Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-01-21 15:02:14    
Itambue Afrika na utamaduni wake

cri
Katika ghorofa ya pili ya jengo jipya la "Golden Resources Shopping Mall" mjini Beijing, ambacho ni kituo kikubwa kabisa cha maduka barani Asia, kuna vibanda viwili vinavyouza vitu vya sanaa vya kiafrika na kahawa na miavuli kadhaa iliyoezekwa kwa makuti yaliyoagizwa kutoka nchi za Afrika, ambayo imekuwa kivutio kwenye kituo hicho cha maduka. Wateja wakijisikia uchovu baada ya kutembelea kwenye sehemu mbalimbali katika jumba hilo wanaweza kupumzika kidogo chini ya miamvuli ya makuti, kuagiza kikombe kimoja cha kahawa na kunywa kahawa huku wakiburudika na muziki mzuri, hii ni starehe kweli kweli. Mwandishi wetu wa habari muda si mrefu uliopita alipokwenda kutembelea kituo hicho cha maduka alivutiwa sana na vibanda hivyo, hakuweza kujizuia kumtafuta mwenye vibanda hivyo.

Mwenye vibanda anaitwa Guan Jun, alihitimu kutoka kitivo cha kiingereza cha chuo kikuu cha lugha za kigeni cha Beijing, aliwahi kusoma na kufanya kazi ng'ambo, na anapenda sana vitu vya sanaa na kupenda kunywa kahawa. Kwa kushirikiana na rafiki yake anayefahamu sanaa na utamaduni wa Afrika, Bwana Guan Jun alifungua vibanda hivyo viwili vinavyoitwa "touch Africa", kibanda kimoja kinauza vitu vya sanaa vilivyoagizwa kutoka nchi za Afrika, na kingine kinauza kahawa na keki. Kwa kuwa vibanda hivyo viwili vina umaalum wa kipekee wa kiafrika, huwapa wateja picha nzuri sana ya kukaribia katika mazingira ya kimaumbile, hivyo watu wengi huvutiwa hata wakapiga picha mbele yake.

Bwana Guan Jun alifahamisha akisema: "Vitu vyote vya kisanaa vinaagizwa kutoka nchi za Afrika, kuna vinyago kutoka nchi za Afrika mashariki, vitu vya shaba kutoka nchi za Afrika magharibi, vinyago vya mawe kutoka Afrika ya kusini na Zimbabwe, na vitu vya sanaa vya mikono kutoka Misri."

Mwandishi wetu wa habari aliona kuwa, vitu vya sanaa vinavyouzwa kwenye kibanda hicho vinaweza kugawanywa katika sehemu nne: yaani mapambo ya kale kama vile vya barakoa mask na vitu vilivyotengenezwa na shaba kutoka Benin na Cameroon; vitu vya sanaa, kama vile vinyago vya mpingo na picha za rangi ya maji za "tingatinga"; vitu vya sanaa vya mikono kama vile ngoma, vibuyu, mikuki, pamoja na vinyago vya wanyama; na vitu vya matumizi ya kila siku na mapambo kama vile chesi, kisu cha kukatia karatasi, mikufu ya pembe za ng'ombe, pamoja na bangili.

Japokuwa Bwana Guan Jun hajawahi kufika barani Afrika, lakini anafahamu sana mambo ya sanaa na utamaduni wa Afrika. Alisema:

"Vitu hivyo vya sanaa vinatoka kwenye nchi zaidi ya 20 za Afrika, kati ya vitu hivyo, vitu vyenye umaalum zaidi ni vinyago vya mpingo kutoka Tanzania na Kenya, mpingo ni mti adimu sana duniani na wenye thamani kubwa ya kisanaa. Vinyago vilivyotengenezwa na wasanii wa kabila la wamakonde nchini Tanzania ndivyo vyenye mvuto mkubwa zaidi, wasanii wa kabila la wamakonde hupenda kusimulia historia ya ukoo au kabila kwa kutumia vinyago, baadhi ya vinyago vina urefu mita kadhaa. Bwana Tingatinga wa Tanzania ni msanii maarufu sana wa picha za rangi ya maji, kwa kuwa michoro yake inajulikana sana nchini Tanzania, na hata inapendwa na watu wa nchi za Ulaya, Marekani na Japan, hivyo picha za rangi ya maji za Tanzania huitwa picha za "tingatinga". Umaalum wa picha za "tingatinga" ni kuwa na rangi ya mng'ao na tofauti kubwa za rangi ambazo hugusa mioyo ya watazamaji. Sanaa za Afrika huonesha hisia na mawazo ya wasanii juu ya maisha na utamaduni wa jamii.

Alipozungumzia lengo lake la siku za baadaye, Bwana Guan Jun alisema:

"Mimi naona kuwa tunapaswa kulifahamu bara la Afrika kwa mtizamo mwingine, vitu vya sanaa vya Afrika ni sehemu ya utamaduni wa Afrika, nataka kufungua matawi mengine ya duka langu nchini China ili kuwafahamisha wachina wengi zaidi kuhusu sanaa za Afrika. Aidha kutokana na upendo wangu kwa utamaduni wa kahawa?pia nataka kueneza utamaduni wa kahawa kwa wachina, nitaagiza kahawa kutoka Kenya, Uganda na sehemu nyingine. Japokuwa kahawa ni kinywaji, lakini hubeba vitu vya kiutamaduni, kunywa kinywaji cha kahawa chenye utamaduni wa kisasa chini ya kibanda cha makuti chenye umaalum wa kiasili wa Afrika kutakuwa ni kivutio kikubwa kwa vijana wachina."

Bwana Guan Jun alisema, vibanda vya "Touch Africa" ni dirisha dogo tu, na sanaa ni sehemu ndogo ya utamaduni, aliona kuwa, utamaduni wa Afrika unastahili kufahamishwa kwa wachina. Alisema:

"Licha ya vitu vya sanaa vya mkono, bado kuna vitu vingi vinavyostahiki kuagizwa kutoka nchi za Afrika, kama vile ngoma za Afrika zenye umaalum wa kiasili ambazo haziwezi kuigizwa vizuri."

Licha ya kuingiza utamaduni wa Afrika, Bwana Guan Jun pia anataka kufanya biashara na watu wa Afrika. Alisema kuwa, bara la Afrika lina raslimali nyingi sana, kutokana na maendeleo ya uchumi wa China na nchi za Afrika, uhusiano wa kibiashara kati ya China na nchi za Afrika bila shaka utaimarishwa zaidi. Bidhaa za China zinakaribishwa sana na waafrika kutokana na kuwa na bei nafuu na sifa nzuri, makampuni ya China yamefanya ushirikiano vizuri na nchi za Afrika katika ufugaji wa samaki, kilimo na sekta nyingine, wachina wameshaanza kuagiza bidhaa kutoka nchi za Afrika, kama vile mbao, kahawa na matunda.

Bwana Guan Jun alisema kuwa, sasa ameanza kufahamu mambo ya Afrika, lengo lake lijalo ni kwenda barani Afrika, kujionea mwenyewe mambo ya utamaduni wa kiafrika, kama vile mila na desturi za Afrika, hali ya jiografia, bonde la ufa, maporomoko ya Victoria na mbuga za wanyama pori.

Idhaa ya kiswahili 2005-01-21