Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-01-24 16:37:06    
Mwimbaji Mashuhuri wa Nyimbo za Kikabila Rozi Amuti

cri

Siku moja katika majira ya baridi, tulimtembelea mwimbaji Rozi Amuti nyumbani kwake mjini Beijing. Tulikaribishwa kwa ukarimu, tulikuwa tukisikiliza kanda ya nyimbo alizoimba za kabila lake la Uygur huku tukiburudika kwa chai ya maziwa, tulijihisi kama tuko katika sehemu ya mbali mkoani Xinjiang, magharibi kabisa mwa China.

Mwimbaji Rozi Amuti alitueleza kuwa kwa miaka mingi alikuwa na matumaini kuwa angerekodi nyimbo zake za kabila la Uygur mkoani mwake Xinjiang. Mwezi Oktoba mwaka huu tumaini lake hilo kweli lilitimizwa kwa kuweza kurekodi kanda ya mkusanyiko wa nyimbo za kabila la Uygur kwa jina la "Huko katika Sehemu ya Mbali". Katika mkusanyiko huo amerikodi nyimbo kumi na moja ambazo zote zinaimbwa sana na ndugu zake wa mkoa huo.

Mwaka huu Rozi Amuti ana umri wa miaka 44, na sasa ni mwimbaji katika Kundi la Nyimbo na Ngoma la Kikabila mjini Beijing. Alizaliwa Urumchi, mji mkuu wa mkoa wa Xinjiang, na alipenda kuimba na kucheza ngoma toka utotoni. Alisema, "Sisi watu wa Uygur tuna mila ya kuimba na kucheza ngoma, nilipokuwa mtoto kila tulipokuwa katika sikukuu fulani tulikuwa tunajikusanya pamoja na kuimba pamoja na kucheza ngoma, na nyimbo zote zilikuwa ni nyimbo zinazoimbwa sana miongoni mwa wenyeji. Kutokana na kukua katika mazingira hayo yaliyojaa nyimbo na ngoma, kwa miaka nenda miaka rudi nimekuwa mshabiki wa nyimbo na ngoma."

Rozi Amuti alipokuwa na umri wa miaka 16 alifaulu mtihani wa kujiunga na kundi la nyimbo na ngoma la mji wa Urumchi na kuwa mchezaji ngoma, lakini alijifunza uimbaji katika saa za mapumziko. Baadaye kwa bahati alikutana na profesa mmoja wa uimbaji Bi. Pan Enze, ambaye aligundua sauti yake ina nafasi kubwa kuboreshwa, akampokea kuwa mwanafunzi wake. Kutokana na kufundishwa na profesa huyo, mwaka 1985 Rozi Amuti alifanikiwa kujiunga na Chuo Kikuu cha Muziki cha Shanghai katika kozi ya uimbaji.

Baada ya kuhitimu masomo yake katika chuo hicho Rozi Amuti alirudi nyumbani kwake mkoani Xinjiang na kujiunga na Kundi la Nyimbo na Ngoma la Mkoa wa Xinjiang. Katika kipindi hicho alishirikiana na mtunzi mashuhuri wa nyimbo Bw. Wang Luobin ambaye aliwahi kuhariri nyimbo nyingi za kabila la Wauygur la mkoa wa Xinjiang. Kutokana na kuelimishwa na Bw. Wang alielewa kwa kina nyimbo alizoimba. Rozi Amuti alisema, "Nyimbo za mkoa wa Xinjiang ni za uchangamfu wa kusisimua, midundo yake ni ya haraka, na maeneo yake ni ya kuchekesha. Mtunzi wa nyimbo Bw. Wang Luobin alinisaidia sana kwa kunielewesha kwa kina na namna ya kuziimba nyimbo hizo. Sauti yangu ni ya juu, katika mazoezi ya miaka mingi mtindo wangu wa kuimba pamoja na ngoma umekuwa mtindo wangu wa kipekee."

Mwaka 1994 Bw. Rozi Amuti alishiriki katika mashindano ya kitaifa ya waimbaji wa kikabila, na baada ya mashindano ya raundi kadhaa, mwishowe alitwaa tuzo ya kwanza katika mashindano hayo. Kutokana na uhodari wake, mwaka 1997 alichaguliwa kuwa mwimbaji wa Kundi la Nyimbo na Ngoma la Kikabila mjini Beijing. Hili ni kundi pekee la kitaifa la michezo ya kikabila nchini China ambalo limekusanya wasanii wengi wakubwa wakubwa wa kikabila. Akiwa katika kundi hilo usanii wake uliinuka haraka sana.

Jambo ambalo hawezi kulisahau ni kuwa miaka miwili iliyopita kundi lake lilionesha michezo katika Mkoa wa Tibet ambao unapakana na Mkoa wa Xinjiang. Huu ni mkoa ulioko kwenye mita 3000 juu ya uso wa bahari, wasanii wenzake wengi walijisikia vibaya kutokana na kukosa hewa ya kutosha na walikuwa hawawezi kucheza vizuri kama kawaida yao, lakini Rozi Amuti hakuwa kama wao, nyimbo na ngoma zake ziliwanogea sana watazamaji. Mmoja wa watazamaji bibi mzee mwenye umri wa miaka 80 hata alipanda jukwaani na kumzawadia "hada" yaani kitamba cha hariri nyeupe kikimaanisha heshima na pongezi kwake. Akikumbuka jambo hilo alisema, "Nilipovishwa shingoni 'hada' hiyo nilisikia furaha na faraja kubwa, nikiwa mwimbaji wa kabila langu naona hii ni sifa kubwa kwangu na pia ni msukumo wa kujiendeleza zaidi. Mpaka sasa nalikumbuka wazi."

Tokea mwaka 1997 hadi sasa Rozi Amuti anafanya kazi katika kundi hilo la nyimbo na ngoma la kikabila. Ameacha alama za nyayo zake kote vijijini na mijini nchini China. Kadhalika, katika nyakati tofauti alikwenda kwenye nchi zaidi ya kumi zikiwemo Ufaransa, Ujerumani, Uturuki na Japan, na nyimbo zake zilipokewa kwa shangwe.

Katika maisha yake ya baada ya kazi anapenda kuzungumza na wenzake huku akinywa chai, au kuwaalika marafiki zake kwenda kuangalia sinema na michezo ya sanaa. Kuhusu matumaini yake ya siku za baadaye anasema, anapenda sana maskani yake alikozaliwa, kwa hiyo atarudi mkoani Xinjiang na kuwafundisha waimbaji wengi ili nyimbo za kabila la Wauygur mkoani Xinjiang zijulikane kote nchini China na duniani, na kuufahamisha mkoa wa Xinjiang ulivyo.

Idhaa ya kiswahili 2005-01-24