Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-02-01 23:15:01    
Wataalamu wa China wazungumzia uchaguzi mkuu wa Iraq

cri

    Uchaguzi mkuu wa Iraq umemalizika tarehe 30 Januari, na sasa umeingia katika siku za kuhesabu kura. Ingawa matukio ya mashambulizi yalitokea hapa na pale lakini yalikuwa machache, na wapiga kura hawakuathiriwa nayo, kwamba kiasi cha 60% ya watu wa Iraq walipiga kura. Hii ni idadi kubwa kuliko ilivyokadiriwa hapo awali. Ingawa matokeo ya hesabu ya kura yatatolewa baada ya siku kumi hivi lakini hali iliyotokea katika siku ya uchaguzi huo imewavutia wataalamu wa China. Yafuatayo ni maoni yao.

    Mtaalamu wa Taasisi ya Uhusiano wa Kimataifa ya China Bw. Li Shaoxian anaona kuwa uchaguzi huo ulifanyika bila matatizo mengi. Alisema, "Uchaguzi huo ulifanyika katika hali ya kuridhisha kwa kiasi fulani kuliko ilivyokadiriwa. Tunaposema uchaguzi huo umefanyika katika hali ya utulivu tunamaanisha mambo mawili. Kwanza usalama haukuvurugwa na mashambulizi. Awali, hali ya usalama ilikuwa inawatia sana watu wasiwasi. Lakini mashambulizi yalitokea machache tu hapa na pale, ambayo hayakuathiri sana uchaguzi huo. Pili, watu wengi walijitokeza kupiga kura, idadi yao inachukua zaidi ya 60%. Hii ni idadi kubwa kuliko iliyokadiriwa. Hali hiyo imedhihirisha mambo mawili: moja ni kuwa watu wa Iraq wanatamani amani ili wapate maisha ya kawaida. Pili, waumini wa madhehebu ya Shia na Wakurd waliokandamizwa kwa muda mrefu na utawala wa Saddam wengi walijitokeza katika upigaji kura. Ingawa waumini wa madhehebu ya Sunni walikuwa wachache lakini sio wachache sana kama ilivyokadiriwa katika upigaji kura huo."

    Kuhusu athari ya uchaguzi huo, Bw. Li Shaoxian aliona kuwa uchaguzi huo pengine utazidi kufarakanisha nguvu za kisiasa nchini Iraq. Alisema, "Hali ya upigaji kura imedhihirisha kuwa madhehebu ya Shia yanaongoza kisiasa nchini Iraq. Hasa vikundi viwili vikubwa vya madhehebu hayo, ni kikundi kinachoongozwa na Ayatollah Ali Sistani na kikundi kinachoongozwa na waziri mkuu wa serikali ya mpito Iyad Allawi. Zaidi ya hayo, hadhi ya Wakurd imeinuliwa. Hali inayotiwa wasiwasi ni madhehebu ya Sunni. Kutokana na kuwa watu wachache wa madhehebu hayo walijitokeza katika upigaji kura huo na baadhi vya vikundi hata vilisusia kupiga kura, hali ya kisiasa ya kutokuwa na uwiano kati ya vikundi vitatu vikubwa vya kisiasa nchini Iraq itatokea, au kwa maneno mengine, mfarakano wa kisiasa nchini Iraq utakuwa mkubwa. Kwa hiyo, namna ya kuunganisha pamoja vikundi hivyo na kukwepa mfarakano huo litakuwa tatizo kubwa baada ya uchaguzi huo. Bunge la mpito na serikali ya mpito litakabiliwa na kazi kuu mbili: Kuimarisha usalama, na kukwepa mfarakano."

    Kuhusu kama matokeo ya uchaguzi huo yanaweza kusababisha vita vya wenyewe kwa wenyewe. Mtaalamu Yin Gang wa Taasisi ya Asia ya Magharibi na Asia alisema kuwa matokeo hayatasababisha vita wenyewe kwa wenyewe. Alisema, "Kutokana na jinsi vikundi vya kisiasa vilivyokuwa katika uchaguzi huo, na kwa mujibu wa uchambuzi wa hali ya jamii nchini Iraq, vita wenyewe kwa wenyewe havitatokea, jamii ya Iraq itakuwa na maafikiano."

    Bw. Li Shaoxian aliongeza kuwa Umoja wa Mataifa na serikali ya muda ya Iraq ilitoa kazi muhimu katika ufanisi wa uchaguzi huo. Alisema, "Kutokana na kuwepo kwa askari laki 1.5 wa Marekani nchini Iraq, kwa hiyo ufanisi wa uchaguzi huo unasaidiwa na askari wa Marekani. Lakini kwa upande mwingine Umoja wa Mataifa pia umetoa mchango mkubwa katika maandalizi kama kuweka tarehe ya kufanya uchaguzi, kuchagua bunge la mpito na serikali ya mpito na kutunga katiba ya kudumu, yote hayo yalipangwa kwa mujibu wa azimio Nam. 1546 la Umoja wa Mataifa."

    Vyombo vingi vya habari vinaona kuwa Marekani imezama ndani ya matope ya vita nchini Iraq, kwa hiyo itaondoa askari wake kutoka nchi hiyo. Mtaalamu Sun Bigan aliona vingine, kuwa Marekani haitaondoa askari wake kabla ya kupata faida yake ya kiuchumi na kimkakati kutoka Iraq. Alisema, "Marekani imepoteza mali nyingi nchini Iraq na watu wake wengi wameuwawa huko. Kwa hiyo wengi wanasema kuwa Marekani imezama ndani ya matope ya vita nchini Iraq. Lakini je hali hiyo inamaanisha kuwa Marekani itaondoa askari wake kutoka Iraq? Kwa makisio yangu, Marekani haitawabakiza askari wake laki 1.5 nchini humo, lakini pia haitaondoa askari wake baada tu uchaguzi kumalizika. Sio askari wake laki 1.5 wa Marekani watabaki Iraq, na sio wote watakaoondoka, bali wataendelea kwa kiasi fulani ili kudhibiti hali ya Iraq na kuipatia Marekani faida za kiuchumi na kimkakati."

Idhaa ya Kiswahili 2005-02-01