Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-02-03 20:22:46    
Kilimo cha China

cri

    Nafaka muhimu za China ni mpunga, ngano, mahindi, maharagwe na viazi. Mpunga ni nafaka muhimu kabisa nchini China, uzalishaji wa mpunga unachukua asilimia 40 ya uzalishaji wa nafaka zote. Mpunga hupandwa katika bonde la Mto Changjiang, sehemu ya kusini mwa China na uwanda wa juu wa Yunnan na Guizhou. Katika miaka ya karibuni mpunga pia umeanza kupandwa kwa wingi katika tambarare za sehemu ya kaskazini mwa China. Uzalishaji wa ngano unachukua asilimia 20 ya uzalishaji wa nafaka zote. Ngano inalimwa nchini kote, na tambarare ya kaskazini ni sehemu muhimu kwa kilimo cha ngano. Uzalishaji wa mahindi unachukua asilimia 25. Mahindi hupandwa katika mikoa ya kaskazini mashariki, kaskazini, na kusini magharibi mwa China. Maharagwe hupandwa katika tambarare ya kaskazini mashariki na tambarare ya kati ya Mto Manjano na Mto Huai. Viazi vitamu vinapandwa katika sehemu kubwa, zikiwemo bonde la Mto Zhujiang, sehemu ya kati na ya chini ya Mto Changjiang, sehemu ya chini ya Mto Manjano na bonde la Sichuan.

    Mazao ya biashara nchini China ni pamoja na pamba, karanga, cole, ufuta, miwa, chai, tumbaku, mforosadi na matunda. Sehemu muhimu za uzalishaji wa pamba ni bonde la Mto Manjano, sehemu ya kati na ya chini ya Mto Changjiang na bonde la Mto Manasi mkoani Xinjiang. Karanga hupandwa mikoani Shandong, Guangdong, Guangxi na Liaoning. Miwa hupandwa katika sehemu ya kusini mwa China.

    China ina mbuga zinazotumika hekta milioni 300. Mbuga nyingi za kimaumbile ziko katika mkoa wa Mongolia ya ndani, sehemu kati ya Mlima Tianshan na Mlima Aertai mkoani Xinjiang na uwanda wa juu wa Qinghai na Tibet. Kuna aina zaidi ya 400 za mifugo wakiwemo nguruwe, ng'ombe, mbuzi, farasi, punda, nyumbu, ngamia, kuku, bata na sungura. Tangu mwaka 1978, kufuatana na maendeleo ya kasi wa ufugaji, uzalishaji wa nyama, mayai, maziwa na ngozi unaongezeka kwa kasi na mauzo ya bidhaa katika nchi za nje pia yanaongezeka.

    Mashirika ya vijijini yalipata maendeleo kwenye msingi wa kazi ya mikono na usindikaji wa mazao ya kilimo. Baada ya mwaka 1978, mashirika ya vijiji yalipata maendeleo makubwa na kuwa uti wa mgongo wa uchumi wa vijijini. Mwaka 1999, mapato ya viwandani ya mashirika ya vijijini yalikuwa yuan trilioni 2.5, na mapato ya mauzo ya bidhaa katika nchi za nje ni yuan bilioni 720. Hivi sasa kuna mashirika milioni 20 ya vijijini ambao yana wafanyakazi milioni 125. Mashirika hayo yanashughulikia utengenezaji wa viwandani, kilimo, usafirishaji, ujenzi, biashara na huduma ya chakula. Bidhaa zinazotengenezwa na mashirika ya vijijini ni pamoja na vifaa vya kilimo, vitu vya mahitaji ya kila siku, chakula, mazao ya kilimo, na bidhaa za viwanda vyepesi. Baadhi ya bidhaa zimeingia katika soko la kimataifa, na kuwa sehemu muhimu ya mauzo ya bidhaa za China katika nchi za nje.

    Kabla ya kutekeleza sera ya mageuzi na kufungua mlango, mazao ya uvuvi yalitegemea maziwa ya asili, mito na bahari za karibu, na uzalishaji wa samaki katika maji baridi na maji yenye chumvi wote si mkubwa. Baada ya mwaka 1978, China ilianza kutoa kipaumbele kwa ufugaji wa samaki na uvuvi katika bahari ya mbali, na uzalishaji wa uvuvi uliongezeka kwa kiasi kikubwa, ambao kwa wastani unaongezeka kwa tani milioni 2 kila mwaka. Hivi sasa China ina makampuni zaidi 20 ya uvuvi katika bahari ya mbali, na pia ina makampuni katika nchi za nje.

Idhaa ya Kiswahili 2005-01-25