Iraq tarehe 30 ilifanya uchaguzi mkuu wa kwanza wa mfumo wa vyama vingi katika historia yake, wapiga kura walikwenda kwenye vituo vya sehemu mbalimbali vya kupigia kura, kuwachagua wabunge 275 wa bunge la mpito la Iraq kutoka vyama 111 vya kisiasa na kuunda serikali ya mpito ya nchi hiyo, ili kumaliza ukaliaji wa Marekani nchini humo kwa njia ya amani na kurejesha mamlaka na uhuru wa nchi hiyo.
Kutokana na sheria ya idara ya uchaguzi ya Iraq, vituo zaidi ya 5000 vilivyopo kwenye sehemu mbalimbali nchini humo vilifunguliwa kwa wapiga kura saa moja asubuhi. Walinzi zaidi ya 5000 walikuwa wapiga kura wa kundi la kwanza, ili waweze kufika kwenye vituo hivyo kwa wakati na kubeba jukumu la ulinzi. Maofisa wa serikali ya muda ya Iraq walikuwa wapiga kura wa kundi la kwanza katika kituo cha kijani mjini Baghdad. Rais Gazi Al-Yawar wa serikali ya muda ya Iraq aliwataka wapiga kura wasiache kutumia haki yao ya kupiga kura na kutoa mchango wao kwa ajili ya kujenga mustakbali wa Iraq.
Kama jinsi ilivyokadiriwa, raia katika mitaa ya waislam wa dhehebu la Shia kusini mwa Iraq na katika mitaa ya Kurd kaskazini mwa nchi hiyo walifululiza kwenda vituo hivyo kupiga kura. Lakini katika vituo vya upigaji kura vilivyoko katika mitaa ya waislam wa dhehebu la Sunni, katikati na magharibi ya nchi hiyo, wapiga kura walikuwa wachache sana. Baadhi ya vituo vilichelewa kufunguliwa kwa saa kadhaa na kufungwa kabla ya saa kadhaa kutokana na kuwa na wapiga kura wachahce. Mji wa Samara ulioko katika sehemu ya pembe tatu ya Sunni ulikuwa na kituo kimoja tu cha upigaji kura. Huko Al-Ramadi, mji mkubwa kabisa ulioko mkoani Al-Anbar, dalili yoyote iliyohusika na uchaguzi haikuonekana, na katika mji wa Tikrit, maskani ya rais wa zamani Saddam, mtu mmoja tu alipiga kura.
Saa kumi na moja alasiri, mwenyekiti wa tume ya uchaguzi huru ya Iraq Bw. Adel Al-Lami alitangaza kuwa asilimia 72 ya wapiga kura milioni 13 nchini Iraq waliojiandikisha walikwenda vituo kupiga kura na idadi ya raia wa Iraq wanaoishi katika nchi za nje na kupiga kura ilizidi laki 1.8.
Ingawa serikali ya muda ya Iraq ilichukua hatua mfululizo za ulinzi kwa ajili ya kuhakikisha uchaguzi huo unafanyika bila vikwazo, lakini haikuzuia mashambulizi yaliyofanywa na watu wenye silaha dhidi ya vituo vya upigaji kura vilivyopo sehemu mbalimbali. Siku hiyo, idadi ya mashambulizi yaliyotokea katika sehemu mbalimbali nchini Iraq ilikuwa kumi kadhaa na kuwaua watu wasiopungua 36 na zaidi ya watu 90 kujeruhiwa. Jeshi la muungano la Marekani na Uingereza pia lilithibitisha kuwa ndege moja ya C130 ya Uingereza ilianguka ardhini na kulipuka katika sehemu ya kaskazini mwa Iraq, sababu yenyewe haijajulikana.
Wachambuzi wanaona kuwa kujitokeza vizuri kwa waislam wa madhehebu ya Shia na wakurd katika uchaguzi huo, hakuwezi kuondoa manung'uniko ya waislam wa madhehebu ya Sunni wanaochukua asilimia 30 ya watu wote nchini Iraq kususia uchaguzi huo. Waumini wa madhehebu hayo wanaona kuwa haiwezekani kufanya uchaguzi wa haki katika hali ya kukaliwa na nchi za kigeni, na ususiaji huo utafanya dhehebu la Sunni liwe katika kando ya mfumo wa kisiasa.
Idhaa ya kiswahili 2005-01-31
|