Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-02-01 15:12:42    

Barua 0201


cri
Msikilizaji wetu Yaaqub Saidi wa sanduku la posta 2519 Kakamega Kenya ametuletea barua kama kawaida yake akianza kwa salamu akitarajia sisi wazima kwa uwezo wake mwenyezi Mungu. Lengo na madhumuni ya kutuandikia barua hii, ni kutoa shukrani zake za dhati kufuatia barua zetu kwake ambazo amezipokea kwa wingi. Hivyo angependa kutuhakikishia kuwa ataendelea kufanya kila juhudi kuwashawishi wasikilizaji wengine kuisikiliza Radio China kimataifa ambayo ni Radio ya jadi yenye kutangaza kote duniani.

Anasema amepitia barua zetu ambazo zimemwezewsha kuwashauri na kuwashawishi mashabiki na wasikilizaji wengi hasa katika mkoa wa magharibi mwa Kenya ambao hawakosi kutuma salamu kwa wenzao kote katika Afrika mashariki. Pili angependa kutoa pendekezo lake kwamba lingekuwa jambo mwafaka iwapo tungefikiria kuwatunukuu na kuwapa zawadi wasikilizaji wa vipindi vya Radio China kimataifa kila mwanzo wa mwaka na mwisho wa mwaka ili kuwapa motisha na hima ya kusikiliza na kushiriki katika mashindano mbalimbali.

Anasema tunaweza kuanza kwa kuwapa zawadi kama fulana, kofia, beji kubwa yenye maandishi ya CRI na zawadi nyingine kadhaa, anadhani pendekezo lake hili litachukuliwa kwa wema, wasikilizaji wa Kenya wangependa kutoa shukrani kwa Radio China kimataifa kwa kushirikiana na idhaa ya shirika la utangazaji la Kenya KBC kutoa matangazo, siku zijazo wasikilizaji wengi toka Kenya watachukua nambari ya kwanza toka kwa wenzao wa Tanzania. Pia anapenda kutupongeza watangazaji kwa kazi yetu nzuri ambayo ni ya kupendeza, hivyo anatuhimiza tuzidi kuwahudumia bila kuchoka na kukoma.

Tunafurahi kuona kuwa hivi karibuni wasikilizaji wetu wa Kenya wameongezeka kwa kiasi kikubwa kuliko zamani kutokana na usikivu mzuri kwa kupitia Kampuni ya KBC, na tunafanya juhudi kuboresha matangazo yetu ya masafa mafupi kwa Afrika ya mashariki, kwani wasikilizaji wetu wa Tanzania ni wengi kwa miaka mingi iliyopita, lakini hivi sasa ni dhahiri usikivu kwa wasikilizaji wa Tanzania na sehemu nyingine za Afrika ya mashariki kwa kupitia matangazo ya masafa mafupi sio mzuri sana, tumetoa ripoti kwa idara husika za Radio China kimataifa, na wameahidi kufanya juhudi kadiri iwezekanavyo ili kuwawezesha wasikilizaji wetu wasikilize vipindi vyetu bila matatizo yoyote.

Msikilizaji wetu Ombeni Urio wa sanduku la posta 36219 Kigamboni Dar es Salaam Tanzania ametuletea barua akisema kuwa yeye ni msikilizaji mwenye kuipenda sana Radio China kimataifa kwani radio hii imekuwa na msaada sana kwake kwani imemwezesha kufahamu sehemu mbalimbali nchini China zinazovutia kwa utalii kupitia tovuti yetu.

Anasema amefurahia sana mandhari nzuri ya China. Ingawa bado hajafika nchini China kuweza kushuhudia moja kwa moja, ila kupitia tovuti nzuri ya kuvutia ya Radio China kimataifa ameweza kujifunza mambo mengi sana. Sio hayo tu bali pia ameweza kujua hali ya kiuchumi ya China pamoja na ushirikiano baina ya China na nchi mbalimbali za kiafrika hususan Tanzania.

Mwisho anapenda kutushukuru sana kwani tunaonesha ni jinsi gani tunavyowajali wasikilizaji wetu, anamwomba mungu amsaidie siku moja aweze kufika na kuiona China, nchi ambayo ina watu wakarimu wanaopenda sana wageni hususan watanzazania, anasema mungu awabariki sana. Pia ameambatanisha picha yake ili tuweze kumfahamu msikilizaji wetu mwema kutoka hapo Kigamboni, Dar es Salaam, Tanzania.

Idhaa ya kiswahili 2005-02-01