Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-01-26 16:22:01    
Jumba la unajimu la Beijing

cri
Jumba la unajimu la Beijing ni kubwa kabisa nchini China. Siku chache zilizopita jengo moja jipya la jumba hilo lilifunguliwa kwa umma. Jengo hilo linawavutia watu wengi kutokana na kuwa na chombo cha kitarakimu cha kuonesha filamu za unajimu, na vyombo vingine vyingi vya kisasa. Leo tunatembelea pamoja jumba la unajimu la Beijing.

Jumba la unajimu la Beijing lipo katika sehemu ya magharibi ya mji wa Beijing. Unapoingia kwenye jumba hilo mara utaona jengo nzuri jipya. Unapotazama jengo hilo kutoka nje, utaona mpira mmoja mkubwa na vitu vyenye umbo la ajabu visivyoonekana vizuri nyuma ya kioo kikubwa, hali ambayo inakufanya ujisikie kama uko katika mbingu usiyo na kikomo. Hilo ni jengo jipya la jumba la unajimu la Beijing, lililoanza kufunguliwa kwa kwa umma siku chache zilizopita.

Bw. Andrew Sanders, mtalii kutoka London, alivutiwa na jumba hilo lenye umbo la ajabu na kipekee, alimwambia mwandishi wetu wa habari akisema:

"mimi ni mtalii, jana nilipopita katika jengo hilo nilivutiwa nalo, na leo nimekuja hapa kuitazama, jengo hili ni nzuri sana."

Yenye sifa kubwa zaidi ni ukumbi wa sinema wenye chombo cha kitarakimu ambacho ni cha kisasa kabisa duniani. Mkuu wa jumba hilo Bw. Zhujin alifahamisha kuwa:

"Sio tu mfumo wa kompyuta wa chombo hicho ni wa kisasa kabisa, bali pia mfumo wa projekta yake ni wa kisasa kabisa, tunashirikisha mifumo hiyo miwili kuonesha filamu, matokeo yake ni mazuri kabisa ambayo hayajawahi kuoneshwa mahali pengine."

Filamu iliyooneshwa siku hiyo inaitwa KUTAFUTA UHAI, kadiri sauti ya kipekee kutoka mbinguni iliposikika, watazamaji walijisikia kama wanatembelea mbinguni. Ndani ya sinema hiyo ya mviringo, ukuta na paa ndio kioo, ambacho kinaonesha mandhari ya mbingu, ambapo nyota zinatameta karibu na watazamaji, na dunia inazunguka mbele yao.

Baada ya kutazama filamu hiyo mtalii kutoka Uingereza Bwana Andrew Sanders alisema:

"Ingawa sifahamu Kichina, lakini nafahamu mambo yote kupitia picha nzuri za filamu hiyo. Jumba hili jipya ni zuri zaidi kuliko majumba mengine makongwe ya unajimu katika nchi nyingine."

Ndani ya Jumba hilo jipya kuna kumbi mbili zinazoweza kuonesha filamu kwa vyombo maalum. Ukumbi mmoja unaweza kubembea na kuzunguka, na una viti vinavyoweza kuwafanya watazamaji wajisikie kama wanaanguka kutoka juu. Ukumbi mwingine una vyombo vya kutoa upepo na maji nyuma ya viti, na kupitia chombo cha kuuliza maswali na kupokea majibu, watazamaji wanaweza kuuliza maswali wakati wanapotazama filamu.

Bw. Zhujin alisema anatumai kuwa watu wanavutiwa na unajimu kupitia mazingira yaliyotengenezwa na vyombo hivyo vya kisasa ambayo yanafanana sana na hali halisi ya mbinguni.

Kila ifikapo siku ya mapumziko, watu elfu nne au tano wanakwenda huko kutazama filamu.

Wasikilizaji wapendwa, mbali na filamu, maonesho yanayofanyika katika jumba hilo jipya pia yanawavutia watu wengi. Maonesho yanayofanyika hivi sasa ni maonesho ya mfumo wa jua na sayari zake, makundi ya nyota na historia ya unajimu ya China, miongoni mwa maonesho hayo, jumba la maonesho ya jua ni jumba lenye watu wengi kabisa, ambapo wanaweza kulifahamu jua kwa pande zote moja kwa moja.

Paa na ukuta wa jumba la jua ni anga yenye nyota. Watu wanafahamu mara moja mwundo wa jua kupitia mfano mkubwa wa jua wenye urefu zaidi ya ule wa mtu mzima uliowekwa katikati ya jumba hilo. Na kupitia darubini maalum watu wanaweza kutazama jua la wakati ule moja kwa moja.

Katika jumba la jua, mwaandishi wa habari alikutana na mzee mmoja, Bw. Han, ambaye alimleta mjukuu wake kutembelea jumba la unajimu la Beijing. Mzee huyo alisema:

"Napenda unajimu. Niliwahi kutembelea jumba hilo na kutazama filamu za unajimu miongo kadhaa iliyopita. Niliposikia habari kuhusu kufunguliwa kwa jumba jipya, nimemleta mjukuu wangu kutembelea hapa. Natumai kuwa atavutiwa na unajimu na kufahamu mfumo wa jua na mchakato wa kuumbika kwa dunia kupitia filamu na mifano hiyo."

Jumba la zamani liko katika sehemu ya magharibi ya jumba jipya. Jengo hilo lenye mtindo wa kizamani ni zuri pia, kwa kuwa liko pamoja na jumba jipya, jumba hilo la zamani linavutia zaidi, na jumba jipya linaonekana la kisasa zaidi.

Ndani ya jumba hilo la zamani kuna jumba la sinema lenye viti zaidi ya 600, ambapo filamu mbalimbali zinazofahamisha ujuzi wa unajimu zinaoneshwa kila siku, na maonesho ya sayansi kuhusu unajimu na maonesho ya watu waliotoa mchango mkubwa kwa shughuli za unajimu duniani yanafanyika mara kwa mara. Jumba hilo ambalo lipo kwa karibu miaka 50 limepokea na kuelimisha vizazi kadhaa. Mpaka sasa, watu bado wanatembelea jumba hilo la zamani. Mbali na majumba hayo mawili, jumba la unajimu la Beijing lina kituo cha kale cha unajimu. Vyombo vyingi vya unajimu vilivyotumika zaidi ya miaka 300 iliyopita vimewekwa ndani ya kituo hicho kwa ajili ya maonesho. Vyombo hivyo vinaonesha mafanikio makubwa yaliyopatikana siku za kale nchini China. Aidha, washabiki wa unajimu wanaruhusiwa kutumia darubini wakati hali maalum ya unajimu inapotokea.

Hivi sasa, kutembelea jumba la unajimu la Beijing na kutazama filamu za unajimu, maonesho ya huko, na kujifunza ujuzi wa unajimu kumekuwa ni njia mpya ya wakazi wa Beijing kujionea sayansi na teknolojia.

   

Idhaa ya kiswahili 2005-01-26