Uchaguzi mkuu wa Iraq utafanyika tarehe 30 mwezi huu. Tarehe 26 Rais George W. Bush wa Marekani alitoa hotuba kwenye mkutano wa kwanza na waandishi wa habari tangu kuapishwa kwake akitaka Wairaq wengi zaidi wajitokeze kwenye upigaji kura. Wakati huo huo, ofisa wa Umoja wa Mataifa alilaani jeshi la Marekani kuingilia mambo mengi ya maandalizi ya uchaguzi huo na "kufanya juhudi" kupita kiasi.
Suala la Iraq ni jambo linalomsumbua Rais Bush. Si kwa sababu tu serikali ya Rais Bush ilianzisha vita vya Iraq bila ya kujali upinzani wa nchi nyingi, bali pia hali ya usalama nchini Iraq inaendelea kuwa mbaya na askari laki 1.5 wa Marekani hawawezi kujinasua kutoka matope nchini Iraq. Ingawa Rais Bush na maofisa waandamizi wa Marekani wanatumia kila nafasi kutetea vita hivyo, lakini ukweli usiopingika ni kuwa, vita hivyo vina athari mbaya kwa hali ya mashariki ya kati, utaratibu duniani na hata vita dhidi ya ugaidi.
Marekani inataka kujinasua kutoka hali hiyo mbaya mapema iwezekanavyo, kwa hiyo inachukulia uchaguzi huo kama ni "bua lake la kujiokoa kutoka majini". Rais Bush alianzisha vita nchini Iraq kwa visingizio vya Saddam Hussein kuwa na silaha kali na kuwa na uhusiano na kundi la Al-Qaeda, lakini mambo yote yamethibitisha kuwa visingizio viwili vyote si kweli. Hivyo kuisaidia Iraq kujenga nchi yenye demokrasia kumekuwa kisingizio kingine cha kujitetea kwa Rais Bush. Kama uchaguzi mkuu utafanyika kwa mafanikio, inaonekana kuwa Marekani itaweza kupunguza lawama kutoka kwa nchi nyingine kutokana na kuanzisha vita bila ya sababu yoyote.
Katika hali hiyo, Rais Bush alitoa mwito yeye mwenyewe akiwataka Wairaq wengi zaidi washiriki kwenye upigaji kura, na hii ndio imeonesha kuwa Marekani ina wasiwasi kuhusu suala la Iraq. Wasiwasi huo uko katika sehemu mbili. Kwanza, Marekani haina uhakika kuhusu uchaguzi mkuu wa Iraq kuweza kufanikiwa au la. Jeshi linaloipinga Marekani si kama tu linaanzisha mashambulizi dhidi ya jeshi la Marekani na kikosi cha kulinda amani cha Iraq, bali pia linaanzisha migogoro dhidi ya wananchi wa kawaida nchini humo ili kuwazuia Wairaq wasishiriki kwenye uchaguzi mkuu, na kitendo hicho kimekuwa na athari kadhaa. Aidha, vyama muhimu vya madhehebu ya Suni kususia uchaguzi huo kumewatia watu wasiwasi kuwa kama matokeo ya uchaguzi huo yataweza kuwakilisha maoni ya watu wengi.
Pili, Marekani haina uhakika kama itaweza kudhibiti uongozi nchini Iraq. Lengo muhimu la siasa ya serikali ya Rais Bush ni kudhibiti uongozi wa mchakato wa ukarabati wa siasa na uchumi nchini Iraq. Uchaguzi huo utawapatia wananchi wa Iraq fursa ya kutoa maoni yao. Wairaq wengi wamesema kuwa, hawataki kuishi katika hali ya Iraq kukaliwa na jeshi la Marekani, na kutaka jeshi hilo liondoke mapema ili waweze kupata haki ya kujitawala. Hivyo uchaguzi huo utakuwa na matokeo gani, viti 275 katika bunge vitachukuliwa na nani, na kama serikali mpya ya mpito itakubali kuisikiliza Marekani au la kunafuatiliwa sana na Marekani.
Marekani inaonekana kama ni mwenyeji wa suala la uchaguzi mkuu wa Iraq, na inajaribu kujipatia sura ya mwanzilishi wa demokrasia nchini Iraq ili kuweka msingi wa kuendelea kuongoza katika mchakato wa kisiasa nchini humo. Hivyo mkuu wa idara ya kutoa msaada kwa uchaguzi ya Umoja wa Mataifa Bi. Carina Perelli alilaani vikali "juhudi zinazopita kiasi" za Marekani. Alisema kuwa, Umoja wa Mataifa umelitaka jeshi la Marekani lisiingilie kazi ya uchaguzi mkuu, lakini jeshi hilo linajitia hamnazo.
Uchaguzi mkuu ni jambo la Wairaq wenyewe, katika hali ya hivi sasa, kama Wairaq wengi watashiriki kwenye upigaji kura au la itaamuliwa na wao wenyewe. Watu wengine kuingilia jambo hilo kutatia vikwazo uchaguzi huo, na kuathari haki na usawa wa uchaguzi huo.
Idhaa ya Kiswahili 2005-01-28
|