Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-01-27 16:20:31    
Wanawake wa China wafuatilia kupunguza mwili

cri

Kutokana na kuinuka kwa hali ya maisha, wanawake wa China wanafuatilia sura zao siku hadi siku. Wanawake wengi wanaona kuwa, mwili mwembamba na wenye afya ni ishara ya urembo, hivyo wanawake wengi zaidi na zaidi wanafuatilia kupunguza mwili wao.

Bibi Liu Lin wa mji wa Chongqian, kusini magharibi mwa China alijifungua mtoto miezi mitatu iliyopita, mwili wake umenenepa zaidi ya alivyokuwa kabla ya kupata ujauzito. Ili kurudi kazini kwa sura mpya, muda si mrefu uliopita Bi. Liu Lin alijiunga na kituo cha kupunguza mwili cha wanawake. Alisema:

"Mimi nilijifungua mtoto muda si mrefu uliopita, nitarudi kazini baada ya miezi kadhaa, hivyo nakuja hapa kufanya mazoezi ya kupunguza mwili ili nijisikie vizuri kama nilivyokuwa hapo mwanzo."

Bi. Liu Lin anakwenda kufanya michezo ya mazoezi ya viungo kila wiki. Kucheza michezo ya mazoezi ya viungo ni njia nzuri ya kupunguza mwili, wanawake wengi nchini China wanapenda kucheza michezo hiyo. Ili kuwarahisishia wanawake waweze kufanya michezo hiyo nyumbani, vituo vingi vya televisheni nchini China kila asubuhi vinatangaza vipindi vya michezo ya mazoezi ya viungo.

Licha ya michezo ya mazoezi ya viungo, wanawake wengi pia wanapenda kufanya mazoezi ya Yoga yanayotoka India na kujulikana duniani kote. Yoga ni njia nyingine ya kujenga mwili. Kwenye ukumbi wa mazoezi ya Yoga, mwandishi wetu wa habari aliona kuwa, wachezaji wakimaliza mazoezi yote ya Yoga, walitumia nguvu kubwa mwili. Hivyo watu wakishikilia kufanya mazoezi ya Yoga wanaweza kupunguza mwili. Bibi Chen Hongjun mwenye umri wa miaka zaidi ya 20 anayefanya mazoezi ya Yoga ni mwembamba na mrembo, alisema:

"Naona kufanya mazoezi ya Yoga kunanifaa sana. Zamani mimi nilikuwa mnene, baada ya kuanza kufanya mazoezi ya Yoga mwili wangu ulianza kupungua. Ninapofanya mazoezi ya Yoga, misuli yangu yote inachezacheza, na ndiyo mwili wangu unapungua kwa ufanisi."

Kutokana na kuongezeka kwa idadi ya wanawake wanaofanya mazoezi ya Yoga, kumbi za Yoga nchini China pia zimeongezeka haraka. Mji wa Beijing una majumba mia moja hivi ya kufanyia mazoezi ya Yoga. Mshauri wa kujenga mwili Bwana Chen Chuan alisema kuwa, tofauti na njia nyingine, kufanya mazoezi ya Yoga kunaweza kunyoosha kila sehemu ya mwili, kunasaidia kuboresha mfumo wa ndani wa kutoa uchafu kwa binadamu. Hivyo umbo la mchezaji litakuwa zuri sana, atakuwa siyo mnene wala mwembamba sana.

Katika miaka ya karibuni, pia imekuwa na njia nyingine ya kupunguza mwili kwa kufanya usingaji (massage) na tiba ya chakula. Watu wanaboresha mzunguko wa kusaga chakula mwilini na muundo wa mafuta mwilini kwa kula chakula maalum na kufanya usingaji ili kupunguza mwili. Bibi Li Wenhua ni mwanachama wa jumba moja la urembo liitwalo National Beauty mjini Shanghai, bibi huyu mwenye sura nyororo na umbo zuri, mwaka mmoja uliopita alikuwa msichana mnene. Alisema:

"Zamani nilikuwa nasikia uchovu kila nikitembea kwa muda, lakini sasa tatizo hilo halipo tena hata kama nikifanya mazoezi magumu. Ili kupunguza mwili, katika mwaka mmoja uliopita nilijiunga na shughuli za kupunguza mwili kwa kula chakula chenye nyuzi nyingi kilichosindikwa kutokana na mboga na matunda, chakula hicho hunisaidia kurekebisha mmeng'enyo wa chakula mwilini. Isitoshe, msingaji anapaka mwili wangu kwa mafuta yaliyosindikwa kutokana na mimea, halafu ananifanyia usingaji kwa dakika 40 au 50 hivi, matokeo yake ni mazuri sana."

Kutokana na kuinuka kwa hali ya maisha ya watu wa China, wachina wengi wanapenda kutumia fedha ili kuwa na umbo zuri la kupendeza na afya njema.

Kutokana na uwezo mkubwa wa soko la kupunguza mwili, Bibi He Xiuhong mwenye umri wa miaka zaidi ya 30 anaendesha klabu ya kupunguza mwili ya wanawake mkoani Zhejiang, mashariki mwa China. Alisema kuwa, licha ya kununua afya katika klabu hiyo, watu wengi zaidi wanaenda huko kwa lengo la kupunguza mwili.

Hivi sasa wanawake wa China wanafuatilia sana kufanya mazoezi, kulala vya kutosha na kula chakula mwafaka ambazo ni sababu tatu za kumudu urembo. Kwa mfano wanajaribu kupunguza nyama na sukari na chakula chenye mafuta mengi, wanapendelea zaidi mboga, matunda na samaki.

Idhaa ya kiswahili 2005-01-27