiano wa uhusiano kati ya nchi za magharibi na Russia. Hii pia si kazi rahisi.

    Jana Rais Vladimir Putin wa Russia ambaye aliwahi kumwunga mkono kithabiti Bw. Yanukovych alimpongeza Bw. Yushchenko na kusema kuwa, Russia inatoa kipaumbele kwa uhusiano wa ujirani mwema na Ukraine. Alisema kuwa, kuendelea kuimarisha uhusiano wa kiwenzi kunafuata maslahi ya muda mrefu ya wananchi wa nchi hizo mbili. Waziri wa mambo ya nje wa Russia Bw. Sergey Lavrov juzi pia alisema kuwa, Russia inamkaribisha Bw. Yushchenko kufanya ziara nchini Russia kwanza baada ya kushika madaraka ya urais. Alisema kuwa nchi hizo mbili zitaendelea kuimarisha ushirikiano na hakuna chaguo lingine. Bila shaka kitendo hicho cha Russia kinalenga kuwaonesha viongozi wapya wa Ukraine ishara ya wazi ya kuboresha uhusiano. Lakini katika hali ya Russia na nchi za magharibi kushindana nchini Ukraine, kama kuboresha ushirikiano kutaweza kutekelezwa kihalisi bado kunafuatiliwa zaidi.

Idhaa ya Kiswahili 2005-01-21