Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-01-28 16:42:16    
Dimba la uchaguzi mkuu wa Iraq lafunguliwa

cri

Tarehe 30 mwezi huu, uchaguzi mkuu nchini Iraq utafanyika tarehe 30 mwezi huu. Huu ni uchaguzi wa kwanza unaohudhuriwa na vyama vingi katika historia ya Iraq. Wapiga kura nje ya Iraq watapiga kura kuanzia tarehe 28. Uchaguzi huo utachagua bunge la mpito la taifa na mabunge ya mikoa zaidi ya kumi na bunge la Wakurd. Huu ni uchaguzi unaofanyika katika mazingira yasiyo ya kawaida ambayo jeshi la muungano la Marekani na Uingereza linaendelea kuikalia Iraq baada ya kuuangusha utawala wa Saddam. Matokeo ya uchaguzi huo yataathiri mchakato wa ukarabati wa siasa nchini Iraq.

Jambo linalozingatiwa zaidi ni bunge la mpito la taifa litakaloanzishwa kutokana na uchaguzi huo. Kuna wagombea 7471 watakaogombea viti 275 vya bunge hilo wakiwa wanawakilisha vikundi 75 vya kisiasa vikiwemo vikundi vya Shia, Suni na Kurd, na miungano 9 ya wagombea na wagombea huru 27. Bunge la mpito la taifa litawajibika kutunga katiba ya taifa na kupendekeza wajumbe wa bodi ya wenyeviti yenye rais na makamu rais wawili na kuunda serikali ya mpito. Kwa mujibu wa azimio la Umoja wa Mataifa Nam. 1546, uchaguzi mkuu rasmi wa Iraq utafanyika kabla ya tarehe 31 Desemba mwaka huu na kuunda bunge na serikali rasmi.

Watu wa Kurd watashiriki kupiga kura katika uchaguzi huo na watachagua bunge la Wakurd. Kuna wagombea wa bunge la Wakurd 463 wakiwakilisha vikundi vya siasa 12 na muungano wa wagombea. Mbali na hayo, watu 7850 watagombea viti vya mabunge ya mikoa.

Kutokana na takwimu, kuna watu milioni 15 wenye haki ya kupiga kura wenye umri kuanzia miaka 18 nchini na milioni 1.2 nje ya Iraq. Hadi sasa idara zinazoshughulikia uchaguzi huo zimeweka vituo 5572 nchini Iraq, na vingine bado havijatangazwa kutokana na hali mbaya ya usalama.

Kwa mujibu wa kanuni za katiba ya muda ya Iraq, uchaguzi huo unafanyika kote nchini bila kugawa sehemu na utatumia daftari moja la majina ya wagombea, na utaamua idadi ya viti vya vikundi vya siasa katika bunge la mpito kutokana na idadi ya kura. Miongoni mwa wagombea walioandikishwa, wagombea waliopendekezwa na waziri mkuu wa serikali ya muda Iyad Allawi, na wagombea waliopendekezwa na rais wa serikali ya muda Gazi al-Yawar na wagombea waliopendekezwa na kiongozi wa madhehebu ya Shia Bw. Ali Sistani ni wagombea wenye uwezo mkubwa zaidi wa kupata ushindi katika uchaguzi huo. Kadhalika, wagombea wa muungano wa Wakurd huenda wakaungwa mkono zaidi na wapiga kura wa Kurd.

Lakini kutokana na kuwa baadhi ya vikundi vya siasa vimetangaza kutoshiriki kwenye uchaguzi huo, uchaguzi huo unatiliwa mashaka kama utakuwa wa kuaminika na kuheshimika. Vikundi hivyo vinaona kuwa uchaguzi huo unaofanyika katika hali ya kukaliwa na nchi nyingine na kutokuwa na usalama hauwezi kuwa wa haki, na ukifanyika kwa lazima hautakuwa na faida yoyote kwa watu wa Iraq.

Hivi sasa, wachunguzi elfu 12 tayari wako nchini Iraq, miongoni mwao 128 wanatoka nchi za nje. Serikali ya muda imewahi kuuomba Umoja wa Mataifa utume wachunguzi nchini humo, lakini kutokana na hali mbaya ya usalama Umoja wa Mataifa haukuitikia. Kabla ya hapo, Umoja wa Ulaya na Russia zilitangaza kutopeleka wachunguzi huko Iraq. Kutokana na kuwa nguvu za uchunguzi wa uchaguzi huo hazitoshi, vikundi vya siasa vina wasiwasi kwamba udanganyifu huenda ukatokea katika uchaguzi huo.

Idhaa ya kiswahili 2005-01-28